Sunday, March 19, 2017

TAARIFA KUTOKA ACT WAZALENDO

TAARIFA KWA UMMA
UTANGULIZI:

Ndugu waandishi wa Habari, kwanza nawashukuru kwa kuitikia wito wetu leo 
na kufika hapa ili kuchukua ujumbe tunaotaka kuutoa na kuuwasilisha kwa 
umma. Tuna mambo mahsusi matatu tunayopenda umma ufahamu. Nayo ni 
haya yafuatayo;-

A. UCHAGUZI UBUNGE WA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI
> Ndugu Waandishi wa Habari.

> KAMA mnavyofahamu tayari mchakato wa kuwapata wabunge 
watakaowakilisha nchi katika bunge la Afrika mashariki (EALA),umeanza na Chama 
cha ACT wazalendo ni miongoni mwa vyama vitakavyoshiriki Uchaguzi huo baada 
ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa na katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano 
wa Tanzania.
> Naomba kupitia kwenu waaandishi wa habari, tutumie nafasi hii kuwatangazia 
wanachama wote wa ACT Wazalendo kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea 
wa nafasi hizo ndani ya chama umeshaanza kuanzia jana tarehe 18 Machi 2017 
na fomu za wagombea zimeanza kutolewa leo Machi 19/2017 na mwisho wa 
kurudisha fomu hizo ni siku ya Jumanne Machi 21, 2017 saa kumi kamili jioni.
> Kwa wanachama walio Dar es salaam fomu watazipata hapa Makao Makuu ya 
Chama na walio mikoani tumeshawatangazia wawasiliane na Afisa Mawasiliano 
ya Ndani wa Chama kwa ajili ya kupatiwa fomu hizo.
> Chama cha ACT Wazalendo kitawapatia watanzania watu walio bora na makini 
watakaoenda kuiwakilisha nchi ndani ya Jumuiya hiyo na tuna uhakika wa 
wagombea watakaoteuliwa na Chama chetu watakuwa makini na hodari wa 
kujenga hoja kabla ya kuwa wabunge na baada ya kuwa wabunge.
B. MKUTANO MKUU WA KIDEMOKRASIA
> Ndugu Waandishi wa Habari,
> Chama chetu cha ACT wazalendo mbali na vikao vyake vya kikatiba(Mikutano), 
inavyohudhuriwa na wajumbe maalum, pia ina mkutano mkuu wa Kidemokrasia 
unaofanyika kila mwaka na Mwaka huu mkutano mkuu wa Kidemokrasia 
utafanyika Machi 25/2017 katika hoteli ya Corrido Spring Jijini Arusha
> Mkutano huu huwashirikisha wanachama wote na wasio wanachama huku 
ukiwa hauna wajumbe Mahususi na unajikita zaidi katika kujadili masuala ya 
maendeleo ya nchi na dunia kwa ujumla
> Maandalizi ya mkutano huu yameshakamiliki kwa asilimia zaidi ya tisini na 
tutakuwa na mijadala mbali mbali kutoka kwa wawakilishi wa taasisi za ndani na 
nje ya nchi, hivyo tunatoa wito kwa wakazi wa jiji la Arusha na viunga vyake 
kuhudhuria mkutano huu na kujadiliana masuala tofauti kwa ajili ya nchi yetu
> Ninawakaribisha watu wote nanyi waaandishi wa habari tunawakaribisha sana 
katika mkutano huuu
C. KATIBA MPYA YA NCHI
> Ndugu Waandishi wa Habari,
> Wakati nchi yetu ikijiandaa kuwapata wawakilishi wapya katika Bunge la Afrika 
ya Mashariki, Chama cha ACT Wazalendo, tunamuomba Rais Magufuli na tunamkumbusha umuhimu wa watanzania kuwa na Katiba bora itakayoamua maslahi ya nchi katika mfumo ulio rasmi mbali na matakwa ya mtu mmoja pale 
atakapokuwa anajisikia kufanya hivyo.
> Tunamkumbusha Rais Magufuli kuendelea na mchakato wa kuwapatia 
watanzania wanyonge Katiba iliyo bora kwa kuanzia pale Rasimu ya pili ya Jaji 
Joseph Sinde Warioba ilipoishia. Rais Magufuli aanzie na Rasimu ya Jaji Warioba 
ambayo ilikuwa inatoa nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale 
wasipotekeleza wajibu wao kulingana na nafasi walizo nazo.Tunaamini Rais Magufuli kwa namna anavyojinasibu kuwa ni Rais wa Wanyonge, 
hatalinda maslahi ya Chama chake pekee katika kuwapatia watanzania Katiba iliyo 
bora, bali ataangalia maslahi mapana ya Taifa letu.
Katiba iliyo bora itamnufaisha kila mmoja katika jamii hivyo tunawaomba 
Masheikh, Wachungaji Mapadri, Maaskofu na Taasisi nyinginezo kukazania jambo 
hili la Katiba mpya yenye kukidhi kiu na matakwa ya watanzania, kwa ajili ya 
kuifanya Tanzania iwe bora mbele ya uso Raia wake na katika Nyanja za 
kimataifa.
Msafiri Mtemelwa
Naibu Katibu Mkuu (Bara)
ACT Wazalendo
Dar es salaam.
19/03/2017

No comments: