Tuesday, March 27, 2018

MICHUANO YA COPA COCA-COLA UMISSETA 2018 YAZINDULIWA MKOANI DODOMA

Waziri Jafo akigawa zawadi ya mipira kwa baadhi ya shule za sekondari zitakazoshiriki. Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo akihutubia wakati wa uzinduzi huo.
Meneja wa chapa ya Coca-Cola, Sialouise Shayo, akiongea wakati wa uzinduzi huo. Waziri Jafo akikagua moja ya timu na kugawa vifaa kwa baadhi ya shule za sekondari
Waziri Jafo katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa UMISSETA baada ya uzinduzi.
Wakazi wa Dodoma walijitokeza kushuhudia uzinduzi.

Mashindano ya shule za sekondari ya UMISSETA ngazi ya mkoa yamezinduliwa mkoani Dodoma, na mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Waziri wa TAMISEMI,Selemani Jafo.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wanafunzi wa shule za sekondari,walimu, viongozi mbalimbali wa mkoa na michezo.

Mbali na uzinduzi,Waziri alikabidhi vifaa vya michezo kwa timu za sekondari zilizokuwepo kwenye uzinduzi huo.Vifaa hivyo vya michezo vimetolewa na kampuni ya Coca-Cola ambayo ni mdhamini mkuu wa mashindano haya,ambapo mwaka huu imepanga kutoa vifaa vya michezo kwa shule 4,000 za sekondari zilizopo sehemu mbalimbali nchini.

Waziri Jafo, alisema kampuni ya Coca-Cola kwa kudhamini mashindano hayo kutafanikisha jitihada za kuendelea kuibua vipaji vya wachezaji chipukizi wa michezo ya soka ,mpira wa kikapu na pia kupitia mashindano haya kutaibuliwa vipaji vya wanariadha watakaotamba katika kipindi cha miaka ijayo. 

 “Nafahamu kuwa udhamini wa Coca-Cola wa mashindano haya unamalizika mwishoni mwa mwaka huu,lakini natoa ombi maalum iangalie uwezekano wa kuendelea kuongeza kipindi cha kutoa udhamini .

Mashindano haya ya UMISSETA ni tanuru ya kuibua vipaji na rekondi ipo ya wachezaji wazuri wa soka waliofanya vizuri na wanaoendelea kufanya vizuri katika michezo mbalimbali,vipaji vyao viliibuliwa katika mashindano haya wengi pia wamechezea baadhi ya klabu kubwa za soka za Yanga na Simba”alisema. 

Waziri Jafo,alitoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza kudhamini mashindano ya michezo kuanzia ngazi za chini,na kusisitiza kuwa sekta ya michezo inazidi kukua ambapo hivi sasa lengo lake sio burudani bali ni biashara kubwa na ushahidi wa suala hili upo wazi. 

Jafo pia alishauri kamati ya maandalizi ya mashindano haya ya UMISSETA ,kwa miaka ijayo ihakikishe uzinduzi wake ngazi ya kitaifa unafanyika mkoani odoma badala ya mkoani Mwanza ili yaendane na mkakati wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kuhamishia shughuli za serikali katika mji wa makao makuu ya nchi. 

Kwa upande wake Meneja wa chapa ya Coca-Cola, Sialouise Shayo,alisema kampuni ya Coca-Cola inajivunia kuwa mdhamini wa mashindano haya kwa kipindi cha miaka 3 mfulilizo na inaamini vipaji vingi vimeibuliwa na vitaendelea kuibuliwa .

”Udhamini wetu katika mashindano haya tumejikita katika kutoa vifaa vya michezo kwa wachezaji wanaoshiriki kuanzia ngazi ya mkoa hadi ngazi ya taifa,kutoa mafunzo kwa makocha wanaofundisha timu na zawadi kwa timu zinazofanikiwa kufanya vizuri”,alisisitiza 

Shayo alisema mbali na uzinduzi wa UMISSETA ngazi ya mkoa uliofanyika mkoani Dodoma utafanyika katika mikoa ya Kagera,Tanga,Mtwara,Singida na Zanzibar ambapo uzinduzi kwa ngazi ya taifa utafanyika mkoani Mwanza ambapo pia mashindano haya yatafanyika.

No comments: