Friday, September 1, 2017

WAKIMBIZI 12000 WA BURUNDI KUREJEA NCHINI KWAO


WAKIMBIZI 12,000 kutoka nchini Burundi walioonesha nia ya kurejea nchini kwao na kujiandikisha, wanatarajia kuanza kurudi kuanzia Septemba 7, mwaka huu.
Aidha, serikali imesema atakayesema Tanzania inafukuza wakimbizi nchini, itabidi kukaa naye meza moja ili aeleze kuhusu kauli hiyo kwani kufanya hivyo ni kuchafua jina la nchi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema hayo jana katika mkutano wa Kamisheni ya Utatu inayoshughulikia kuwarudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao kwa hiari yao.
Mwigulu alisema kuwarejesha kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ni haki ya mkimbizi yeyote kuondoka na kurejea katika nchi yake. Alisema kwa kuwa kazi ya kuwarejesha itaanza Alhamisi ijayo, inawezekana kukawepo idadi kubwa ya wakimbizi wenye kuonesha nia ya kutaka kuondoka kwa hiari, lakini pia kazi ya kuwarejesha ni endelevu ambayo inaweza kuwa na ongezeko kubwa la wanaotaka kurudi.
Mwigulu alisema kwa maana hiyo ni wajibu wa mashirika ya kimataifa kusaidia na kuwezesha kazi ya kuwarejesha makwao pamoja na maeneo watakayoishi nchini Burundi ili kazi ya kuwarejesha iwe endelevu zaidi. “Ili kufikia lengo ni muhimu kupanga kwa umakini kwa kuangalia malengo ya mbeleni ya wakimbizi ili kuepuka kurudi kwa ghafla,” alieleza Mwigulu na kuongeza kuwa sheria za kimataifa zinahitaji kuona utayari wa nchi husika katika kutoa ulinzi kwa wakimbizi watakaorudi.
Alisema Serikali ya Tanzania inatambua hali ya Burundi imetulia na inaruhusu wakimbizi walio tayari kurejea nchini kwao kwani Agosti 22, mwaka huu, Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza alipokutana na Rais John Magufuli, alikiri hali kuwa shwari nchini humo na kwamba warudi wakajenge nchi yao.
Kuhusu Tanzania kufukuza wakimbizi, alisema vipo vyombo vya nje vilivyodhani kuwa Tanzania inafukuza wakimbizi, wakiongeza zaidi kuwa inatumia jeshi na kuwatoa kwa nguvu, jambo ambalo siyo la kweli.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Burundi, Pascal Barandagiye alisema ni muhimu kwa kamisheni hiyo kujiunga ili wakimbizi hao wanaoomba warudi mapema na isichukue muda mrefu sana. Alisema wako tayari kuwapokea warudi ili waende kusaidia kujenga nchi yao. 
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR), Chansa Kapaya alisema ni muhimu kwao kuwa na imani na kule wakimbizi wanakokwenda kuwe na usalama kwa kuwa ni kazi inayokubalika kimataifa.



No comments: