Wednesday, August 2, 2017

LEO MAHAKAMA KUU - JUA HATIMA YA WABUNGE 8 WA CUF WALIOVULIWA UWANACHAMA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania inatarajia kutoa uamuzi kuhusiana na mapingamizi yaliyotolewa na upande wa serikali katika kesi iliyofunguliwa na wabunge nane wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao walivuliwa uanachama wiki iliyopita,

Wabunge hao walivuliwa uanachama wiki iliyopita na Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na a Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika shauri hilo, Mawakili wa serikali wameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na wabunge hao ya kuishtaki Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Katibu wa Bunge pamoja na Wabunge wapya walioteuliwa na tume.

Shauri hilo lipo kwa Jaji Lugano Mwandambo na maamuzi ya pingamizi hilo yanatarajiwa kutolewa Agost 4, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaiomba mahakama kutoa zuio kwa Bunge kuwaapisha wabunge wapya ambao walitangazwa wiki iliyopita NEC hadi hapo kesi yao ya msingi waliyoifungua kupinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama itakapoamuliwa.

Aidha, wabunge hao wanaiomba mahakama kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa Baraza kuu la chama hicho wa kuwavua uanachama.

Kesi hiyo ya madai namba 143 ya mwaka 2017, inatarajiwa kutajwa tarehe 31 mwezi huu.
Upande wa walalamikaji unawakilishwa na Mawakili Peter Kibatala na Omari Msemo huku serikali ikiwakilishwa na Mawakili wanane ukiongozwa na Wakili Gabriel Malata

No comments: