Friday, December 8, 2017

MTOTO WA MIAKA 12 AUWAWA KIKATILI NA MWILI WAKE KUTUPWA MAKABURIN

Mwili wa mtoto  Lucia Thomas ambaye amefanyiwa ukatili ukiwa ndani ya Jeneza kwaajili ya kuagwa na kusafirishwa kuendelea Mkoani Mara Wilayani Bunda.
Baadhi ya majirani na ndugu jamaa na marafiki wakiwa nje kwaajili ya kuaga mwili wa marehemu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Edward akisisitiza kufungwa kwa vituo bubu vya kufundishia wanafunzi kwenye mtaa ambao anauongoza. 

Mchungaji wa Kanisa la heri wenye moyo safi , Samweli Samson akihubiria na kutoa neno la faraja kwa familia.

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye hali ya masikitiko na maombolezo.

Na,Joel Maduka,Geita

Mtoto Lucia Thomas  Mwenye umri wa miaka 12  amekutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa eneo la makaburi mtaa wa mkoani mjini Geita.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Edward amedai pamoja na kunyongwa hadi kufa, mwili wa mtoto huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Kiandege wilayani Bunda pia ulikuwa na dalili za kubakwa kabla ya kuuawa.

Mama Mkubwa wa mtoto  huyo  Bi, Grace Thomas amesema  hata wao wameshangazwa na tukio hilo kwani mtoto huyo alikuja Geita akitokea Jijini Mwanza akiwa salama na kwamba kwa mtut ambaye ametenda ukatili huo ni vyema  kwa vyombo vya sheria vikafuatilia kwa umakini hili waweze kumchukulia hatua za kisheria.

Mama Mzazi wa Mtoto huyo Bi, Mary Thomas alisema mwanaye alitoka nyumbani jana Alhamisi saa 12:30 jioni akiwa ameongoza na mtu aliyesema ni mwalimu wake wa masomo ya maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa maelezo kuwa anaenda kuchukua karatasi za mitihani ya somo la Uraia.

Aidha ameongeza kuwa baada ya kuona usiku umeingia bila mtoto kurejea nyumbani, alikwenda kwa mwalimu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la ambapo waliongoza hadi nyumbani kwa mwalimu aliyeondoka na mwanaye na kumkuta lakini akawatoroka kwa kujifanya anampa mtu begi alilolishika mkononi.

Baada ya mwalimu huyo kutorejea huku mtoto haonekani, waliendelea kumtafuta mtoto wake usiku kucha bila mafanikio ndipo alipoenda kutoa taarifa polisi alikotakiwa kurejea iwapo itapita saa 24 bila mtoto kurejea nyumbani.

“Kabla ya saa 24 kumalizika, taarifa zilinifikia kuwa mwili wa mwanangu umeonekana makaburini akiwa tayari amefariki huku ukiwa na michubuko shingoni na akiwa amefungwa kamba miguuni huku hana nguo ya ndani,” Bi,Mary alisema kwa uchungu.

Kutokana na tukio hilo, uongozi wa serikali ya mtaa wa mkoani umepiga marufuku vituo vyote vya masomo ya ziada eneo hilo na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinazotambulika kisheria badala ya vituo vya vichochoroni.

No comments: