IGP Simon Sirro. |
Na Dotto Mwaibale
WANANCHI wa Kata ya Kibwegere, Kibamba wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam wameiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo kuwasaidia kupunguza vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya vijana katika eneo hilo na kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Majira kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, wananchi hao walisema hali siyo shwari katika eneo hilo kufuatia vijana hao kualika wenzao kutoka maeneo mengine na kwenda kufanya vitendo vya ujambazi.
"Tunaiomba kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya itusaidie kukabiliana na vitendo hivi vya wizi vinavyofanywa na hawa vijana kwa kushirikiana na wenzao kutoka maeneo mengine," alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Mkazi huyo alisema katika vipindi tofauti vijana hao walifanya tukio la ujambazi kwa kuvamia nyumba tatu katika eneo hilo na kusabisha vifo vya watu wawili ambao waliwataja kuwa ni Mwalimu wa shule moja ya awali iliyopo eneo hilo na mzee Kaberege ambao waliuawa katika matukio yaliyofanyika mwaka jana huku wengine wakijeruhiwa.
"Matukio haya yote ya wizi wa kuvunja fremu za biashara, wizi wa mifugo kama nguruwe na ng'ombe yamekuwa yanafanyika lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na polisi hali inayotukatisha tamaa wananchi," alisema mzee wa eneo hilo.
Mzee huyo aliongeza kuwa vijana hao wamekwisha fanya matukio mengi ya uhalifu bila kuogopa polisi kwa kuingia kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo zaidi ya mara moja lakini polisi hawajachukua hatua yoyote hadi mpaka wananchi wanapoteza imani na jeshi hilo hasa kituo cha Mbezi Mwisho kwa kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Aliongeza kuwa viongozi wa eneo hilo wameshindwa kushughulikia suala hilo kwa kuwa baadhi ya watoto wao ni wahusika wa matukio hayo na kuwa polisi hawafiki kwa wakati wakipatiwa taarifa na upelelezi wa kesi kuhusu matukio hayo unachelewa hivyo kuwazidishia hofu wananchi.
Alitaja maeneo wanayopenda kukaa vijana hao kuwa ni karibu na nyumba moja isiyoisha ujenzi wake - pagala - iliyopo karibu na nyumba ya mjumbe aliyetajwa kwa jina la baba Elia na eneo la karibu na ghara la pikipiki la Masawe na nyuma ya maabara moja ya Mama Gema.
Wananchi hao wamemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Siro, kuwasaidia katika jambo hilo linalorudisha maendeleo yao nyuma ikiwezekana wawekewe kituo kidogo cha polisi eneo hilo ukizingatia kile wanachokitegemea cha Kibamba CCM kufungwa kuanzia saa 12 jioni hivyo kutoa mwanya kwa wahalifu kufanya matukio yao bila ya woga.
Vijana wanaofanya matukio hayo wamedaiwa kuvaa mavazi ya kike madera ili waweze kuficha siraha zao na kupita kirahisi barabarani bila ya kutambuliwa na kushukiwa kiurahisi.
"Tunaomba viongozi wa serikali kuingilia kati baadhi ya maeneo ambayo hayajaendelezwa maana yamekuwa vichaka vya kujificha wahalifu kabla na baada ya matukio," alisema mzee huyo.
Alisema hapo Kibwegere kunamaeneo mengi ambayo hayajaendelezwa zikiwepo nyumba ambazo hajijaisha ujenzi wake hivyo wanamuomba waziri mwenye dhamana kutembelea eneo hilo ikiwezekana kuyarudisha serikalini ili kusaidia kuondoa kero hiyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo wa Kibwegere CCM, aliyejulikana kwa jina moja la Nyingi, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa wananchi wamekuwa wagumu katika ushilikishwaji wa ulinzi katika eneo hilo.
"Tulijaribu kuwashirikisha wananchi katika suala zima la ulinzi na usalama katika eneo letu kwa kufuata muongozo wa jeshi la polisi lakini muitikio ulikuwa mdogo kwani kuna baadhi yao walidai wao hawana vitu vya thamani hivyo walio na uwezo ndio washiriki mchakato huo.
"Hatujui ni nini kilichowafanya washindwe kujitokeza katika jambo hili lakini hapa kwetu kunachangamoto kubwa ya wananchi kujitokeza katika shughuli za maendeleo kwa mfano ujenzi wa hata madarasa ya shule watu hawajitokezi licha ya kuwepo kwa msongamano wa wanafunzi kwa kukosa madarasa," alisema Mwenyekiti huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne Murilo, alisema kuwa mfumo wa ulinzi uliopo kuanzia kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya kata unawasaidia polisi kujua changamoto za wizi zilizopo katika maeneo hayo hivyo hata tukio la uhalifu linapotokea polisi hufika kwa wakati eneo la tukio.
"Katika kila kata Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa husika na wao ndio wanatoa taarifa polisi ya tukio lolote la uhalifu na katika maeneo hayo unayoyataja sijapata taarifa zozote za uhalifu nakuomba wasiliana na viongozi hao kwanza halafu unipe mrejesho," alisema Kamanda Muliro.
Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Werema Werema hakutofautia na maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibwegere CCM kuhusu changamoto iliyopo ya wananchi kushiriki katika suala zima la ulinzi na usalama katika eneo hilo.
"Kama ulivyoongea na mwenyekiti na mimi siwezi kuwatofauti naye kwani aliyoongea ndio niliyonayo hivyo kama ni kupata ya nyongeza karibu ofisini tuzungumze," alisema Werema.
No comments:
Post a Comment