Tuesday, February 13, 2018

BRITISH COUNCIL YATOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI JIJINI DAR ES SALAAM.


 Meneja Mradi wa Connecting Classroom kutoka British Council,Ephraim Kapungu,akimkaribisha Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni,Kiduma S.Mageni (kulia) kufungua mafunzo ya siku tatu ya uwezeshaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyofanyika katika Kituo cha Walimu cha Mzimuni kilichopo Magomeni jijini Dar es Salaam leo. Picha zote na Elisa Shunda


Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni,Kiduma S.Mageni (kulia) akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya uwezeshaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari yaliyofanyika katika Kituo cha Walimu cha Mzimuni kilichopo Magomeni jijini Dar es Salaam leo. Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirika la British Council Tanzania. Wanaomsikiliza Kushoto kwake ni Meneja Mradi wa British Council nchini,Ephraim Kapungu na Mwezeshaji wa taasisi hiyo,Edwin Shunda.

 Meneja Mradi wa British Council nchini,Ephraim Kapungu akizungumza na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wakati wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam leo.


Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni,Kiduma S.Mageni akizungumza katika ufunguzi huo.


NA ELISA SHUNDA - DAR ES SALAAM

Shirika la British Council nchini linawapatia mafunzo ya uongozi walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari ya siku tatu yanayofanyika katika Kituo cha walimu Mzimuni ambapo mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha na kuwaongezea  walimu hao uwezo wa kiungozi na kiutendaji pamoja na maarifa ya kiutawala kwa walimu wenzake anaowaongoza,wanafunzi, wazazi pamoja na jamii inayozunguka shule.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Ofisa Elimu wa  Manispaa ya Kinondoni,Kiduma Mageni amelipongeza Shirika la British Council kwa kujitolea kutoa elimu hiyo ambayo walimu wakuu hao wakiizingatia na kuifanyia kazi kwa vitendo itawaletea matokeo chanya katika shule wanazozisimamia na kuwajengea heshima katika utawala wao pamoja na jamii nzima inayoizunguka shule hiyo.

“Kitendo cha British Council kujitolea kutoa mafunzo ya uongozi ya uwezeshaji kwa walimu wakuu wa shule za sekondari na msingi ni jambo zuri la kuwashukuru sana wanaongeza chachu ya kumsapoti Rais Dk.John Pombe Magufuli katika chagizo la kauli yake ya Elimu Bure hivyo basi ninyi walimu tumieni fursa hii mnayoipata kujifunza mengi katika semina hii na kwenda kuifanyia kazi katika shule zenu mnazoziongoza naamini kwa kutumia mafunzo haya mtaenda kubadilisha fikra hasi kuwa chanya katika shule zenu zitakazoleta matokeo mazuri ya nidhamu,morali kwa walimu wa kufundisha na ufaulu wa kiwango cha juu kwa matokeo ya wanafunzi wenu” Alisema Mageni

Aidha Meneja Mradi wa Connecting Classroom Bwana Ephraim Kapungu kutoka British Council ambao ndio wafadhili wa mradi huo amesema, British Council imekuwa ikifanya kazi na wizara ya elimu katika kuwajengea uwezo wa kiuongozi wakuu  wa mashule, mbinu bora za ufundishaji kwa walimu wa darasani, na kuwawezesha viongozi wakuu wa elimu wakiwemo watunga sera kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kielimu ya kimataifa ili kujifunza na kubadilishana mawazo na viongozi wa nchi zingine.

“Sisi British Council kupitia mradi wa Connecting Classroom tumekuwa tukishirikiana na wadau wengine wa elimu pamoja na serikali katika kujengea walimu uwezo wa kuboresha na kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili  wanafunzi wenye uhitaji maalumu ili kuhakikisha wanapata fursa ya kupata elimu bora inayoendana na uhitaji wao lakini pia kupitia mradi huu tumekuwa tukiwezesha na kufadhili urafiki wa kielimu kati ya shule za Tanzania na shule rafiki kutoka nchini Uingereza” Alisema Kapungu.

Nao wa wawezeshaji wa mradi wa Connecting Classroom Bw. Frank Mhando na Edwin Shunda wamesema kuwa kupitia mafunzo hayo wanawajengea uwezo walimu katika nyanja za uongozi bora wa mashule, mbinu bora za  kufundishia na ushirikiano wa kielimu ili kuwapa maarifa mapya walimu wapate mawazo mapya ya kuweza kuwasaidia katika uongozi na ufundishaji.

Imeandaliwa na mtandao wa www.timetza.com

No comments: