Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho kilimdekeza kwa kiasi kikubwa Katibu mkuu wake, Seif Sharif Hamad.
Profesa Lipumba amesema hali hiyo imesababisha CUF kushindwa kupata viongozi watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kutokuwepo kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar aliyepo upande wa Maalim Seif, Nassor Ahmed Mazrui amesema chama hicho hakimdekezi katibu huyo, bali kinaringia kura anazopata kila anapowania urais wa Zanzibar.
Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 18, 2018 wakati akifungua kikao cha kwanza cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF kinachofanyika makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam.
“CUF tumemdekeza kwa muda mrefu na zile nyimbo tulizokuwa tukiimba ya kuwa akipata Seif tumepata sote zilikuwa zimemuingia kichwani kwelikweli na yeye alitafsiri kuwa akikosa Seif tumekosa sote,” amesema.
“Matokea yake tumekosa kuwa na uwakilishi katika Baraza la Uwakilishi jambo ambalo limetuathiri kisiasa hasa Zanzibar. Hili kosa kubwa tuliowakosea Wazanzibari”
Katika ufafanuzi wake, Mazrui amesema Maalim Seif anabebwa na kura za urais wa Zanzibar na wananchi wameonyesha wazi kumpenda na kumkubali.
“Maalim Seif anatamba na kura na watu wanampenda. Kura ni demokrasia ndicho anachoringia katibu mkuu wangu, mbona yeye (Profesa Lipumba) akigombea anapata kura chache na kila kukicha zinashuka hajioni?” amehoji Mazrui.
“Mimi ni mfanyabiashara nikiona mambo hayaendi sawa katika shughuli zangu nafanya mabadiliko ili kuimarisha . Kwa hiyo CUF tunamthamini sana Maalim Seif na kila kukicha anatuongezea majimbo.”
Amesema ziara yake ya Pemba imesaidia kuimarisha chama hicho na hivi sasa wananachi na viongozi wa CUF wanaijua vyema Katiba ya chama tofauti na hapo awali.
No comments:
Post a Comment