Saturday, March 25, 2017

Hotuba ya Anna Mghwira maazimisho ya Azimio la Arusha


MKUTANO WA KIDEMOKRASIA, ARUSHA


MARCH 25, 2017
  
MADA:  UZOEFU WA KUNADI SERA ZA KIJAMAA KATIKA MAZINGIRA YA UBAPARI UCHWARA:

Mama Anna Elisha Mghwira,
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo.


Ndugu wananchi wote
Wageni Waalikwa,
Viongozi wa ACT WAZALENDO,
Mabibi na Mabwana.


Salamuni wote.

Kutetea sera za ujamaa katika kipindi cha ubepari uchwara ni kwendakinyume na nyakati.

Mwaka 2015 tulipotetea sera hizi, tuliona majibu ya baadhi ya watu katika jamii yetu juu ya kushindwakwa ujamaa, kuporomoka kwa ukomunist Urusi na udikteta wa China chini ya serikali ya Kikomunist.

Hatukupata majibu ya kushindwa kwa ubepari na kwa ubepari uchwara hapa kwetu. Kwa kawaida wanaopinga ujamaa huwa hawaji na hoja za kutosha za ubepari na faida zake kwa raia wa kawaida, wafanya kazi na wachuuzi wadogo. Kwa hiyo tunapojadili jambo hili tunajikuta kukutana na ombwe la hoja juu ya kushindwa kwa ubepari uchwara kama ambavyo ujamaa nao umeshindwa.Kwa hitimisho tumesema kila wakati turudi kwenye misingi.

Ni fedhehakwaWaafrika kudai chochote katika dhana hizi mbili: ujamaa na ubepari. Kwa sababu ukiacha ujamaa kama dhana ya udugu na ushirikiano, ubepari wa aina yoyote haukuwa na mizizi ya kukomaa mpaka ujio wa wageni walowezi katika bara hili.

Kwa upande mwingine pia Waafrika hawajawa na mchango wa kihistoria katika mifumo ya dunia. Wamechukuliwa na mawimbi ya utumwa, ukoloni, ubepari na ubepari mambo leo. Hatujaandika kilicho chetu bado. Mpaka sasa sisi tunaandika maisha yetu kulingana na watu waliokuja katika maisha yetu na si jinsi sisi wenyewe tulivyo.

Hii ni changamoto kubwa katika kujadili maada hii. Kwa hiyo ninapenda kujikita katika kuangalia namna ambavyo Mwafrika wa asili angetaka kujulikana  kama angeamua hivyo. La kwanza Mwafrika wa asili angekuja kuzungumza nasi kwa lugha yake ya utoto: Kinyakyusa, Kimakonde, Kihaya nk. Kiswahili bado ni lugha ya matokeo na si lugha ya asili. Ni lugha ya pili ama ya tatu kwa wengi wetu. Pili mwafrika huyu ama Mtanganyika (nalo si jina la asili ) angelielezea anakotoka kama taifa lake: Wamasai ni taifa, Wabarbaig ni taifa, Warimi nao ni taifa. Mataifa haya yalikuwa nchi kamili zenye muundo wa utawala ulioheshimu watu wake, lugha na taratibu zingine.

Kulikuwa na mahusiano mazuri na mabaya kati  ya makabila. Kulikuwa na vita pia za kikabila na kitaifa cha wakati ule. Kulichukuliwa wanawake wa Kiiraq mateka na Wabarbaig kwa mfano. Mtemi Sarwat wa Wairaq alipigana na Wabarbaig na mpaka leo kuna semi zinazoashiria utamaduni huu. Hii ndio asili yetu. Tukiichunguza vizuri inafanana na jamii zingine duniani.

Kisichofana na utu ni tabia iliyoingia ya mataifa ya mbali kuja kwetu na kujipa ukuu, wa kiuchumi, kisiasa na kijamii dhidi ya watu weusi na kwa sababu ya matumizi ya nguvu wakafanikiwa kutwaa nchi zetu na kuziweka chini ya himaya zao kwa muda mrefu.

Wajerumani ndio walioanza kutuunganisha si kwa sababu ya kutaka tuungane bali kwa sababu ya kutaka kuwa na kundi la kazi ( work class) linaloshabihiana na ambalo ingekuwa rahisi kulitawala. Kiswahili kikashika kasi wakati ule pia kwa uwepo wa lugha za mwambao zilizoshabihiana na Kiswahili. Waingereza hawakujali umoja huu. Wao waliwagawa watu ili iwe rahisi kuwatawala. Na kwa hiyo lugha za makabila na ukabila zilirudi tena, bila unafuu katika kujiunda kama mataifa na kama taifa moja ndani ya nchi na ndani ya bara zima.

Ubepari uchwara ni matunda ya mfumo wa ukoloni. Leo ni kipenzi cha nchi nyingi za afrika bila falsafa na siasa zinazoujenga mfumo huu.

Maana ya ubepari uchwara ni nini hasa:  Maana yake halisi ni utambulisho wa kundi la jamii katika mfumo wa kibaguzi linaloundwa na wakulima wadogo (peasants), na kwa kiwango kikubwa wafanya biashara / wachuuzi wadogo.

Historia ya maendeleo ya Ulaya inawaelezea hawa kama chimbuko la siasa zinazopingana na kundi la mabepari halisi wanaomiliki njia kuu za uchumi, ambazo mabepari uchwara wadogo kiuchumi wanalitegemea kwa kuuza nguvu kazi yao kujipatia maisha. Kiutamaduni mabepari uchwara hawaupendi ubepari halisi kwa ababu unawanyonya lakini huiga kwa kila namna na kutaka sana kuwa kama kundi hilo. Kwa mantiki hii, dhana ya ubepari uchwara inahusisha maendeleo ya vitu katika mfumo wa kisiasa unaowanyima fursa ya kumiliki njia kuu za kiuchumi.

Kundi hili ndilo pia baadae lilibadilika na kuwa daraja la kati katika mfumo wa ubaguzi wa kiuchumi na kisiasa. Wanafalsafa kina Marx na Lenin waliuelezea vizuri mfumo huu. Mahusiano kati ya kundi hili la raia na kundi la mabepari ndilo lililozaa aina ya siasa za ujamaa na ubepari barani ulaya na hata Marekani ambayo raia wake wa sasa wengi ni kutoka mataifa ya Ulaya.

Katika mfumo wa ubaguzi, mabepari uchwara walidharauliwa na mabepari halisi. Mfumo wa dini nao ulionekana kupendelea ubepari halisi na kwa hiyo mafundisho ya dini yalielekeza laana kwa kundi hili kama kundi lililoachwa na Mungu. Ilidaiwa kuwa tabia ya ubepari uchwara haibadiliki hata mtu akiwa na cheo kikubwa kama cha uwaziri mkuu. Katika nchi za ufalme kama Uingereza na Uholanzi, waziri mkuu ndiye Kiongozi wa serikali na mwenye nafasi ya juu. Hata hivyo ikitokea alitokana na kundi la mabepari uchwara, alidharaulika vile vile kwa asili yake.

Mabepari uchwara walionekana kama watu wasio na malengo, wasio na mipango ya muda mrefu na wategemezi. Kundi hili ndilo pia lililozalisha siasa za kijamaa likitafuta usawa na kundi la ubepari halisi.

Licha ya kudharaulika kwake, mabepari uchwara ndio waliojenga  hoja za kujenga mfumo wa huduma  za kijamii bure kwa jamii. Kwa mfano inafahamika kama kundi lililohudumia wajane, na masikini wa chini yao. Ndio pia waliokuwa wabunifu wa mifumo ya kijamii, maeneo ya starehe, upashanaji habari na umbeya ulioambatana nao, na kuunda makundi ya kijamii ya kusaidiana.  Tunaweza kufupisha historia hii kwa namna hii. 
Huu ndio ubepari uchwara: ubepari unaotamaniwa na watu wasiomiliki njia kuu za uchumi. Aina hii ya ubepari unafanana sana na kiwango cha maendeleo tulipo leo Tanzania. Tofauti ya ubepariuchwara wa Ulaya na wa hapa kwetu ni kuwa wa wenzetu una mzizi ya historia ya mataifa yao, na historia ya maendeleo yao kiuchumi na kisiasa.
Ubepari uchwara wetu hauna mizizi. Unaelea katika ya wimbi la umasikini wa fikra mbadala na hali halisi. Kwa sehemu ni kama tuna bahati kuundiwa mifumo na watu wengine na sisi kupata fursa ya kuchagua mfumo wa kufuata ama kuacha. Kwa sehemu ni hasara kwa sababu asili ya utu inataka uzoefu wako uzae matokeo yake.
Kwa sababu hii bila wengi wetu hapa ni hawa mabepari uchwara wanaotamani ubepari halisi. Azimio la Arusha la kuweka mipango ya maendeleo na maisha yetu haina maana tena. Dhana rahisi za kuletewa zilizofanyiwa kazi na watu wengine ndizo tumezipenda.
Kwa sababu hii hatuwezi kudai kuwa na uzoefu wa kutosha kuzitangaza sera hizi. Hata hivyo mwaka 2015 tulijaribu kuzitangaza tena na matokeo yake tuliyaona. Watu wengi walipenda kiwango cha uchambuzi na ufafanuzi. Kwa kuwa hakukuwa na mbadala wa hoja inawezekana watu walipenda kwa kukosa mbadala. Inawezekana pia kuwa walipenda kwa uhaisia wake.
Hata hivyo, msingi wa ubepari ni uchumi na siasa inayotetea uchumi huo. Wakati wa kampeni za marekani tuliona jinsi ambavyo mfumo wa kibepari  ulivyoshabihiana hata miongoni mwa wagombea wa itikadi tofuati. Mama Clinton hakuwa tofuati na Trump katika msimamo wao juu ya ubepari na misingi yake. Walitofautiana katika uwezo wa uwasilishaji. Hii iliacha ombwe la hoja kama ilivyotokea kwetu mwaka 2015.
Hapa niseme hivi kuwa siasa ni muhimu sana katika kujenga uchumi. Kila mrengo wa kiuchumi una siasa zinazoujenga ama kuubomoa. Hiki kitu kinakosekana kabisa hapa kwetu.  Nyakati za uchaguzi ndizo pia ni nyakati za kuwambia raia sisi ni nani na tunataka nini kwa maisha ya raia wetu.
Katika kuuza sera zetu  pia msingi mkuu wa hoja zetu ulikuwa uchumi. Tulitaka na bado tunataka uchumi wetu umilikiwe na wananchi kupitia mfumo shirikishi wa utawala. Tulitaka na badotunataka kuona serikali ikisimamia njia za uchumi.
Tulitaka sana mabadiliko makubwa katika kukuza uchumi wa viwanda utakaotokana na kilimo.  Kwa hiyo mkazo wetu ungekuwa kuimarisha kilimo cha wakulima wetu wadogo, Nyerere aliwaita peasants…aina ya mabepari uchwara masikini kabisa, wasio na kitu sipokuwa nguvu zao dhaifu.
Udhaifu wa masikini wa Tanzania na afrika unaongezwa na kukosekana kwa siasa zinazolenga kujijenga katika maisha halisi ya watu. Hakuna ushindani wa kisiasa katika hili. Kuna ushindani wa majina, wa vyama na hali ya hewa chafu wakati wa uchaguzi. Hakuna dhamira ya kweli ya kujenga nchi na kuitoa katika makucha ya ubepari halisi na ubepari uchwara unaotafuta kuiga ubepari halisi.
Kwa hiyo kwa mfano sasa tunaposikia uchumi wa viwanda bila kilimo, tunajiuliza utawezekanaje? Tunaposikia uchumi wa viwanda bila siasa inayoelezea malengo haya, tunajiuliza itakuwaje? Maswali ni mengi kuliko majibu lakini mwisho wa siku ni huyu mkulima mdogo anayeumia na kwa kuwa hawa ni wengi maumivu yake ni makubwa pia.
Kwa hiyo uzoefu tu wa kunadi sera hizi hautoshi, hautoi jawabu na haujibu maswali ya watu juu ya hali zao kiuchumi, kijamii na kisiasa. Tunahitaji kwenda mbali zaidi ya kunadi sera.Tungependa kuona mijadala ya bunge ikilenga mambo haya pia. Tungependa kuona mikutano ya kisiasa ikizungumzia hoja hizi na kuzioanisha na itikadi zinazotetea amakupinga hoja hizi.
Kukosekana kwa aina hii ya mifumo katika siasa zetu inatulazimishia ufukara wa kisiasa na kuzuia ubunifu ambao ungetokana na mijadala na mipango mbadala. Kwa upande wetu tumetoa mchango wetu katika eneo hili. Tumethibitisha kuwa ubepari uchwara upo Tanzania na unafanya kazi. Ubepari halisi umeimarika kwa mkono wa utandawazi na uwekezaji.
Sasa tuna mabepari halisi na mabepari uchwara kwa pamoja. Kinachopungua kwetu nisiasa za kila mrengo na vyaa kjipambanua hivyo. Kuna haja ya mabepari uchwara kuja na siasa zinazogusa maisha yao kupinga ubepari halisi na kulea tabia ya kuhoji mifumo hii inavyofanya kazi.
Ina tija kuendesha siasa za namna hii na kuleta ushindani wenye masilahi kwa taifa. Kwa hiyo ni wajibu wetu kuendelea kuonesha kwa vitendo jinsi mfumo wa ujamaa wa kidemokrasia unavyoweza kuleta unafuu kwenye maisha ya watu.
Kuna mambo ya msingi ya kufanya ili kufikia lengo hili. Kwa mfano umiliki wa ardhi. Wananchi wanaoishi vijijini kwenye maeneo ambayo yamemilikishwa wageni ni lazima wajue hatimayao. Haiwezekani sharia inayotungwa Tanzania impe unafuu mgeni anayekuja kuwekeza kwa muda na kumnyimakabisa haki mwenyeji mmiliki halisi wa ardhi hiyo kwa kigezo cha hati.

Pili mfumo wa uzalishaji kiuchumi unaotegemea kilimo na ufugaji uwekewe mazingira rafiki ya uzalishaji wa ndani kwa mauzo ya ndani na nje. Katika ubepari halisi wakulima na wafugaji wanaendesha shughuli zao kwa ushindani bila bughdha, lakini sisi tumeshindwa kuweka utaratibu wa kuwawezesha hawa kufanya kazi zao kwa ufanisi. Matokeo yake imesababisha migogoro na uhasama mkubwa miongoni mwa makundi haya.

Tatu ni kuhakikisha sekta zote za uchumi zinalenga na zinaleta athari chanya za moja kwa moja kwa mwananchi. Hizi ni pamoja na utalii, misitu, uvuvi, na usafirishaji.

Kwa ujumla mjadala wa azimio la arusha / tabora baadae na muktadha wa maendeleo ya Tanzania umekuwa kama dhima iliyokosa wachezaji.[1] Sisi tunafikiri dhima hii ina tija na inahitaji kuendelezwa. Tuweke mikakati ya kuushawishi umma kuwa inawezekana kulihuisha azimio la arusha na kuendana na Azimio la Tabora.

Kwa hili tulipanga kutoa heshima zetu Arusha kwa historia yake na mchango kwa siasa za Tanzania na Afrika Mashariki. Arusha imekuwa mleziwa mabadiliko ya aina mbalimbali tangu wakati wa ukoloni hadi na wenyeji asili wa mji na mkoa huu. Hongera kwa watanzania wote kwa kuunga mkono mabadiliko ya aina mbalimbali yaliyoasisi taifa letu.

Asanteni kwa kuitikia wito wetu na kwa ushiriki mzuri.

Mungu Ibariki Arusha, Ibariki Tanzania na Afrika.

No comments: