Jana, Disemba 16, 2017, Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilifanya kikao chake cha dharura jijini Dar es salaam, lengo likiwa ni kujadili hali ya kisiasa ndani na nje ya Chama, Hali ya Uchumi wa Nchi, kupokea taarifa juu ya mwenendo wa Chaguzi ndogo katika Kata 43 nchini uliofanyika Novemba 26, 2017, pamoja na kutoa uamuzi juu ya ushiriki wa Chama katika chaguzi ndogo zilizotangazwa karibuni na tume ya uchaguzi nchini (NEC) na kutarajiwa kufanyika Januari 13, 2018.
A: Hali ya Nchi (Kisiasa na Kiuchumi)
Kamati Kuu ilijadili mwenendo wa matukio tangu ilipotoa taarifa yake juu ya kuisnyaa kwa uchumi wa nchi pamoja na taarifa za takwimu za Serikali. Tangu kukamatwa kwa Kiongozi wa Chama, kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, kuhojiwa kwa Katibu Mkuu wa Chama, Kuzuiwa kwa simu ya Kiongozi wa Chama, pamoja na Kompyuta za Chama pamoja na wito wa kutaka kuihoji Kamati Kuu nzima ya Chama kwa sababu ya taarifa yake juu ya takwimu za Serikali. Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo inapinga unyanyasaji unaofanyika dhidi yetu kwa sababu tu ya chama chetu kuzungumzia masuala ya Uchumi wa nchi unaosinyaa.
Juzi, Disemba 13, 2017 Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeitaka Serikali itazame upya vyanzo vyake vya takwimu za uchumi ili kupata picha halisi ya Hali ya uchumi wa Taifa letu. IMF wamethibitisha kuwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania unashuka (unasinyaa) kutoka 7.2% mpaka 6.8%, na kwamba Takwimu za Serikali ni lazima zitazamwe upya. Jambo ambalo sisi ACT Wazalendo tulilisema kabla.
Jeshi letu la Polisi halijavamia Ofisi za IMF na kumuweka ndani Mkurugenzi wake mkazi hapa nchini, inasikitisha kwamba Serikali inawasikiliza na kuheshimu zaidi maoni ya kiuchumi ya IMF kuliko yanayotolewa na Watanzania. Maoni kama ya IMF yalipotolewa na ACT Wazalendo yalisababisha unyanyasaji mkubwa kwa Viongozi wetu. Tunatarajia kuwa Jeshi la Polisi litarudisha vifaa vyote vya chama lilivyo navyo, na kutuacha kuendelea na uchambuzi wa shughuli za Serikali kwa uhuru.
Jambo moja muhimu ambalo watu wa IMF wameiambia Serikali ni suala la kuheshimu Bajeti. Mtakumbuka tulieleza katika kikao kilichopita kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeanza tabia ya kutumia fedha za Mashirika ya Umma bila kufuata taratibu za sheria. Kwa mfano mapema katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali ilipata gawio la shilingi bilioni 300 kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutokana na faida ya benki hiyo mwaka 2015/16. Taarifa juu ya gawio hilo inapatikana katika wavuti ya BOT.
Kinyume na utaratibu, Serikali haikutoa taarifa juu ya gawio hili popote kwenye taarifa zake za kiFedha. Mapato haya hayakupelekwa Bungeni kugawiwa kwa mujibu wa sheria. Taarifa ni kuwa Serikali iliamua kutumia fedha hizi kulipia Mkandarasi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato, pamoja na madeni ya ndege za Bombardier na Boeing bila kufuata taratibu za sheria za fedha na bila Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG kuidhinisha kwa mujibu wa Katiba. Utaratibu unataka fedha kuingia kwenye Mfuko Mkuu (Consolidated Fund) na kisha kuidhinishwa na CAG, na ndipo Serikali kuanza kutumia.
Shilingi bilioni 300 kutumika na Serikali bila kushirikisha Bunge na kufuata sheria za nchi ni kusigina Katiba na kudharau Taasisi za Uwajibikaji za nchi. Kamati Kuu inamtaka CAG afanye ukaguzi maalumu wa fedha hizi na kutoa taarifa kwa Bunge, ili Bunge lichukue hatua za kuiwajibisha na kuisimamia Serikali ipasavyo.
Kamati Kuu pia ilipokea taarifa juu ya hali ya usalama nchini, hasa juu ya mwenendo wa watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Tukio la karibuni likiwa ni kupotea kwa Mwandishi wa magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications, ndugu Azory, mwandishi wa habari za uchunguzi, hasa wa eneo la Kibiti. Tunaungana na Familia yake, waandishi wenzake, wa ndani na Nje ya Nchi, pamoja na Watanzania wote, kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha Azory anapatikana akiwa hai.
B: Nafasi ya Chama chetu juu ya Miswada inayokwenda Bungeni mwaka 2018
Moja ya ajenda kubwa ya Chama chetu ni Hifadhi ya jamii. Chama chetu kinataka haki ya hifadhi ya jamii kwa kila raia ili kuwa na Taifa ambalo raia wake wote wana bima ya afya na uhakika wa pensheni uzeeni. Katika ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu tuliahidi mabadiliko makubwa ya mfumo wa hifadhi ya jamii ikiwemo kuunganisha mifuko iliyopo na kubakia na mifuko 3 tu. Mifuko miwili ya pensheni, na mfuko mmoja ni mfuko wa Taifa wa bima ya afya.
Serikali imeamua kutekeleza wazo letu hilo na tayari muswada wa sheria ya hifadhi ya jamii umewasilishwa bungeni kwa ajili ya kuanza kufanyiwa kazi na kuunda mifuko miwili tu. Tunapongeza hatua hii ya Serikali kuchukua mawazo yetu na kuyafanyia kazi, japo utekelezaji wake unafanyika vibaya, na hivyo utashindwa kuleta mafanikio tarajiwa. Kamati Kuu imeona hatua ya Serikali kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii kwa Wafanyakazi wa sekta rasmi, lakini imesikitishwa na hatua ya Serikali hiyo hiyo kutochukua nafasi hii kuweka mazingira wezeshi ya kisheria kwa Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na wote walio katika Sekta isiyo rasmi kuingia kwenye Hifadhi ya Jamii.
Kamati Kuu ya ACT Wazalendo pia imeona kuwa muswada huu unaopendekezwa bungeni una matatizo makubwa ambayo yanaweza kusababisha wazee wetu 120,000 kukosa kabisa pensheni, hasa watakaoanza kustaafu mwaka huu na waliokwishastaafu tangu mwaka 1999.
Jambo hili ni la kihistoria kidogo, tutaeleza. Serikali mwaka 1999 iliunda Mfuko wa PSPF kwa ajili ya watumishi wa umma. Kabla ya mwaka 1999 Watumishi wa Umma walikuwa hawachangii pensheni zao, bali walikuwa wanalipwa pensheni kutoka Hazina moja kwa moja kupitia bajeti za Serikali za kila mwaka. Hii ndio sababu wastaafu wetu nchini wanapokea pensheni ndogo sana ya shilingi 50,000 tu kwa mwezi na kabla ya hapo shilingi 20,000 tu.
Serikali ya Awamu ya 3 iliamua kuunda Mfuko wa Pensheni ili kuboresha pensheni za watumishi wa umma. Hata hivyo, Serikali ilitakiwa kulipa michango ya wafanyakazi wote walioajiriwa kabla ya mwaka 1999 (pre 1999). Serikali ya Rais Mkapa ilikubali deni lakini haikulipa. Serikali ya Rais Kikwete ilifanya uhakiki wa Deni na kukubali kulipa lakini haikulipa. Serikali ya Rais Magufuli imeamua kutolipa kabisa kisheria. Taarifa ni kuwa Serikali imeamua kuachana na madeni haya, na hivyo wastaafu 120,000 nchini wako hatarini kutolipwa pensheni kabisa, mara tu baada ya muswada huu mpya kupita na kuwa sheria.
Vile vile muswada wa sheria hii unabadilisha kanuni ya mafao, na hivyo kuathiri Wafanyakazi wa Umma hususan Walimu wetu wote nchi nzima ambapo pensheni zao zitakatwa kwa 50%. Jambo hilo litakuwa na athari kubwa mno kwa walimu nchini.
Muswada pia umeshindwa kuwaka bayana jawabu la kujitoa kwenye mafao kupitia kinachoitwa 'Fao la Kujitoa'. Muswada umeweka mamlaka ya fao jipya la kukosa ajira kwa Waziri badala ya kuweka masharti yake wazi kisheria na hivyo kuendeleza utata wa suala zima la wafanyakazi na michango yao. Muswada pia umeendelea na kiwango cha michango cha 20% licha ya tafiti zote kuonyesha kuwa ni kiwango kikubwa mno na kinaweza kupunguzwa mpaka 12% ambapo Waajiri wachangie 7% na waajiriwa 5% ya mishahara yao kwa mwezi kwenye mifuko ya hifadhi ya Jamii.
Muswada pia umeshindwa kuunganisha Michango kwenye mifuko na Fao la Matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Hali ya sasa ni kwamba wafanyakazi wanalipa mara mbili, wanalipia pensheni kwenye mifuko ya pensheni, na wanalipoa NHIF kwaajili ya Bima ya Afya. Wakati Fao la Afya ni kitu kinachopaswa kuwa sehemu ya faida za mafao ya kuingia kwenye Hifadhi ya Jamii.
Kamati Kuu imeiagiza Sekretarieti ya Chama kuanza kazi ya kuhamasisha makundi ya vyama vya Wafanyakazi nchini kuungana na kusimama pamoja kuboresha muswada wa Sheria hii. Lengo likiwa muswada huu usiende Bungeni ili uboreshwe na kulinda maslahi ya wazee wetu wastaafu na wastaafu wajao.
Kamati Kuu imeagiza Chama kuitisha kongamano la wazi kuvileta pamoja vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi wenyewe na wadau wengine muhimu ili kujadili sheria mpya ya pensheni na kujiunga na vyama vya wafanyakazi kuboresha muswada ili kutunga sheria inayohakikisha kuwa kila Mtanzania anakuwa na haki ya Hifadhi ya jamii.
Muswada mwengine ni muswada wa Sheria Mpya ya Vyama vya Siasa nchini, miongoni mwa miswada mibaya zaidi kuwahi kutokea nchini, muswada ambao ukiachwa kama ulivyo na ukawa sheria basi utafuta siasa za vyama vingi nchini.
Maana ni muswada unaompa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini mamlaka ya Udhibiti na Uendeshaji wa Vyama na kupoka mamlaka hayo kwa Vyama vyenyewe kupitia wanachama. Hata zuio haramu la mikutano ya hadhara nchini limewekwa kisheria katika mswada huo.
Kamati Kuu imeiagiza Sekretarieti ya Chama kuanzisha mara moja mazungumzo na Vyama vingine vya upinzani ili kuunganisha nguvu kuupinga muswada huu unaokwenda kurudisha nchi kwenye mfumo wa Chama kimoja cha siasa.
C: Ushiriki wa Chama Kwenye Uchaguzi wa Marudio wa Januari 13, 2018
Kamati Kuu ilijadili na kutathmini kwa kina yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa Novemba 2017. Kwenye uchaguzi huo, ilikuwa dhahiri kuwa;
I. Chama Tawala na Serikali yake kiliongeza matumizi ya mabavu kupitia vyombo vya dola hasa jeshi la polisi ili kuweka mazingira ya kushinda uchaguzi
II. Chama Tawala kilihakikisha kinawatumia vyema watendaji wa halmashari wanaohusika na usimamizi wa uchaguzi ambao wengi waliteuliwa kwa misingi ya ukada kwa Chama hicho ili kujihakikishia ushindi.
III. Mazingira yalipoonekana dhahiri kuwaelemea, Chama Tawala walitumia njia za kimabavu Kama vile kuvamia viongozi, kuteka viongozi, au kuwaweka mahabusu viongozi na mawakala
IV. Kila mbinu ilipoonekana kugonga mwamba, kwenye maeneo kadhaa, Chama Tawala, kwa kutumia vyombo vya dola kiliamua kujitangazia ushindi kimabavu licha ya matokeo kuonesha kuwa wameshindwa
V. Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC ilionekana kutojali kabisa hitilafu zilizojitokeza na kuchukua hatua kurekebisha kabla ya kuitisha Uchaguzi Mpya.
Kutokana na vitendo hivyo, ni dhahiri kwamba uwanja wa demokrasia nchini umevurugwa sana na mchakato mzima wa uchaguzi huru na wa haki kuharibiwa kabisa. Hivyo basi, Kamati Kuu ya Chama chetu imeazimia kuwa Chama chetu KISISHIRIKI kwenye uchaguzi ujao wa marudio wa tarehe 13 Januari 2018.
Hata hivyo tunatambua kuwa kutoshiriki chaguzi tu haitoshi kwani haijibu swali la nini kinafuata baada ya kususia. Chama pia kinatambua kuwa Chama tawala kinafurahia kususiwa na kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kubinya Demokrasia ili Vyama vya upinzani viendelee kususia chaguzi zinazokuja.
Kamati Kuu imeuagiza Uongozi wa Taifa wa Chama kuwafikia wadau wote wa Demokrasia nchini na kuweka mikakati ya pamoja ya hatua za ziada za kuchukua ili kuboresha mazingira ya chaguzi za haki nchini kwetu, pamoja na kuweka shinikizo kubwa kwa Serikali kufanya mabadiliko muhimu ya kisheria, kiutendaji na kikatiba ili kuweka sawa uwanja wa mapambano ya Kidemokrasia.
Chama chetu kitavitembela na kuanzisha mazungumzo na Vyama vyote vya upinzani ili kuona njia bora zaidi ya kimapambano ya pamoja katika kukabiliana na vitendo vya sasa vya Chama Tawala cha kuvuruga uchaguzi huru na wa haki.
Chama pia kitautumia muda wa sasa na mwezi Januari Kama kipindi cha kushirikiana na Vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi wenyewe kupambana dhidi ya Muswada wa Sheria ya Pensheni ambao utawakosesha pensheni malaki ya wafanyakazi wa sekta ya umma hasa walimu kama utapitishwa kama ulivyo. Hatua hizi pia zitahusisha makundi ya walio kwenye sekta isiyo rasmi, kama wakulima, wavuvi, wamachinga, wajasiriamali nk, ambao sheria hii inawaacha nje kabisa.
ACT Wazalendo
Disemba 17, 2017
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment