Saturday, July 1, 2017

UAMUZI WA KAMATI YA UTENDAJI TFF KUHUSU ATAKAYEKAIMU NAFASI YA MALINZI KWA SASA

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, iliyokutana leo Jumamosi Julai 01, 2017 kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam imempitisha Wallace Karia kuwa Kaimu Rais wa shirikisho.

Kadhalika, Kamati hiyo ya Utendaji ya TFF, imempitisha Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF.

Viongozi hao watakaimu nafasi hizo tajwa hadi hapo mahakama itakavyoamua kuhusu kesi zinazowakabili kwa sasa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine. 

Kamati ya Utendaji ya TFF, imekutana kwa dharura kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) inayosomwa pamoja na Ibara ya 35 (6) na kufanya uamuzi huo.

WAPITISHWA KUWANIA NAFASI MBALIMBALI TWFA

Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), imetangaza majina ya wagombea 11 waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaofanyika Julai 8, mwaka huu mkoani Morogoro.

Majina ambayo yamepitishwa ni Amina Karuma, Rose Kisiwa, Somoe Ng’itu, Theresia Mung’ong’o, Hilda Masanche, Salma Wajeso, Zena Chande, Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmin Soudy na Chichi Mwidege.

Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.

………………………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: