Hotuba ya Arusha
Nafasi ya Ujamaa wa Kiafrika katika Uchumi wa sasa
Kumbukizi ya Miaka 50 ya Azimio la Arusha
Ndg. Zitto Kabwe
25 Machi 2017
Viongozi wenzangu wa Chama cha ACT- Wazalendo,
Ndugu Waalikwa Wote,
Mabibi na Mabwana,
NI furaha iliyoje kwangu, na kwa chama chetu –kwamba leo tunakutana katika mji ambao Januari mwaka 1967, wazee wetu waasisi wa Taifa letu walikutana kwa muda wa wiki moja na ilipofika Februari 5 mwaka huo, walitangaza Azimio la Arusha. Miaka 50 baadaye, bado tamko hili la Arusha ni mjadala mkubwa hapa nchini, Afrika na duniani kote.
Profesa Issa Shivji, mmoja wa wasomi maarufu nchini na Mkurugenzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere analiita Azimio hilo kama Waraka wa kimapinduzi –akiuleza kwa maneno kuntu kuwa, nanukuu “ bila shaka, Azimio lilikuwa waraka mojawapo wa kimapinduzi ulioandaliwa na kutekelezwa barani Afrika”. Maneno “ tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha” ni maneno ambayo yaliimbwa na kila Mtanzania mnyonge na mpaka leo bado yanarindima ndani ya mioyo yetu.
Azimio la Arusha ilikuwa ni nyaraka ya kwanza ya Mwafrika kutaka kushika hatma ya maisha yake na kuonyesha dunia kuwa Ujamaa wa Kiafrika unaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii. Hakuna nchi nyingine ya Kiafrika ambayo iliweza kuhamasisha raia wake katika kuelekea kushika hatma ya nchi zaidi ya Tanzania kupitia Azimio la Arusha. Azimio la Arusha liliegemezwa kwenye misingi mikuu ya Usawa, Utu na Umajumui wa Afrika na ulishikiliwa na nguzo ya Mfumo Jumuishi wa Uzalishaji. Hivyo Serikali iliamua kumiliki njia kuu za Uchumi za uzalishaji, usambazaji na ugawaji wa mali zizalishwazo. Kwa maneno machache, naweza kusema kwamba katika miaka 50 ya kuwepo kwake, Azimio lilitekelezwa vema ndani ya Tanzania katika miaka yake 25 ya kwanza na kuwekwa pembeni katika miaka 25 ya mwisho.
Azimio la Arusha Vs Azimio la Tabora
Juni 13 mwaka 2015, ACT Wazalendo kilizindua Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha. Katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama tuliweka nia ya kufanya tathmini ya miaka 25 ya Azimio la Arusha na miaka 25 ya bila Azimio. Tulisema “ ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa mwaka 2017 tunaadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha”. Leo tupo Arusha kufanya hilo. Tutasikia mada mbalimbali za wasomi wetu na wazee wetu walioliishi Azimio na kufanya kazi wakati wa Azimio na baada ya Azimio. Pia tutawasikia wanachama wa chama chetu na wananchi wengine wakijadili kwa uwazi katika kujitazama huku. Nia ya chama chetu sio kulibeba Azimio zimazima, la hasha, ni pamoja na kulikosoa pale tunapoona kuwa hapakuwa sawa. Ni muhimu ikafahamika kwamba, Azimio la Arusha ni nyaraka inayoishi na wala Azimio la Tabora halikuja kulitengua bali kuliimarisha.
Ujamaa na Utekelezaji wake
Watu wengi hutafsiri Ujamaa kwa mitazamo yao na kwa kweli kila nchi huweza kutafsiri Ujamaa kwa namna inayoona inafaa na kwa kulingana na mazingira yake. Lakini misingi ya Ujamaa ni ileile – nadharia ya kuendesha jamii kwa misingi ya njia kuu za uzalishaji, usambazaji na mgawanyo kumilikiwa ama kusimamiwa na jamii yenyewe. Msingi wa Siasa ya Ujamaa kwenye Azimio la Arusha ni KUPINGA UNYONYAJI. Kwamba “Nchi yenye Ujamaa ni nchi ya Wafanyakazi: haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbili za watu; tabaka la chini la watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi”. Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha nalo msingi wake wa kwanza ni HAKUNA UNYONYAJI. Kwamba “ Nchi yenye Ujamaa wa Kidemokrasia haina unyonyaji maana kila mtu huwajibika kufanya kazi na kupata malipo anayostahili kulingana na kazi yake”. Katika Azimio la Tabora, tulisema kwamba Serikali kupitia sera za kodi inapaswa kurekebisha tofauti ya kipato kati ya walionacho na wasionacho. Katika Azimio la Arusha imetamkwa kuwa “ kila mfanyakazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbalimbali hayapitani mno”.
Katika msingi huu wa usawa utaona kuwa lengo ni kupambana dhidi ya tofauti kubwa ya Mapato (Inequality ) miongoni mwa wananchi. Ujamaa wa Azimio la Arusha unataka pasiwe na tofauti kubwa ya mapato na Azimio la Tabora linaeleza kinagaubaga kuwa ni wajibu wa Serikali kurekebisha tofauti hizi kwa njia za kikodi na sera za nchi. Tutarudia dhana hii ya ‘inequality’ baadaye kidogo.
Ndiyo maana, mimi ni mmoja wa watu wanaomshangaa sana kiongozi wetu wa nchi kila ninapomsikia akisema lengo lake ni kuwafanya wanaoishi kimalaika waishi kama mashetani. Kauli hii, kwangu mimi, ni ishara kufilisika kiitikadi ( ideological bankrupt ) kwa sababu lengo lapaswa kuwa kuwanyanyua wale wanaoishi kishetani ili waishi kama wanadamu na wale wanaoishi kimalaika waishi kama wanadamu pia. Mfumo wa kibepari kiasili una watu wengi wanaoishi kama mashetani, wachache wanaoishi kama binadamu na wachache zaidi wanaoishi kama malaika. Anayetamani watu wote waishi kishetani sio mjamaa na wala si bepari bali ni Mufilisi kiitikadi.
Msingi mwingine wa Ujamaa ni Njia Kuu za Uchumi kuwa chini ya wakulima na wafanyakazi “ kwa kutumia vyombo vya Serikali yao na Vyama vyao vya Ushirika” kwa mujibu wa Azimio la Arusha. Hii ndio iliyosababisha utaifishaji mkubwa uliofanywa na Serikali baada ya Azimio kutangazwa. Katika Azimio la Tabora tulisema “Ili kumilikisha uchumi kwa wananchi, Serikali ilitaifisha mabenki, migodi, kampuni za bima na biashara nyingine mbalimbali za ndani na biashara ya nje. Katika kipindi hiki pia serikali ilijenga viwanda mbalimbali hususani viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo kama vile viwanda vya nguo ikiwemo viwanda vya kuchambua pamba, viwanda vya nyuzi na nguo. Jumla ya viwanda 12 vya nguo vilijengwa nchini na kuzalisha maelfu ya ajira kwa wananchi. Serikali pia ilianzisha viwanda vya ngozi, vya kubangua korosho, vya kuzalisha sukari, vya kubangua na kusaga kahawa, vya kamba za katani na magunia ya katani na kadhalika. Serikali pia ilijenga viwanda vikubwa viwili vya kutengeneza vipuri. Kimsingi mpaka mwaka 1978, kabla tu ya vita vya Kagera, nchi yetu ilikuwa katika hatua ya ‘take-off’ kama wachumi tunavyoita. Waasisi wetu wa Taifa walitaka kuondokana na uchumi wa kuzalisha malighafi tu.
Yote haya tuliyafanya kwa pamoja kama Taifa ama kwa kutumia fedha zetu wenyewe za kodi au kwa kutumia mikopo na misaada kutoka nje. Hata hivyo, baada ya Vita ya Kagera uchumi wetu ulianza kuporomoka na nchi yetu kulazimishwa kufuata masharti ya Shirika la Fedha la Dunia (IMF) na Benki ya Dunia”.
Miongoni mwa masharti hayo ikawa ni pamoja na kubinafsisha njia za uzalishaji tulizotaifisha na tulizojenga wenyewe. Tumeendelea kusema “Kuanzia mwaka 1996 tulianza kuona viwanda vyote tulivyojenga kwa pamoja vikibinafsishwa na kupewa watu wachache –wengi wao wakiwa wageni. Tulianza kuona mabenki tuliyomiliki wote kama Taifa yakiuzwa kwa bei ya kutupwa. Kimsingi ubinafsishaji si tu ulikuwa ni ugenishaji wa uchumi wetu bali ulikuwa ni ‘deindustrialisation’.
Leo hii hakuna hata kiwanda kimoja cha korosho kinafanya kazi licha ya kubinafsishwa, lakini Watanzania wote bado wanalipa madeni ya kujenga viwanda hivyo maana tulijenga kwa mikopo. Hali ni kama hiyo kwa viwanda vya nguo ikiwemo vinu vya kuchambulia pamba.
Azimio la Tabora linazungumzia Uchumi Shirikishi unaosimamiwa na dola; sio kumilikiwa na dola. Azimio la Tabora linataka “ wananchi wengi kumiliki uchumi kwa kupitia vyama vyao vya ushirika na jumuiya zao”. Hapa inapaswa kutofautisha dhana ya Shirika la Umma na Shirika la Serikali. Kwa mfano Kampuni ya TANESCO tunaliita ni Shirika la Umma, si sahihi. Hii ni kampuni ya serikali kwa sababu serikali inamiliki asilimia 100 ya kampuni hii. Serikali inaweza kuwa ya serikali ya kibepari ama ya kidikteta. Lakini iwapo TANESCO ingekuwa inamilikiwa na wafanyakazi wa TANESCO, ama Vyama vya Wafanyakazi ama Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutumia michango ya wanachama, kwa asilimia 51, tungeweza kusema kuwa TANESCO ni Shirika la Umma kwa sababu linamilikiwa na wananchi wenyewe. Serikali ya Makaburu wa Afrika Kusini ilikuwa inamiliki kampuni ya Umeme ya nchi ya Afrika Kusini kwa asilimia 100 lakini huwezi kusema makaburu walikuwa wajamaa.
Dhana hii ya uzalishaji ni dhana muhimu sana kwenye tafakuri ya Ujamaa katika miaka hii 50. Mwongozo wa mwaka 1981 ibara za 58 – 62 zinazungumza “ kujikosoa na kukosoana ni silaha ya Mapinduzi”. Ukweli ni kwamba tulifumbia macho ukweli kuwa tulikuwa tunajenga ubepari wa dola badala ya Ujamaa wa wananchi. Azimio la Tabora linataka Dola kusimamia Uchumi kwa umadhubuti unaotakiwa.
Kuna nafasi hiyo katika hali ya sasa ya dunia? Jibu ni Ndio lakini kulingana na mazingira ya kila nchi. Kwa mfano, kule China, wenzetu mashirika yao yanashindana na mashirika binafsi katika soko na tumeona mashirika makubwa ya Serikali ya China sasa yamekuwa mashirika ya kimataifa ( multinationals ). Katika nchi za Scandinavia, kampuni binafsi na watu binafsi wanashiriki katika uchumi wa soko lakini serikali inahakikisha kuwa huduma zote za muhimu za wananchi zinapatika kwa wananchi wote. Huduma hizi ni Elimu, Afya na Hifadhi ya Jamii. Katika nchi hizi kodi ya mapato ni mpaka 50% ya mapato la mtu na wananchi hawalalamiki kwa sababu wanapata huduma zote kabisa bure na bila ubaguzi kulingana na hali ya kipato ya mtu.
Tofauti ya Kipato ( Inequality)
Tumeona kuwa Azimio la Arusha lililenga kujenga Jamii ambayo watu hawapishani sana kwenye kipato. Azimio la Arusha linasema, ninanukuu “ Katika nchi ya Ujamaa kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi hufanya kazi, kila mfanyakazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbalimbali hayapitani mno” mwisho wa kunukuu.
Hii inaonyesha kuwa kutopishana mno kwa mapato miongoni mwa wafanyakazi ilikuwa ni dhumuni kubwa la Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Lakini mtazamo wa viongozi wa waasisi wa nchi yetu ulikuwa kwamba WAFANYAKAZI ndio tabaka kuu na kwamba tabaka la wenye mitaji lisingeweza kuibuka ndani ya nchi ya Ujamaa. Miaka 50 baadaye hali ni tofauti sana kwa sababu kuna mapato ya wajasiriamali ambayo yaweza kupitana mno.
Azimio la Tabora linalenga pia kujenga Taifa ambalo tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi haipitani sana na linapendekeza kutumia sera za kikodi kurekebisha tofauti hiyo. Azimio la Tabora linasema, nanukuu “ unyonyaji ni kutompa mtu ujira stahiki kulingana na kazi yake. Uchumi ni lazima uwe na watu wanaofikiria na kubuni shuguhli za uzalishaji na walipwe kulingana na ujasiriamali wao bila kunyonywa kwa kazi zao. Kama ambavyo nguvu kazi (labour force ) hulipwa kwa mshahara, Mtaji ( capital ) hulipwa kwa riba na ardhi hulipwa kwa tozo (rent), ndivyo ujasiriamali hulipwa kwa faida. Ni wajibu wa Dola kudhibiti ulimbikaji wa mali kupitia mfumo wa kodi…” mwisho wa kunukuu. Hivyo, Azimio la Tabora linasisitiza kwamba “katika nchi ya aina ya ujamaa tunaotaka kujenga, serikali kupitia sera za kodi na sera za nchi hurekebisha tofauti ya kipato kati ya walionacho na wasio nacho”.
Tofauti kubwa kati ya Azimio la Tabora na Azimio la Arusha ni eneo hili la kutambua kundi la wenye mitaji katika ujenzi wa uchumi.
Lakini Maazimio yote mawili yana mtazamo unaofanana kuhusu hatari ya kuwa na jamii yenye tofauti kubwa ya kipato ndani ya wananchi wake. Tutafanya uchambuzi wa hali hii kwa kurejea maandiko ya watafiti mbalimbali wa dunia na kujaribu kuonyesha kwamba ingawa tunaona kana kwamba nchi inasonga mbele, ukweli ni kwamba nchi yetu inarudi nyuma kwenye kuwianisha mapato ya wananchi wake.
Dhana ya tofauti ya kipato (inequality ) na ile ya mgawanyo (redistribution ) ni dhana ambazo ni mjadala wa kudumu katika siasa uchumi ya dunia nzima na sio Afrika ama Tanzania peke yake. Waumini wa Soko Huria wanaamini kwamba nguvu ya soko, juhudi binafsi na ukuaji wa uchumi ndio njia pekee za kugawanya mapato miongoni mwa wananchi. Mabepari wanashawishi serikali kuwa ndogo na isiingilie sana uchumi kwani soko litagawa mapato kwa kila mtu kulingana na juhudi zake. Kwa upande mwingine, waumini wa Ujamaa wanaamini kwamba njia pekee ya kuwaondoa wananchi kwenye umasikini ni kwa kufanya harakati za kisiasa na kijamii ili serikali ishike njia kuu za uzalishaji kwa kutaifisha njia hizo na kuweka mfumo wa malipo ya wafanyakazi ambao unamtosheleza mfanyakazi kuweza kuishi. Njia ya kibepari ndio imetamalaki kwenye dunia ya sasa, na Tanzania ilijaribu njia ya Ujamaa kwa miaka 25 na kutokana na shinikizo la kidunia na nguvu ya vibepari vya ndani iliiacha njia hiyo. Kujenga uchumi wa soko kumekuza mno tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi wa Tanzania.
Hata kwenye mataifa ya kibepari kumeibuka mjadala mkubwa kuhusu mfumo wao wa uchumi. Kuibuka kwa mtu kama Bernie Sanders huko Marekani ambaye amejitambulisha waziwazi kwamba yeye ni Mjamaa ni ishara tosha kwamba mdahalo kuhusu mifumo ya uchumi sio midahalo ya upande mmoja wa itikadi tena. Ni wale tu wenye mawazo ya kufilisika kiitikadi ndio wanaweza kudhani kuwa Ujamaa umezikwa duniani. Kuongezeka kwa kasi kwa tofauti za kipato miongoni mwa wananchi ndani ya nchi moja na miongoni mwa mataifa kutaleta msuguano ambao utarejesha kwa nguvu sana itikadi ya Ujamaa kwenye sera za mataifa mbalimbali. Nchini Marekani, kufuatia kampeni ya Bernie Sanders, chama cha Democrats kiliweza kuweka ahadi za kijamaa kwenye ilani yake ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa kiwango cha mshahara wa kuishi ( living wage ) na upanuzi mkubwa wa Hifadhi ya Jamii ( social security ). Kufuatia kitabu cha Mtaji kwenye karne ya 21 cha mwanazuoni nguli Thomas Piketty, kuna rundo la vitabu hivi sasa kuhusu suala la tofauti ya kipato tu. Asasi za kiraia kama Ford Foundation ya Marekani zimeanza kampeni maalumu ya dunia nzima kuhusu ajenda hii. Mimi mwenyewe nimerekodiwa kueleza uelewa wangu kuhusu ajenda hii na kuwekwa kwenye tovuti ya taasisi hii.
Tunajaribu kuweka mjadala huu kwenye muktadha wa Tanzania kwa kuangalia sera zinazotekelezwa sasa kama zinatufanya kupunguza tofauti ya kipato kwa kuwawezesha watu wa chini kuongeza kipato ama kwa kuwaongezea wenye mitaji kipato zaidi na kunyonya wavuja jasho walio wengi.
Mwezi Juni, 2012, niliandika andiko katika lugha ya Kiingereza (‘The Bottom 30M’, www.zittokabwe.com) kujibu swali la kwa nini Watanzania ni masikini licha ya utajiri mkubwa uliopo nchini. Katika makala hiyo ‘Mafukara milioni 30’ nilihitimisha kwamba Watanzania ni masikini kwa sababu watawala wetu wameamua hivyo kwa kutunga na kutekeleza sera na mikakati ambayo inanufaisha watu wachache katika tabaka la juu la maisha ambao wengi wanaishi mijini na kuacha watu wengi wanaoishi vijijini wakiwa masikini zaidi.
Sababu za umasikini kuongezeka nchini licha ya kwamba uchumi unaonekana kukua kwa kasi (kwamba ukuaji wa uchumi Tanzania haujapunguza umasikini) ni mikakati ya kiuchumi tunayotekeleza, haimsaidii Mtanzania wa kawaida maana hatuoni tofauti ya maisha yake. Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka ya 2002-2012 uchumi umekua kwa wastani wa asilimia saba, lakini umasikini umepungua kwa asilimia 2.1 tu ambayo ni ndogo ikilinganishwa na asilimia ya ukuaji wa uchumi. Katika kipindi hicho umasikini ulipungua kwa asilimia 2.1 kutoka asilimia 35.6 hadi kufikia asilimia 33.4. Kasi hii ya kukua kwa uchumi ni dhahiri imenufaisha watu wachache hususani wenye mitaji na kwamba umasikini haupungui ni dhahiri kwamba nadharia kuwa nchi zinahitaji ukuaji uchumi tu (growth ) ni nadharia isiyo timilifu.
Kijitabu cha The Economist Pocket World in Figures cha mwaka 2012 na mwaka 2017 kinaonyesha kwamba Pato la Taifa la Tanzania liliongezeka kutoka USD 21.4 bilioni mwaka 2009 hadi kufikia USD 48.1 bilioni mwaka 2014. Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miaka 5 uchumi wa Tanzania ulipanuka mara mbili na zaidi. Licha ya Pato la Taifa kupanuka kwa 100%, kasi ya kuwaondoa Watanzania kwenye umasikini ni ndogo mno ambapo mwaka 2014 takribani asilimia 30 ya Watanzania walikuwa ni masikini.
Kwanini uchumi unakua kwa kasi kubwa, lakini ukuaji huu haupunguzi umasikini, unazalisha masikini zaidi?”
Taarifa za serikali pia zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi hautengenezi ajira kwa watu. Kwanini hali hii? Kama kawaida hatukosi majibu ya maswali haya. Tunayarudia majibu haya kila wakati tunapopata nafasi ya kueleza. Kwamba sekta za uchumi zinazokua kwa kasi hazina mahusiano yenye nguvu na wananchi wa kawaida. Sekta hizi ni Madini, Ujenzi, Mawasiliano na shughuli za fedha na Bima. Sekta yenye mahusiano makubwa na wananchi, sekta ya kilimo, haikui kwa kiwango kinachoweza kupunguza umasikini. Mwaka 2015 Sekta ya Kilimo ilikua kwa 2.3% tu. Kwa mujibu wa wataalamu wa Uchumi, ili kupunguza umasikini Tanzania kwa kiwango kikubwa, sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya nane (8%) angalau kwa miaka mitatu mfululizo na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia sita (6%) kwa miaka kumi.
Mapitio ya nguvu kazi ya Taifa ya mwaka 2014 yanaonyesha kuwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini ni milioni 22.3 lakini waliopo kwenye ajira rasmi ni 2.1 milioni tu. Kwahiyo wengi wa watu ambao wapo kwenye ajira zisizo rasmi ni wakulima ambao wengi wapo vijijini. Kwa maana hiyo, sekta ya kilimo inapodumaa, zaidi ya watanzania 20 milioni hudumaa pia maana pato lao haliongezeki.
Kwanini sasa sekta ya kilimo haikui kwa kiwango kinachotakiwa ili kuondoa umasikini Tanzania? Jawabu langu ni kwamba watawala hawataki. Watawala wetu wamechagua Watanzania wengi wabakie mafukara. Umasikini wa Watanzania ni chaguo mahususi la watawala kwa kuamua kutekeleza sera ambazo zinakuza kipato cha mwenye nacho na kufukarisha wananchi wengi wa vijijini. Umasikini unaweza kusababishwa na masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kuwa masikini tu (we are poor because we are poor) au jiografia nk. Ufukara unatokana na kufukarishwa. Unatokana na maamuzi ya kisera ya taifa husika (au mataifa ya nje) ambayo yananyonya juhudi za watu kupata maisha yenye kuwapa huduma zote za msingi kama elimu, afya, maji na muhimu zaidi chakula cha uhakika. Watanzania waliowengi wanafukarishwa na sera za Taifa ambazo zinakwenda kinyume kabisa na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea. Lengo la Katiba ni “kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha … (i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi. (j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi”.
Tangu tulipolitupa Azimio la Arusha malengo haya ya katiba yamekuwa yakikanyagwa na matokeo yake hivi sasa watu wachache binafsi wamejilimbikizia mali nyingi sana na wengi hawana mali kabisa. Vilevile mgawanyo wa umasikini pia upo kijiografia na kimaeneo ambapo masikini wengi zaidi wapo vijijini kuliko mijini.
CCM imewafukarisha wa Vijijini
Mwaka 1991, Watanzania masikini wanaoishi Dar es Salaam walikuwa ni takribani asilimia 28.1 ya wakazi wote wa jiji. Miaka 16 baadaye, asilimia 16 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikuwa wanaishi kwenye umasikini. Kwa upande wa Watanzania wanaoishi vijijini, mwaka 1991 kulikuwa na masikini asilimia 40 ya wakazi wote wa Tanzania vijijini. Mwaka 2007, miaka 16 baadaye, asilimia 37 ya Watanzania wa vijijini walikuwa wanaishi kwenye dimbwi la umasikini. Takwimu hizi zimefafanuliwa vizuri na Ofisi ya Takwimu ya Taifa na Shirika la Twaweza limerahisisha taarifa hizi kupitia chapisho lao ‘Growth in Tanzania: Is it reducing poverty?’
Masikini wanaoishi Dar es Salaam na miji mingine nchini wanaweza kujikwamua kutoka umasikini kutokana na fursa zinazojitokeza mijini. Miundombinu ya usafiri na usafirishaji, viwanda vipya na fursa za ajira zinajengwa zaidi mijini kuliko vijijini. Huduma za elimu na afya zinaboreka zaidi mijini na hata walimu na manesi wanakimbilia kufanya kazi mijini ambako wamerundikana kuliko vijijini ambapo kuna ukosefu wa kutisha wa wafanyakazi wa sekta hizo. Masikini wa mijini sio mafukara. Masikini wanaoishi vijijini licha ya kufanya kazi kwa bidii na hasa kazi za kilimo hawana fursa za kuondokana na umasikini.
Mfumo wa uchumi wa nchi umejengwa kwa misingi kwamba watu wa vijijini hupokea bei za kuuza mazao yao kutoka mijini na vilevile hupokea bei za kununua bidhaa zinazotengenezwa mijini kutoka huko huko.
Barabara za vijijini zina hali mbaya au hazipo kabisa. Huduma za jamii kama elimu, maji na afya ni mbaya. Huduma za nishati ya umeme hazipo kabisa katika vijiji 96 kati ya 100 nchini.
Masikini wa vijijini ni mafukara. Wamefukarishwa kutokana na sera zinazonyonya jasho la kazi yao kwa upande mmoja na sera zinazowanyima maendeleo ya miundombinu kwa upande mwingine. Kufunguliwa kwa miundombinu ya vijijini kama barabara, maji na nishati ya umeme kunaweza kuwaondoa watu wa vijijini kwenye minyororo ya ufukara kwenda kwenye umasikini na hatimaye kutokomeza kabisa umasikini.
Lakini, watawala wanaogawa rasilimali ya nchi hawataki. Wanasema hakuna rasilimali fedha za kutosha kusambaza umeme vijijini ili kukuza viwanda vidogo vidogo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kusambaza maji safi na salama ili kuboresha afya na kumpunguzia mwanamke wa kijijini muda wa kutafuta maji na kujenga barabara za vijijini ili wakulima wafikishe mazao yao sokoni. Ikifika kujenga shule na zahanati na vituo vya afya, wananchi wa vijijini wanaambiwa wajenge wenyewe, wajitolee. Tutarudi kwenye suala la rasilimali fedha zinavyopotea baadaye kidogo. Sera na mikakati ya kijamaa tunayopendekeza ili kuendeleza kilimo na kuondoa umasikini nchini zimeelezwa kwenye Sura inayohusu Kilimo katika kitabu hiki.
Chimbuko la tofauti ya kipato na namna ya kusawazisha pengo
Kama nilivyosema hapo juu suala la tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi na miongoni mwa mataifa ya dunia ni mjadala wa kidunia. Katika eneo hili kwa kiasi kikubwa nitatumia tafiti za wanazuoni wabobezi akiwemo Thomas Piketty wa Ufaransa katika kufafanua dhana, chimbuko na majawabu ya pengo la kipato kati ya wasio nacho na wenye nacho.
Nini vyanzo vya mapato ya wananchi? Katika Azimio la Tabora tulisema kwa ujumla kuwa Mfanyakazi analipwa mshahara, mmiliki wa ardhi analipwa tozo ya ardhi (pango) mwenye mtaji analipwa riba na Mjasiriamali analipwa faida. Tulisema kwa ujumla kwa sababu nchi zetu zenye sehemu kubwa ya Uchumi wenye watu walio kwenye sekta isiyo rasmi ni vigumu sana kuweza kupata takwimu za mafungu ya wananchi na vipato vyao. Kwa nchi ambazo sehemu kubwa ya raia wake wapo rasmi na hujaza fomu za marejesho ya kodi ( tax returns ) mafungu ya mapato na vyanzo vyake kisekta hujulikana. Kwa mfano, Nchini Ufaransa, anaandika Piketty, mgawanyo wa vyanzo vya mapato ni mishahara ya wafanyakazi, kipato cha kujiajiri binafsi, pensheni, mafao mengine ya Serikali na mapato ya mitaji ( riba, gawio na pango la ardhi ). Utafiti uliofanywa kwa Kaya 2.4 milioni unaonyesha kwamba 59% ya mapato ya kaya zote inatokana na mishahara ya wafanyakazi na 6 mapato ya watu waliojiajiri wenyewe. Mapato yatokanayo na riba, gawio na pango la ardhi ni 5% ya mapato ya kaya zote nchini humo. Wafanyakazi rasmi ni asilimia 9 tu ya nguvu kazi ya Taifa letu.
Wafanyakazi wa Tanzania wananyonywa mpaka damu
Hapa nchini kwetu, kama tulivyoonyesha takwimu hapo juu, Wafanyakazi kwenye sekta rasmi ni milioni 2.1 sawa na asilimia 9 tu ya nguvu kazi yote ya Taifa. Hawa wameajiriwa kwenye sekta binafsi (1.4m sawa na 67% ) na sekta ya umma (700,000 sawa na 33%). Hawa wanalipwa mishahara na posho mbalimbali kama chanzo cha mapato yao. Asilimia 91 ya Watanzania wapo kwenye sekta isiyo rasmi na rekodi ya mapato yao yaweza kuwa kizungumkuti kuipata. Hata hivyo tunajua kuwa wengi wameajiajiri wenyewe kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa madini na utoaji huduma. Ni muhimu kusisitiza kuwa Watanzania wengi hawamo kwenye ajira rasmi au isiyo rasmi. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa Jijini Dar es Salaam kwa mfano ni asilimia 60 tu ya wakazi wake wapo kwenye ama ajira rasmi au ajira isiyo rasmi na asilimia 40 hawana kazi yeyote.
Uchambuzi pekee ambao tunaweza kuufanya kwa sasa ni kwa kutumia vyanzo vya mapato ya serikali ambapo tutaona mchango wa kaya kwenye mapato ya Serikali kulingana na vyanzo yake vya mapato.
Kwa mfano, Kitabu cha Mapato ya Serikali Kuu cha mwaka 2016/17 kinaonyesha kuwa Wafanyakazi wote wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi watachangia jumla ya shilingi trilioni 3 kwenye mapato yote ya Serikali kulinganisha na wenye mitaji ambao watachangia jumla ya shilingi bilioni 900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la mitaji na riba (taxes on income/interests, profits and capital gains ).
Hata ukitazama miaka miwili ya nyuma utaona kwammba mwaka 2015/16 makampuni yalichangia shilingi 773 bilioni wakati Wafanyakazi walichangia 2.2 trilioni na mwaka 2014/15 makampuni yalichangia 600 bilioni na wafanyakazi 1.9 trilioni kama kodi zao kwenye mapato ya Serikali. Kwa kutumia kigezo cha Kodi za Mapato, matajiri wanachangia robo tu ya mapato yote ya serikali na wafanyakazi wanachangia robo tatu iliyobakia. Hii inachangia sana kuwepo kwa tofauti ya kipato ndani ya jamii.
Kwanini wafanyakazi wanachangia zaidi kuliko wenye mitaji ni swali ambalo tutalieleza. Sababu kubwa ni kuwa mabepari wana fursa ya kukwepa kodi kisheria wakati wafanyakazi hawana uwezo huo. Kodi za wafanyakazi hukatwa moja kwa moja na waajiri kutoka kwenye mishahara yao.
Kwanini Kodi za Makampuni ni kidogo kuliko za Wafanyakazi?
Wafanyakazi wa hukatwa kodi zao kutoka kwenye mishahara yao moja kwa moja ikiwemo pia makato mengine kama michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya. Makato hayo huanzia asilimia 9 kwa mishahara ya ngazi ya chini mpaka asilimia 30 kwa wenye kulipwa mishahara ya juu kabisa. Kwa hiyo kodi ya wafanyakazi ni kodi ambayo serikali ina uhakika nayo moja kwa moja. Kwa takwimu ambazo tumeziona tayari, ni wafanyakazi wa sekta rasmi tu ndio hubeba mzigo wote wa kodi za wafanyakazi hapa nchini. Lakini kwanini kodi zinazotokana na mapato ya makampuni ziwe kidogo kuliko kodi zinazotokana na mapato ya wafanyakazi?
Kwenye makampuni, Kodi ya Mapato ni asilimia 30 ya faida ambayo kampuni imepata. Lakini mapato yanayokusanywa kwenye kodi hii ni kidogo sana kama tulivyoona, shilingi bilioni 600 tu kati ya mapato yote ya serikali mwaka 2016/17 sawa na asilimia nne tu ya mapato yote ya serikali yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali halisi hii sio ya Tanzania peke yake.
Mwanazuoni Thomas Piketty anaeleza kuwa “ ingawa kodi za faida za makampuni ni kati ya asilimia 40-50 kwenye nchi za magharibi, mapato kwenye kodi hizi hayazidi asilimia 2.5-3 ya Pato la Taifa”. Piketty anaendelea kuandika kuwa “ nadharia ya faida inayotozwa kodi ni nyembamba kuliko nadharia ya mapato ghafi ya ziada kwa sababu makampuni huondoa gharama za uchakavu wa mitambo, riba kwa mikopo na hata gharama za bima.
Kodi kwenye faida imegubikwa na matundu mengi kwenye mfumo mzima wa kodi duniani” (msisitizo ni wangu). Matundu haya ndiyo njia za ukwepaji kodi zinazofanywa na makampuni na hasa makampuni ya kimataifa ( Multinational Corporations ). Nchi za Afrika zimeathirika mno na mfumo wa kodi wa kimataifa na hivyo kupelekea fedha nyingi kutoka Afrika kutoroshwa kwenda ughaibuni.
Azimio la Tabora limeeleza kidogo kadhia hii ambayo Serikali za Afrika hazitilii maanani kabisa licha ya taarifa nzuri ya Rais mstaafu Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini. Ninanukuu “Katika kitabu cha ‘Africa’s Odious debts: How foreign loans and capital flight bled a continent’, waandishi Leonce Ndikumana na James Boyce, wameonesha kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, jumla ya dola za Kimarekani bilioni 11.4 zimetoroshwa kutoka Tanzania kwa njia mbalimbali.
Hizi ni sawa na wastani wa dola za Kimarekani 285 milioni kutoroshwa kila mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi zinatoroshwa na makampuni makubwa ya kigeni yanayofanya biashara na kuwekeza hapa nchini”.
Africa Progress Panel na kikosi kazi kilichoongozwa na Rais Thabo Mbeki ilieleza kuwa Afrika hupoteza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 50 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha unaofanywa hususan na makampuni haya ya kimataifa.
Inasemekana asilimia 30 ya utajiri wa fedha wa bara la Afrika umewekwa kwenye pepo za kodi (tax havens ) kwa mujibu wa kitabu cha The Hidden Wealth of Nations kilichoandikwa na Gabriel Zucman, mhadhiri wa London School of Economics.
Katika kitabu hicho, Zucman ameonyesha takwimu kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi zinazothibitisha kuwa takribani dola za kimarekani bilioni 150 kutoka Afrika zimehifadhiwa kwenye mabenki ya nchi hiyo. Jumla ya Pato la Taifa (GDP) ya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni dola za kimarekani 147.3 bilioni, hivyo fedha za Afrika zilizopo Uswisi ni zaidi ya GDP ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja. Fedha hii ni mara tano ya gharama za kujenga mradi wa Inga Dam kule Kongo ambao ungeweza kuzalisha umeme wa kutosha bara zima la Afrika.
Pamoja na mambo mengine, matundu haya ya ukwepaji kodi yamejengwa ndani ya mfumo wa kodi za kimataifa. Kuna kitu kinaitwa kwa lugha ya kigeni Base Erosion and Profit Shifting ikiwa na maana kuwa makampuni ya kimataifa yanapowekeza hapa nchini huhamisha faida kupeleka nchi zenye viwango vidogo vya kodi na hivyo kutolipa kabisa kodi hapa nchini ama kulipa kodi kiduchu sana.
Kwa mfano, katika kukokotoa kodi kampuni huondoa gharama za riba za mikopo, bima na gharama za utawala na kinachobakia ndio faida ambayo hutozwa kodi. Kampuni hizi huchukua huduma hizi za mikopo, bima na utawala kutoka kwa makampuni dada na kuongeza gharama maradufu na hivyo kuhamisha fedha hizi kana kwamba wanalipia hizi gharama na hivyo kupunguza sana wigo wao wa kodi. Ndio maana siku za nyuma tulisikia kampuni za madini hazilipi kodi ya mapato kwa sababu nyingi zilikuwa zikitumia mtindo huu wa kumomonyoa wigo wa kodi.
Wakati nikiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Madini ya Jaji Mark Bomani tulikuta ushahidi wa kampuni ya Geita Gold Mines ambayo uwiano wa mtaji wake na mikopo (debt-equity ratio) ulikuwa asilimia milioni 12. Hii iliifanya kampuni hii kumomonyoa kila walichokipata katika uchimbaji wa dhahabu nchini kwetu na kukihamishia njia kana kwamba ni malipo ya mikopo waliyochukua kumbe ni mbinu ya kukwepa kodi na kupora dhahabu ya Tanzania.
Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, tuliagiza ukaguzi wa ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa na iligundulika kuwa karibia kila sekta ya uchumi ilihusika na ukwepaji kodi.
Mfano ambao huwa naukumbuka mara kwa mara ni mfano wa mauzo yetu ya Korosho kwenda nje. Hupenda kuurudia na nitaurudia tena hapa.
Mwaka 2011 Tanzania iliuza Korosho kwa nchi ya India. Kwenye rekodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ilionyesha kuwa tuliuza tani 80,000 za korosho kwa bei ya dola za marekani 1000 kwa kila tani sawa na dola za kimarekani 80 milioni.
Uchunguzi ulionyesha kuwa katika nchi ya India rekodi yao ya Korosho walizonunua kutoka Tanzania ilikuwa ni dola za kimarekani 120 milioni kwa sababu wao walinunua tani 120,000 za korosho kutoka Tanzania. Hii ina maana kuwa tani 40,000 hazikurekodiwa kwenye forodha zetu na hivyo wauzaji kukwepa kodi ya ushuru wa korosho wa zaidi ya dola za kimarekani 12 milioni.
Pia kwenye kodi ya Mapato ya kampuni iliyouza korosho hizi mapato ya zaidi ya dola 40 milioni hayatoonekana na hivyo kufanikiwa kukwepa kodi. Huu ni mfano ninaopenda kuuleza katika kueleza namna mfumo wetu wa kodi ulivyojaa matundu na kuhitaji kufanyiwa kazi kubwa ya kuufumua.
Kwa hiyo makampuni yana njia nyingi za kukwepa kulipa kodi na hivyo wamiliki wake kujilimbikizia mali nyingi na kuongeza tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi. Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tofauti ya kipato itazidi kuongezeka na kuleta hatari kubwa kwa ustawi wa wananchi na usalama wa nchi yetu.
Moja ya suala ambalo chama cha ACT Wazalendo ililieleza na halikuelezwa na chama kingine chochote katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ilikuwa ni hili la kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ili kila anayepaswa kulipa kodi alipe kwa haki na kwa uwazi. Tuliahidi “ kuweka mfumo mpya wa kodi za kimataifa ili kuzuia makampuni ya kimataifa kumomonyoa wigo wa kodi kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za kimataifa za kurekebisha mfumo wa kodi za kimataifa, kupitia mikataba ya kikodi na nchi nyengine ili kuzuia ukwepaji kodi na kujengea uwezo kitengo cha kodi za kimataifa ili kudhibiti ukwepaji kodi”.
Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini katika eneo hili?
Serikali ya Awamu ya Tano ilisifika kwa makusanyo makubwa ya kodi katika miezi yake ya mwanzo ya kuongoza nchi yetu. Lakini haijafanya juhudi yeyote ya ndani au ya nje kuhakikisha kuwa nchi inaondoa tofauti kubwa ya kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho. Mara kadhaa Rais wa Jamhuri ya Muungano amekuwa akisikika kusema kuwa “anataka waliokuwa wanaishi kitajiri waishi kishetani”.
Sina hakika kama hili ni jambo la mantiki katika kufumua mfumo wa uchumi ili watu wengi zaidi waweze kuondoka kwenye umasikini. Juhudi za kuendesha kampeni ya kimataifa ili kuboresha mfumo wa kodi za kimataifa zimeshuka chini na kiukweli kama nchi tumerudi nyuma wakati dunia nzima inashiriki kwenye kampeni hizi. Juhudi za ndani za kuongeza makusanyo ya kodi kama hazitatazama mfumo wa kodi za kimataifa, basi hazitakuwa na faida yeyote na tutabakia na kodi za wafanyakazi na vibarua tu kuendesha nchi yetu. Tunaendelea kinyume kinyume, kwamba Pato la Taifa linakua kwa kasi lakini 1) Idadi ya Watanzania masikini inaongezeka na 2) Tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi inaongezeka kwa matajiri kuwa matajiri zaidi na masikini kuwa masikini zaidi
Tunahitaji Ujamaa tena?
Nchi yetu imeharibiwa sana na ufinyu wa fikra na kukumbatia mifumo ya uzalishaji inayonyonya wananchi na rasilimali za nchi. Kuhubiri Ujamaa inaonekana ni dhambi ama kurudi nyuma lakini mifumo yetu ya uchumi bado inaendeshwa na nchi za kibeberu. Ubeberu ( imperialism ) ni mfumo wa mataifa mengine yenye nguvu kuendesha mataifa dhaifu.
Bado nchi za kiafrika zinahitaji Ujamaa ili kupambana na unyonyaji wa kimataifa. Bila ya kuwa na nadharia iliyo sahihi ni namna gani utapambana na ubeberu? Tunao mfano mzuri wa utoroshwaji wa fedha katika hotuba hii. Ukielewa ubeberu utaelewa ni kwanini tunapoteza mabilioni ya fedha kwenda nje, na huwezi kuelewa ubeberu bila kuelewa nadharia ya Ujamaa wa Kiafrika na Ujamaa kwa Ujumla.
Ujamaa uliturudisha nyuma? Wapo watu wengi wanaamini hivyo. Lakini watu hao hao huimba sifa za Tanzania kuwa na Umoja, Amani na Utulivu. Mwaka 1989 Mwalimu Nyerere, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini alisema, “ Wenzangu mmesimama hapa. Patel kasimama hapa akasema vizuri kabisa: ‘ tunashukuru kwa ushirikiano mzuri kwa Watanzania. Hapa Amani nzuri hakuna utengano wa ukabila au nini! […] Lakini Waswahili wanasema ukiona vyaelea vimeundwa. Vimeundwa. Sio tu utulivu umekuja wenyewe tu. […] sio kwamba Azimio la Arusha limeondoa umasikini hata kidogo. Umasikini si huu bado tunaendelea nao? Si huu mpaka leo? Uchumi si huuhuu bado tunasumbuka nao? [….] Azimio la Arusha limetoa ahadi ya Matumaini. Ya Haki, ahadi ya matumaini kwa wengi’. Hapa Mwalimu anasema nini? Kwamba Azimio la Arusha lilifanya kazi moja kubwa sana ya kuunganisha nchi.
Nchi ya mlinganisho na Tanzania ilikuwa Ivory Coast. Yenyewe ilifuata Ubepari, mliona kilichowapata? Kenya mliona kilichowapata? Ujamaa uliweka mazingira ya kupata maendeleo iwapo tukitekeleza sera sahihi. Hata hao wawekezaji tafiti zinaonyesha kuwa kivutio chao kikuu nini? STABILITY! Hatuna? Lakini tunawapa nini? MSILIPE KODI miaka 10. Kongo wawape kutolipa kodi daima muone kama wataenda. Ujamaa ulijenga Taifa letu na tunahitaji Ujamaa kuongoza Sera zetu kuelekea maendeleo makubwa zaidi. Ujamaa sio umasikini. Ujamaa ni kutokuwapo unyonyaji na wananchi kumiliki uchumi wao. Baya nini hapo?
Nimalize kwa kunukuu maneno ya Mwalimu J.K Nyerere; “ Hivi kweli Waswahili wachache nyinyi mtawale Watanzania kwa nguvu bila matumaini, halafu watakaa tu kwa amani-amani ya matumaini-matumaini yakiisha kutakuwa na ghasia za kijamii na nitawashangaa Watanzania hawa wakatae kufanya ghasia”
Nami nawashangaa sana Watanzania kukalia kimya uvunjifu wa wazi wa Haki na sheria za nchi. Simameni mlinde nchi yenu, hamna cha kupoteza isipokuwa minyoyoro ya umasikini. Long Live Azimio la Arusha, Long Live Azimio la Tabora.
Asanteni sana
Arusha, 25/3/2017
No comments:
Post a Comment