Judith Ferdinand @BMG
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amefanya uzinduzi rasmi wa Kliniki ya Tiba Saidizi kwa Waathirika kwa Dawa za Kulevya iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Waziri Mkuu Majaliwa alifanya uzinduzi huo jana ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi Jijini Mwanza aliyoianza jumatano iliyopita mkoani Mwanza ambapo anakagua na kuzindua shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema ili kupambana na changamoto hiyo na kuwakomboa vijana ambao wamekuwa wahanga wa dawa za kulevya, serikali imeazimia kuanzisha kliniki za waathirika wa dawa za kulevya katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es salaam, Iringa na Mwanza.
Aidha alisema serikali itatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali kwa ajili ya vijana ambao ni wahanga wa dawa za kulevya na kuwasaidia kuwarudisha kwenye mienendo mizuri na kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Hata hivyo aliwaomba wananchi kuwapeleka hospitali walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya ili kupatiwa matibabu na pia kuwaamini wale ambao hupatiwa matibabu katika kliniki za aina hiyo kwani hubadilika mienendo yao na kuwa na maadili baada ya matibabu.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subi alisema jumla ya shilingi milioni 132 zimetumika katika ujenzi wa kliniki hiyo ikiwa ni ushirikiano baina ya serikali na wadau mbalimbali ikiwemo shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kupitia shirika la watu wa Marekani la Centres for Disease Control and Preventation (CDC).
Dkt.Subi alisema katika mkoa wa Mwanza waathirika zaidi wa dawa za kulevya ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa ambao kwa kiasi kikubwa wanaishi maeneo ya mjini na kubainisha kwamba maeneo yenye vijana hao katika Manispaa ya Ilemela ni Kirumba, Nyamanoro, Kitangiri, Bwiru, Bugogwa na Kayenze Jiji la Mwanza (Nyamagana) maeneo yanayokumbwa na hatari hiyo kwa wingi yakiwa ni Igogo, Nyakabungo, Nyegezi, Sahara, Rufiji, Igoma Liberty, Kapri Point na maeneo mengine ya halmashauri za mkoa wa Mwanza.
Alisema changamoto iliyopo ni asilimia kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya kutoona umuhimu wa kwenda kwenye matibabu bila kupelekwa na ndugu ama jamaa zao ambapo mwaka 2017 Hospitali ya Sekou Toure ilipokea watumiaji 113 walioathirika na pombe, waathirika 144 wa dawa za kulevya ikiwemo bangi na mirungi, ambao asilimia 77 walikuwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45.
Alitahadharisha kwamba matumizi ya dawa za kulevya ni hatari katika jamii hivyo wanajamii wajiepushe nayo kwani yana athari nyingi ikiwemo kudumaza maendeleo ya jamii kutokana na watumiaji wake kushindwa kufanya kazi pamoja na magonjwa mbalimbali ikiwemo virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na homa ya ini.
Baadhi ya waliokuwa wakitumia dawa za kulevya walikiri dawa za kulevya kusababisha madhara makubwa ambapo Nyamizi Sospeter alisema kwa kipindi cha miaka saba alichokuwa akitumia dawa za kulevya alikuwa akitumia njia yoyote ikiwemo wizi ili kupata pesa ya kununulia dawa hizo ambapo alishukuru kuanzishwa kwa kliniki hiyo kwani imewasaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya na sasa wameanza kuimarika kiafya.
No comments:
Post a Comment