Thursday, March 1, 2018

WANAWAKE ACT WATAKA WACHUNGUZI NJE YA JESHI LA POLISI, UTEKWAJI WA RAIA

TAARIFA YA NGOME YA WANAWAKE KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA HALI NA MWENENDO WA SIASA NA HAKI ZA RAIA NCHINI

Haki za Binadamu zinavunjwa, Haki za kiraia zinakandamizwa, Demokrasia inafutwa:


Ndugu Wahandishi wa habari awali ya yote  Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT Wazalendo ilifanya kikao chake jana na kujadili, kutafakri na kufikia maazimio kadhaa juu ya hali yetu kama nchi kisiasa na kijamii hivyo tumeamua kuwaita Leo kuwashirikisha mambo kadhaa kuhusu hali inayoendelea hapa Nchini.

Ngome ya Wanawake ya Act Wazalendo inasikitishwa na inapinga na mwenendo wa hali ya kisiasa ndani ya nchi yetu ambapo vitendo na matukio yenye kukiuka Utu, heshima ya binadamu,  demokrasia, haki za  kiraia na kisiasa kutamalaki [Kushamiri].

Matukio hayo yanaashiria kupotea kwa Utu na Usawa wa binadamu, tishio kubwa dhidi ya uwepo wa mfumo wa vyama vingi, uhuru wa maoni, pamoja na amani na usalama wa nchi yetu.

Tangu utawala wa awamu ya tano uingie madarakani tumeshuhudia kuongezeka kwa matukio mbalimbali ya kusikitisha kinyume na utamaduni mzuri ambao nchi yetu ilikuwa ikiujenga.

 Matukio ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha, kutekwa na kuteswa hasa na jeshi la polisi sasa yamekuwa sehemu ya maisha ya watanzania! Hali hii haikubaliki, na tumeona tujitokeze na kuchukua wajibu wa kusema na kukemea ili kulinusuru taifa na hatari inayolinyemelea..


MFUMO WA VYAMA VINGI NI TAKWA LA KIKATIBA, SI HISANI YA WATAWALA.

Nchi yetu iliingia katika mfumo wa vyama vingi rasmi mwaka 1992 kutokana na mapambano ya muda mrefu ya wananchi waliokuwa wakihitaji kusikika kwa sauti zao, lakini pia kuwa na ushindani katika mchakato wa kutafuta uongozi wa nchi.

 Mfumo huu tangu kuanzishwa kwake, umesaidia kuibua madhila na matatizo mengi ya wananchi ambayo hapo awali yalikuwa yakifichwa na watawala na hivyo watu kuendelea kuteseka pasipo kupata msaada.

 Mfumo wa vyama vingi ulileta fursa ya kuibua uozo ambao haukuwa ukiwekwa bayana na hivyo kufanya serikali na mamlaka kuwajibika ipasavyo kwa watu.

Hata hivyo, wakati tukiwa bado katika safari ya ujenzi na uimarishaji wa mfumo huo, tunashuhudia utawala huu wa awamu ya tano ukitenda na kuendesha nchi katika namna ambayo inaturejesha nyuma katika mfumo wa chama kimoja.

Moja kati ya mambo yanayofedhehesha sana katika utawala huu ni vitendo vya ukiukaji wa demokrasia ambavyo dhahiri vinakwamisha na kuhujumu mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi.

Hii leo, tunaona Bunge la Jamhuri ambalo ni chombo nyeti cha uwakilishi wa wananchi linahujumiwa na kupotezwa nafasi na heshima yake, Wananchi wamenyimwa fursa ya kufuatilia moja kwa moja mikutano ya wawakilishi wao wakijadili masuala yanayowahusu bungeni.

 Kinyume na awamu za utawala zilizopita, hivi sasa tunaona kurushwa kwa matangazo ya Bunge kukiwa ni kwenye kudhibitiwa kwa hali ya juu.

 Tunachoshuhudia ni mtu mmoja tu katika nchi hii, aitwaye Rais, ndiye anayeonyeshwa moja kwa moja kila shuguli aifanyayo.

 Hata wakati ambapo redio au televisheni ya taifa inapokuwa ikirusha matangazo ya Bunge, inapotokea Rais ana shughuli yoyote wakati huo huo, hata ikiwa ndogo kiasi gani, matangazo ya Bunge yanakatizwa na kurushwa ya Rais!

 Hali hii inashusha na kukandamiza haki na hadhi ya Bunge kama chombo cha wananchi wa Jamhuri.


MICHAKATO YA UCHAGUZI NI KAMA MCHEZO WA KUIGIZA.

 Pamoja na kwamba kwa upatikanaji na muundo wake, Tume yetu ya Uchaguzi si huru, lakini leo tunashuhudia dhahiri kabisa Tume ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi vikitumika na dola kuhujumu vyama vya upinzani katika chaguzi mbali mbali, Tunashuhudia chama tawala kikilaghai na kuwanunua wawakilishi wa vyama vya upinzani na kisha serikali inaiagiza Tume ya Uchaguzi kuitisha chaguzi kwa gharama kubwa.

Pia, tunashuhudia ukiukaji mkubwa wa sheria na haki katika chaguzi hizo kwa maslahi ya chama tawala.


Vitendo vya kuvuruga shughuli za kampeni kwa vyama vya upinzani,kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani,  kukamatwa ovyo viongozi wa vyama vya upinzani na kuwaweka ndani, yamekuwa ni matendo yanayotendwa na kusimamiwa na jeshi la polisi huku ima kwa kutumwa na viongozi waliopewa ridhaa na wananchi (watawala) au kutochukua hatua stahili dhidi ya unyanyasaji na ukandamizwaji.
Mambo haya yanaonyesha kwamba, serikali ya awamu ya tano chini ya John Pombe Magufuli, haitaki mfumo wa vyama vingi na inafanya kila juhudi kuuhujumu.

 Sisi Ngome ya Wanawake ambao ni wazazi na walenzi wa taifa, tunapinga vikali hali hiyo na hatuko tayari kuiona ikitamalaki ndani ya nchi yetu kwani tunaelewa na kutambua umuhimu wa vyama vingi nchini katika kuleta changamoto za maendeleo.

Tungependa kuwakumbusha watawala ya kwamba, Mfumo wa Vyama vingi nchini ni takwa na hitaji la kikatiba na kisheria. Sura ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 3(1) inatambua uwepo wa Mfumo wa Vyama vingi nchini. Kitendo cha rais aliyeko madarakani, aliyeingia kwa mujibu na kiapo cha Katiba hiyo, kuzuia shughuli za kisiasa za vyama (vya upinzani) ni kitendo cha dharau kubwa kwa wananchi ambao ndio msingi wa uwepo wa taifa na Katiba.

Ni rai yetu kwa Rais na utawala wake, kwamba aongoze nchi kwa kuheshimu matakwa hayo ya kikatiba na siyo kwa matakwa na maslahi yake binafsi. Madhara ya kuzuia mfumo wa vyama vingi kuchukua nafasi yake stahiki, ni makubwa mno kwa utulivu na amani ya nchi. 

HAKI ZA KIJAMII KUPOROMOKA NA HAKI ZA KIBINADAMU KUENDELEA KUKANDAMIZWA.

Wakati tafiti zikionyesha kuporomoka kwa idadi ya watu kutoka makundi maalum (Watoto, Wajawazito na wazee) wanaopaswa kupata matibabu bila malipo wanalazimika kulipia, Idadi ya wagonjwa wanaochangia kitanda au godoro kuongezeka, Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya kuwa ni tatizo, Gharama za huduma katika hospitali za umma kuwa juu na Upungufu wa madaktari.

Upande mwingine tunashuhudia ndani ya nchi yetu matukio mabaya ya watu kupotea, watu kutekwa, kupigwa na hata kuuliwa bila hatua zozote za maana kuchukuliwa na vyombo vyenye dhamana husika. Mbaya zaidi ni kwamba, vyombo vinavyotegemewa kuchukua hatua za kiusalama, ndivyo vinakuwa watuhumiwa wa kwanza wa matendo na matukio haya.

Wanasiasa, waandishi, wanaharakati na hata raia wamepotea, kutekwa, kupigwa risasi, na kuuliwa pasipo sababu za msingi wala pasipo kuwa na maelezo yenye kueleweka.

 Tunasikitishwa na tunapinga mwendelezo wa matukio haya kwani ni matukio ambayo yanapelekea kutoweka kwa amani na utulivu katika jamii zetu, jambo ambalo ni jipya katika utamaduni wa nchi yetu.

 Tungependa kuona haki za binadamu hasa haki ya kuishi ikiheshimiwa si kwa maneno, bali kwa dhati ya matendo.

 Serikali yoyote yenye kuruhusu au kutochukua hatua pindi ambapo raia wake wanapouawa kwa namna au sababu yoyote ile, inakuwa imepoteza uhalali wa utawala wake. Wajibu wa kwanza wa dola ni kuhakikisha usalama na uhai wa watu wake pasipo kubagua kwa mitazamo ya siasa (vyama), ukanda,  udini au ukabila.


NINI KIFANYIKE?

Jambo la kwanza, Tunahitaji kurejea mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Katiba mpya itakuwa ni jawabu la msingi kwa changamoto nyingi tulizozizungumzia katika taarifa yetu. Ni muhimu serikali ikatambua kuwa Katiba Mpya ni hitaji la Taifa. Msimamo wetu kama chama, na ambao tuliueleza ndani ya Ilani yetu ya Uchaguzi, ni kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya kutoka pale Tume ya Jaji Warioba ilipoishia. Tunatoa rai kwa wadau na wananchi wote tuungane pamoja kuidai Katiba yetu Mpya ili tulinusuru taifa letu.

Pili, Tunaitaka serikali iache kujenga mazingira kandamizi na hofu, kutishia Wananchi  (Wanyonge ), kuwanyanyasa kiasi kwamba wanashindwa kupumua na kufaidi utanzania uliojengwa katika misingi ya Utu na heshima kwa binadamu wote bila kujali uvyama, udini na ukabila. Kwa kujenga mazingira ya kuogopesha, yenye wasiwasi na kuzua taharuki kila uchao kwa kutumia vyombo vya dola kuwanyamazisha Wananchi. Sio vema kuchukulia kwamba kila anayehoji, anayedadisi, anayetoa mawazo mbadala ni mchochezi, mamluki hivyo anapaswa kuangushwa kwa mkono wa Chuma ima kwa kudhalilishwa, kufirisiwa, kusukumwasukumwa, kujeruhiwa, kuteswa au kuuliwa.  Ili kujenga na kudumisha amani na utulivu wa Nchi yetu tunahitaji mazingira yanayofaa na yanayolinda uhuru wa kudodosa, kudadisi, kuchunguza, kutoa mawazo mbadala, kuhoji na kupinga mienendo yote itakayolitia taifa letu kwenye vurugu na kudumaa kimaendeleo.

Tatu, Tunaitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya  Rais Magufuli iache ukandamiza wa demokrasia na haki za binadamu.

Ni muhimu nchi iendeshwe kwa kufuata misingi ya haki na Utu. Nchi inayominya haki dhidi ya wananchi wake huzaa taharuki, hofu na hali ya unyonge hivyo ni rahisi kutumbukia katika machafuko kwakuwa wananchi watachoka kukandamizwa, kubuluzwa, kunyanyaswa na kuonewa.

Jeshi la Polisi liache kutumika kukandamiza raia,kwani Wajibu wa jeshi hilo siyo kukandamiza raia, bali ni kulinda mali na haki zao.

Kutokana na jeshi la Polisi kutokutimiza wajibu wake ipasavyo,wakati huu imewafanya wananchi wajihisi wapo hatarini zaidi wanapokuwa katika mikono ya Polisi kuliko sehemu isiyo na Polisi, hali hii haipaswi kuachwa iendelee.

Nne, Tunaomba mfumo wa vyama vingi uachwe ufanye kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria. Kitendo cha dola kuhujumu mfumo huu hakikubaliki. Tunaikumbusha serikali iliyoko madarakani kwamba, imeingia kwa mujibu wa Katiba na kwa mfumo wa vyama vingi. Juhudi zozote za kuhujumu mfumo huu tunazichukulia kuwa juhudi za kuhujumuu Taifa na  hatutazikubali kamwe.


Tano, Tunaomba iundwe Tume huru ya Uchunguzi ili kusaidia kufanya uchunguzi juu ya matukio ya mauaji na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani, kama vile kutekwa kwa watu mbalimbali katika nchi yetu. Tunadhani uchunguzi huru nje ya ule utakaofanywa na Jeshi la polisi utajenga na itakuwa rahisi  kukubalika na utatoa ukweli wa mambo na kuanika kama utakavyoonyesha kwakuwa Jeshi letu la Polisi limekuwa mtuhumiwa wa kwanza kwenye kushiriki vitendo hivyo.


Sita, Tunapenda kuunga mkono pendekezo la Kiongozi wa Chama chetu Ndg. Zitto Kabwe alilolitoa mjini Arusha tarehe 24/2/2018 wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya nchi kisiasa na maendeleo ya ziara yake kwenye Kata tunazoongoza.  Pendekezo hilo ni Kufanyika kwa Mkutano wa Kitaifa wenye kuwahusisha wadau wote kujadili na hali ya mwenendo wa siasa za nchi yetu, na kukubaliana mkondo mzuri wa kuchukua ili kuepusha migongano.


Chiku A. Abwao
Mwenyekiti Ngome ya Wanawake Taifa
ACT Wazalendo


Imetolewa leo tarehe 01 Machi, 2018WA

No comments: