Thursday, March 8, 2018

MWENYEKITI WA MTANDAO WA WANAFUNZI ABDUL NONDO AOKOTWA IRINGA BAADA YA KUPOTEA KWA SIKU KADHAA

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyekuwa hajulikani alipo tangu usiku wa kuamkia jana na kuacha ujumbe usemao “I AM AT HIGH RISK”, amepatikana Mafinga mkoani Iringa.
 Tokeo la picha la ABDUL NONDO
Mkurugenzi wa Idara ya Sheria ya Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Paul Kisabo amesema  kwamba Abdul Nondo amepatikana mkoani Iringa katika wilaya ya Mafinga jana jioni baada ya kuzinduka na kujikuta ametupwa barabarani.

“Nondo amepatikana Mafinga katika Kituo cha Polisi hivi punde, amezinduka na kujikuta akiwa ametupwa, akauliza watu eneo alipo ndipo wakamwambia yupo Mafinga, amejikokota na kuelekea kituo cha polisi kuripoti.

“Kilichomsaidia alikuwa anakumbuka namba mojaya dada yake ambayo alikuwa ameikariri kichwani, ikabidi aombe simu polisi, kumpigia dada yake ambaye naye alijulisha baba yake mdogo aliyepo Dar es Salaam kuwa ndugu yao amepatikana.

“Nondo ameongea na baba yake mdogo kupitia simu ya polisi na kudai kuwa laini zake zote za simu lakini simu yake bado anayo na yupo salama,” -Paul Kisabo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amethibitisha kupatikana kwa mwanafunzi huyo, Abdul Nondo na kusema sasa bado yupo katika Kituo cha Polisi Mafinga akitoa maelezo.

No comments: