Friday, June 30, 2017

WIZARA YA MAMBO YA NDANI:- WATUHUMIWA 16 WA KIBITI SURA ZAO ZIMESHAPATIKANA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Eng. Hamad Yussuf Masauni ametangaza kuwa, Jeshi la Polisi linawaska watuhumiwa 16 wa mauaji ambayo yamekuwa yakiendelea kufanyika katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji Mkoani Pwani kwa muda mrefu sasa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Masauni amesema kuwa watuhumiwa hao wanafahamika na tayari jeshi la polisi lina picha za watuhumiwa wote ambao wanasakwa.

“Nchi yetu ipo katika changamoto ya matukio katika maeneo ya Kibiti na Rufiji, ambapo matukio haya wakati mwingine yanaripotiwa ndivyo sivyo na vyombo vya habari na kusababisha hofu kwa wananchi. Sisi kama serikali lazima tuwatoe hofu wananchi wetu. Tuwaombe wanahabari mfikishe ujumbe sahihi zaidi.

“Jana tulifanikiwa kuwadhibiti wahalifu wawili kabla hawajatekeleza uhalifu wao, kwa hiyo jeshi letu linafanya kazi vizuri sana. Suala la kumaliza uhalifu wa Kibiti ni la lazima wala sio la mjadala tena.

“Maandalizi ya mkoa Mpya wa Kipolisi wa Rufiji yamekamilika na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo tayari ameshateuliwa,” alisema Masauni.

No comments: