Sunday, July 2, 2017

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUTUMIA HUDUMA ZA HOTELI MTANDAONI

Na Jumia Travel Tanzania

Kuna faida nyingi za kutumia mitandao inayotoa huduma za hoteli badala ya kuwasiliana nao au kutembelea tovuti zao moja kwa moja. Kwani unaweza kuperuzi aina tofauti za hoteli, kujua huduma walizonazo pamoja na bei kabla ya kufanya maamuzi ni hoteli gani umependezewa nayo.

Mbali na kuwepo kwa manufaa mengi kwa mteja pindi anafanya huduma za hoteli mtandaoni changamoto kubwa hujitokeza kwenye kufanya uchaguzi na maamuzi. Jumia Travel ingependa kukushirika mambo muhimu ya kuzingatia pindi unapoingia mtandaoni na kuchagua ni hoteli gani unayotaka kwenda.

Wapi unaweza kufanyia huduma hizo? Kwa wasafiri wengi wazoefu wanafahamu kuwa ni gharama kubwa kutumia huduma za hoteli kupitia kwenye tovuti zao. Badala yake hutumia mitandao inayotoa huduma hizo kwani huwa na bei nafuu tena na ofa kadha wa kadha. Kwa mfano, mmojawapo ya mitandao hiyo ni pamoja na Jumia Travel, ambao una aina mbalimbali za huduma za malazi kwa watu wa hadhi tofauti. Tofauti ya mitando hii na tovuti za hoteli ni kwamba zenyewe zinampatia mteja machaguo ya hoteli mbalimbali, mahali popote na kwa mujibu wa bajeti aliyonayo.
 
Fikiria kuhusu umbali, kufikika kwake na gharama za usafiri. Jambo linalofuatia baada ya kujua ni mtandao gani unaoweza kuutumia kupata huduma unayoitaka ni mahali unapotaka kwenda. Lakini pia ni vema kujiuliza je hapo unapotaka kwenda kunafikika kiurahisi na gharama za usafiri zikoje kukutoa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Usipokuwa makini unaweza kujikuta unakwenda kufikia sehemu ambayo itakupasa kutumia gharama kubwa za usafiri au ni ngumu kufika kwenda kwenye shughuli zako.

Chumba cha aina gani unachokipendelea? Hoteli au sehemu yoyote ile ya malazi inakuwa na machaguo tofauti kulingana na matakwa ya mteja. Kuna huduma ya chumba kimoja, chumba kimoja chenye vitanda viwili ndani, chumba chenye maliwato ndani yake na kadhalika. Hivyo lazima ujue ni chumba cha aina gani unakitaka ili hata iwe rahisi kumuelezea mtoa huduma hotelini, lakini hayo yote hutegemea bajeti yako kwani bei huwa tofauti.

Je unaweza kupata huduma siku hiyo hiyo? Dharura hutokea na huwa haiepukiki kwenye masuala ya kusafiri. Kwa mfano unaweza kupewa maagizo na bosi wako kusafiri kwenda mkoani siku hiyo hiyo na tayari tiketi ya usafiri umekwishakatiwa. Sio hoteli zote zinakubali au kupokea huduma kwa siku hiyo hiyo, hivyo yakupasa kutafiti ni hoteli gani zinafanya hivyo.



Pitia maoni ya wateja waliowahi kukaa hapo. Kuna umuhimu wa kutafiti wateja waliowahi kukaa sehemu unayotaka kwenda wanasemaje kuhusu huduma zao. Hii itakusaidia kujua kwamba itakufaa au la. Sidhani kama utashawishika kwenda kwenye hoteli ambayo wateja wameacha maoni mtandaoni kwamba wahudumu wa pale sio rafiki na wala hakuna ulinzi wa kutosha.

Wateja wanaopendelea sehemu hiyo ni watu wa aina gani? Hoteli huwa zinajengwa kwa malengo tofauti kulingana na aina fulani ya wateja. Zipo kwa ajili ya wafanyabiashara, familia, fungate kwa wanandoa, watalii na kadhalika. Kama wewe ni mfanyabiashara basi chagua hoteli itakayokufaa kwa dhumuni ulilonalo, usije kujikuta unakwenda kwenye hoteli ambayo wanafamilia na watoto huwa wanapenda kwenda kupumzika na ukakwazika.

Huduma nyinginezo - maegesho ya magari, kifungua kinywa, bwawa la kuogelea, sehemu ya kufanyia mazoezi. Kama msafiri na mara nyingi huwa sio wenyeji kwa mahali unapokwenda ni vema kujua ni huduma gani unaweza kuzipata kwenye hoteli unayotaka kwenda. Mfano wa huduma nyingi zinazotolewa na hoteli kwa sasa ni kama vile, kifungua kinywa, maegesho ya magari, mgahawa au chakula, kufuliwa na kupasiwa nguo na huduma ya usafiri. Kwa hiyo pindi unapoamua unakwenda kufikia wapi ulizia vitu hivyo ili kujua kama vinapatikana bure au kuna gharama utakazoziingia kama mteja.





Namna ya kufanya malipo. Sio hoteli zote zinaruhusu kufanya malipo taslimu pale unapofika hotelini na sio zote pia huruhusu mteja kutumia benki au mtandao. Kwa hiyo itakuwa ni jambo la msingi kujua sera ya malipo ya hoteli unayotaka kwenda. Kwani unaweza kukuta kuna hoteli nyingine inakupasa kulipia siku 2 kabla ya kwenda pale au hata wiki moja nyuma. Mara nyingi hii hufanyika ili kuzuia tabia ya wateja kusema wanakwenda halafu hubadili maamuzi, hoteli huwatoza kiasi kadhaa cha fedha wateja wenye tabia hizi ili kuepuka hasara.

Muda wa kuingia na kutoka. Kwa sababu umekwishalipia huduma kwenye hoteli fulani haimaanishi kwamba unaweza kwenda au kutoka muda wowote unaoutaka wewe. Kila hoteli inakuwa na utaratibu wake iliyojiwekee na ni muhimu kuzingatia kwani unaweza kujuikuta unakosa huduma uliyokwishailipia au kuingia matatizoni. Kwa mfano, sehemu nyingi za malazi hapa Tanzania muda wa wateja kuingia hotelini huwa ni saa 4 au 5 asubuhi na kutoka pia inakuwa ni hivyo hivyo siku inayofuatia.
 
Kwa dondoo hizo chache Jumia Travel inaamini kuwa utakuwa umepata mambo mapya ya kujifunza na wakati mwingine utakuwa makini kama ulikosea kipindi cha nyuma. Kufanya huduma za hoteli kwa njia ya mtandao ni kitu ambacho kinatumika duniani kote kwa sasa kwani ni njia rahisi, uhakika na salama. Kikubwa ni kuweza kujifunza namna ya kufanya hivyo kwani kuna faida lukuki badala ya kutumia njia za kawaida tulizozioea kama vile kuwapigia simu ndugu, jamaa na marafiki zako wakusaidie kufanya hivyo huko uendako.

No comments: