MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliyeambatana na Azam FC kuelekea mchezo wake wa marudiano dhidi ya Mbabane Swallows, amesema wanauhakika mkubwa wa timu hiyo kusonga mbele kwa raundi ijayo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam FC inakabiliwa na mchezo huo muhimu utakaofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, mjini Mbabane, Swaziland Jumapili hii saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, ambapo inahitaji ushindi wowote au sare yoyote ili kuweza kusonga mbele.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz, Karia alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC kuweza kushinda, huku akidai kuwa ina mahesabu mazuri kutokana na kuondoka na ushindi katika mchezo wa kwanza.
“Ukiangalia kimahesabu wao ndio wanamahesabu mazuri, na ndio maana hapa kuna uwakilishi mzito umekuja kutoka TFF tupo wawili, tunauhakika ya kwamba tutafanya vizuri, Azam FC kwa sasa wapo vizuri,” alisema.
Karia alitoa ushauri kwa wachezaji wa timu hiyo kuzingatia nidhamu ya mchezo wakiwa uwanjani huku akiwataka wahakikishe wanapata bao mapema ili kuuweka mchezo kuwa mgumu kwa wenyeji.
“Kwa hali hiyo sisi tunauhakika kabisa Azam FC wapo katika nafasi nzuri ya kupita na mambo mengine tunamwachia Mungu, cha msingi wachezaji wa Azam FC wawe na nidhamu ya mchezo ya kujua kuwa wanacheza ugenini na nadhani mwalimu atakuwa amelichukulia uzito, Azam FC sio wageni kwenye michuano ya kimataifa, karibu wanamiaka mine sasa wanashiriki na makosa waliyojifunza nyuma huko watayarekebisha ili waweze kupita,” alimalizia.
Azam FC inaelekea kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa jambo ambalo linatoa mwanga kwa timu hiyo kuweza kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano, ambayo itakutana na moja ya timu 16 zilizotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuingia hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment