Saturday, July 1, 2017

JUMIA TRAVEL KUZINDUA RIPOTI YA UTALII TANZANIA


Na Dotto Mwaibale


KATIKA jitihada za kuchochea ukuaji wa utalii na ukarimu nchini, kampuni ya Jumia Travel ambayo inajihusisha na huduma za hoteli mtandaoni inatarajia kuzindua ripoti itakayotoa mustakabali mzima wa sekta hiyo.




Akizungumzia juu ya uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo, Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee amebainisha kuwa ripoti hiyo itaangazia masuala mbalimbali yanayoikumba sekta ya utalii na mchango wa wadau wake nchini.



“Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Jumia Travel kuwasilisha ripoti yake juu ya mustakabali wa sekta ya utalii Tanzania, mara ya kwanza ilikuwa 2016. Ndani ya ripoti hii tumeangazia hali halisi ya sekta hii ilipo kwa sasa, ukuaji wake, changamoto inazokumbana nazo pamoja na mchango wa wadau mbalimbali nchini. Tunaamini kwamba uwepo wa shughuli zetu kwenye nchi zaidi ya 40 barani Afrika unatupatia fursa ya kuwashirikisha mambo mengi wadau wa hapa nchini na serikali kwa ujumla ili sekta hii ikue na kuimarika zaidi,” alisema Bi. Dharsee.



Ikiwa inafanya shughuli zake mtandaoni,  Jumia Travel kupitia ripoti hii pia imetoa maoni yake namna teknolojia inavyoathiri sekta hii kwa sasa hususani jinsi gani ilivyobadilisha mfumo wa biashara na utoaji wa huduma mbalimbali.



Ripoti hii pia imejumuisha maoni ya wadau mbalimbali kama vile watoa huduma za hoteli, vyama mbalimbali vya wadau wa utalii, watunga na wasimamia sera pamoja na wataalamu katika sekta ya utalii nchini Tanzania. Na kwa kuongezea, ripoti tofauti za hivi sasa kuhusu uchumi wa taifa na sekta ya utalii kutoka kwenye mashirika yanayoaminika duniani na taasisi za kiserikali pia zimetumika.



“Tumefanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali kwenye sekta tuliyomo. Lengo kubwa ni kutoa ripoti isiyoegemea upande wowote na kwa namna moja ama nyingine tunaamini itakuwa yenye manufaa katika ukuaji wa sekta nzima ya utalii nchini,” alisisitiza Bi. Dharsee.

No comments: