Harbinder Sethi |
Na Dotto Mwaibale
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru kwa mara nyingine mshtakiwa Harbinder Sethi akatibiwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ndani ya siku 14.
Korti imesema iwapo hilo halitatekelezwa, mkuu wa gereza afike mahakamani kujieleza. Sethi yupo mahabusu katika Gereza la Segerea.
Amri hiyo ya mahakama imetolewa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai kesi ilipangwa leo Ijumaa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba shauri lipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo, wakili Joseph Makandege anayemwakilisha Sethi alieleza kuwa kumekuwepo mfululizo wa amri za Mahakama zikiagiza mteja wake akapatiwe matibabu na kufanyiwa uchunguzi Muhimbili.
“Hadi leo asubuhi tuliwasiliana na mteja wetu na kubaini hajapelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kama amri za Mahakama zilivyoagiza, hivyo ni rai yetu kwamba kitendo hicho cha kutotekelezwa amri za Mahakama ni ukaidi wa amri halali za Mahakama yako tukufu,” amesema Makandege.
Alisema kwa kuwa upande wa mashtaka umekaidi amri za Mahakama, anaomba itoe adhabu inayostahili.
Makandege alisema kitendo cha upande wa mashtaka cha kutotekeleza amri za Mahakama kinasigana na kukiuka mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Mashtaka .
“Mkurugenzi wa Mashtaka katika kutekeleza majukumu yake anapaswa kuongozwa na kutenda haki, lengo ni kutogeuza mashtaka ya jinai na mahakama kuwa ni vyombo vya utesaji,” amesema.
Ameomba Mahakama itoe adhabu stahiki kwa kuwa hilo linaonyesha dhahiri kuwa mashtaka yaliyopo ni ya hila yenye lengo la kuwaadhibu washtakiwa na hasa mshtakiwa wa kwanza Sethi kabla hawajahukumiwa.
Wakili Makandege ameiomba Mahakama iitupilie mbali hati ya mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa ili Sethi apate wataalamu wa matibabu yake katika hospitali ikiwemo Muhimbili.
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai tatizo limeshajitokeza katika utekelezaji wa amri za Mahakama.
Swai amedai Magereza wamekuwa wakiwatibu wafungwa na mahabusu hata pasipokuwa na amri ya Mahakama.
Alisema kilichojitokeza ni utaratibu wa kumpeleka Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Tumejitahidi kuwasiliana na Magereza wapo katika hatua za mwisho, tunaomba muda wa ziada ili tuiwezeshe Magereza kukamilisha utaratibu wa kumpeleka Sethi Muhimbili, hatujakataa tunaomba muda,” amesema Swai.
Hakimu Huruma Shaidi amesema ni lazima amri za Mahakama zifuatwe. Ameahirisha kesi hadi Oktoba 13.
Alisema hadi siku hiyo, Sethi awe ameshapata matibabu na iwapo atakuwa hajapatiwa, mkuu wa gereza alipo afike mahakamani kujieleza.
Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi wakidaiwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh309,461,300,158.27.
Wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
No comments:
Post a Comment