Kiwanda kinacholalamikiwa na wakazi wa Mwanagati ambacho kimejengwa katika makazi ya watu kikiwa kimezungushiwa fensi ya ukuta.
|
Wananchi wa Kitunda
Mwanagati waishio Block 5 na 6 wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya
Kansa na Kifua kikuu kutokana na uwepo
wa Kiwanda cha kuyeyusha taka za plastiki kilichojengwa katika eneo hilo
ambalo ni makazi ya watu kwa takribani miezi mitano sasa.
Kiwanda hicho ambacho
kimejengwa katika viwanja namba 133 na 135 block 5 kimekuwa ni tishio kubwa kwa
afya za wakazi wa maeneo yanayozunguka na yale yaliyo jirani na kiwanda hicho kutokana
na kuzalisha harufu mbaya na kali inayochafua hewa (air pollution) hali ambayo
imesababisha baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kulalamika kuanza kuathirika na
hali hiyo kwa kuugua kifua, tumbo, kichefuchefu na kupungukiwa hamu ya kula.
Wamedai kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikifanya kazi mchana
kutwa na usiku na wakati mwingine kinafanya kazi mpaka usiku kucha mpaka
asubuhi. Mbali ya kuchafua hewa kiwanda
hicho kimekuwa pia kikisababisha makelele hususan kwa wale walio jirani kabisa
na kiwanda hicho na kuwafanya kushindwa kupumzika vizuri majumbani mwao.
“ Kiwanda hiki kinahatarisha sana afya
zetu kwani kinasabisha tuvute hewa chafu
na mbaya sana kiasi ambacho familia zetu
zimeanza kuugua, tunanyemelwa na magonjwa ya kansa na kifua kikuu ” alilalamika
mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Onesmo.
Naye mkazi mwingine
jirani na kiwanda hicho Bw. Solomoni Mbalaje alisema hali ni mbaya sana kwani
mke wake kwa sasa ni mgonjwa na kutokana na harufu kali inayozalishwa na
kiwanda hicho hatoki nje badala yake amekuwa akishinda ndani tu. Amesema kuwa mmiliki
wa kiwanda hicho ambaye haishi Mwanagati huleta malori yaliyojaa takataka za plastiki kama vile chupa za maji
na mifuko ya plastiki iliyotumika kutoka maeneo mbalimbali hapa Dar es salaam
na mikoani na kuyayeyusha kiwandani hapo.
Taarifa zinasema kuwa
wakazi wa maeneo hayo ya block 5 na 6 walifikisha malalamiko yao katika ofisi
ya Serikali ya Mtaa wa Mwanagati ambapo baada ya kikao cha pamoja na mmoja wa
wamiliki wa kiwanda hicho ilibainika kuwa hawana kibali cha Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira –Nemc na hawana pia hati ya Wizara ya Ardhi
ya kubadilisha matumizi ya eneo hilo kutoka makazi kuwa kiwanda. Hata hivyo
Serikali ya mtaa wa Mwanagati ilishindwa kushughulikia suala hilo na kuamua
kulipeleka kwa Mtendaji wa Kata ya Mzinga ambako mpaka leo hakuna hatua yeyote
iliyochukuliwa.
Aidha wakazi wa maeneo
hayo wanadai kuwa wamepeleka malalamiko yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la
Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kwamba bado wanasubiri kupata
majibu kabla ya kuamua ni hatua gani zaidi wachukue.
No comments:
Post a Comment