Wednesday, January 25, 2017

WAKUU WA WILAYA WATEMBELEA SHAMBA LA JARIBIO LA MAHINDI LA KITUO CHA MAKUTUPORA MKOANI DODOMA

 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Profesa Faustine (kushoto), akizungumza na wakuu wa wilaya za Dodoma na maofisa watendaji na wenyeviti wa serikali za mitaa na wadau wa kilimo  alipotembelea shamba la Jaribio la Mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) chini ya Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (WEMA) katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha  Makutupora mkoani Dodoma leo.
 Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma wakiwa kwenye mkutano na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Profesa Faustine (hayupo pichani), walipotembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutupora mkoani Dodoma leo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi, Bahi, Elizabeth Kitundu, Mpwapwa Jabir Shekimweri na Mshauri wa Kilimo Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba.
 Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Hussein Mansour akizungumza (kushoto), akiwaelekeza jambo Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Dodoma walipotembelea shamba la Jaribio la Mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) chini ya Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (WEMA) katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha  Makutupora mkoani Dodoma leo. Kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu, Kongwa, Deogratius Ndejembi, Mpwapwa, Jabir Shekimweri na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Profesa Faustine Kamuzora.

 Wanahabari, watafiti wa kilimo, wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji wakiwa kwenye mkutano kabla ya kutembea shamba hilo la jaribio la mahindi.
  Wanahabari, watafiti wa kilimo, wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji wakiwa nje ya lango kuu la kuingia katika shamba hilo wakisubiri kupewa taratibu za kuingia.
 Mshauri wa Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (Wema), Dk.Alois Kullaya (kulia), akitoa maelezo kabla ya kuingia kwenye shamba hilo la jaribio la mahindi.
Mtafiti wa Kituo hicho,Ismail Ngolinda (kulia), akitoa maelekezo kuhusu shamba hilo.
Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kushoto), akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya kutembelea shamba hilo. Kutoka kulia ni  Mshauri wa Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (Wema), Dk.Alois Kullaya, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Profesa Faustine, Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Richard Muyungi, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Hussein Mansour na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kanda ya Kati Dodoma, Dk. Leon Mroso.

 Mshauri wa Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (Wema), Dk.Alois Kullaya, akielekeza kuhusu mahindi hayo ya jaribio hilo.
Picha ya Pamoja.


Na Dotto Mwaibale, Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Profesa Faustine Kamuzora amesema utafiti wa kilimo ni muhimu ili kuongeza chakula nchini.

Kamuzora alitoa kauli hiyo alipotembelea shamba la Jaribio la Mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) chini ya Mradi wa Mahindi Yanayostahimili Ukame (WEMA) katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha  Makutupora mkoani Dodoma leo.

Alisema bila ya kuwepo kwa utafiti wa kilimo hatuwezi kufikia ufanisi wa kupata chakula kingi hivyo matokeo mazuri ya utafiti ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo.

Alisema majaribio ya kisayansi ni muhimu na ni mkombozi kwa mkulima hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi na ukame.

Katika hatua nyingine Kamuzora aliwataka wakuu wa wilaya na watendaji na wenyeviti wa serikali za mitaa wa mkoa wa Dodoma waliotembelea shamba hilo kuwa mabalozi kwa wananchi wao kwa kile walichokiona kwenye shamba hilo la majaribio. 

Aliomba kuwepo na subira wakati utafiti huo ukiendelea na kusubiri kuthibitishwa na vyombo vyenye dhamana na kama wataona unafaa basi utatumika.

" Utafiti haufanywi kwa siku moja na kuanza kutumika una mlolongo mrefu ili kutoa nafasi kwa vyombo husika kuona kama upo salama na kuruhusu kutumika" alisema Kamuzora
Alisema vyombo vyenye dhamana vikiridhika vitatoa kibali cha kuanza utumiaji wa teknolojia hii mpya licha ya nchi nyingine za wenzetu kuanza kuitumia,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi alisema ni muhimu sasa kuharakisha matumizi ya teknolojia hiyo badala ya kupoteza muda mwingi ukizingatia kuwa hivi sasa nchi inakabiliwa na ukame hasa katika wilaya yake.

"Kazi inayofanywa na watafiti wetu ni nzuri ila nawashauri wafanye utafiti utakaosaidia katika kipindi hiki cha  mabadiliko ya tabia nchi yaliyopo maeneo mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwawa Jabir Shekimweri alisema utafiti huo umeonesha mafanikio makubwa hasa pale unapoyaangalia mahindi yaliyotumia mbegu iliyotokana na teknolojia hiyo kuwa ni bora na makubwa wakati yale yaliyotumia mbegu za kienyeji kuwa dhaifu.

"Nisema kuwa mbegu za utafiti huu zitakapoanza kutumika zitasaidia sana wakulima hasa wa wilaya yangu ambayo inakabiliwa na ukame katika baadhi ya maeneo" alisema Shekimweri.

No comments: