Friday, July 1, 2022

Mohamed Mchengerwa : Tamasha la Utamaduni la Kwanza la Kitaifa litazinduliwa kesho Julai 2, 2022 uwanja wa Uhuru Mkoani Dar es salaam

Na. Vicent Macha.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema Tamasha la Utamaduni la Kwanza la Kitaifa litazinduliwa kesho Julai 2, 2022 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akiongea na waandishi wa Habari Mkoani Dar es salaam.

Amebainisha hayo leo Julai 1, 2022 jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema uzinduzi huo utaanza saa 2:00 asubuhi na Mgeni Rasmi ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Tamasha la Utamaduni la Kwanza la Kitaifa kuwanzia tarehe 01-03 Juali, 2022 litakaloongozwa na Kauli mbiu ‘Utamaduni wetu, Fahari yetu, tujiandae kuhesabiwa, Kazi Iendelee,” amesema Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amebainisha kwamba Tamasha hilo litahusisha matukio mbalimbali ikiwemo matembezi ya Hisani ya Utamaduni, maonyesho ya vyakula vya asili, burudani za ngoma za asili pamoja na usiku wa Taarabu utakaofanyika katika viwanja vya Coco Beach pamoja na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani Julai 7, 2022 jijini Dar es Salaam.

Amesema tamasha hilo linalenga kuamsha ari ya Watanzania kutambua, kutamini, na kuendeleza urithi wa utamaduni wa Mtanzania tuliourithi kutoka kwa wazazi wetu pamoja na kuchochea mchango wa Sekta ya utamaduni na sanaa katika maendeleo ya kijamii pamoja na kuenzi lugha ya Aushi ya Kiswahili.

Ameeleza kwamba kuandaliwa kwa Tamasha hili ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa akiwa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba, 2021 katika Tamasha la Utamaduni Mwanza.

Kwamba aliagiza matamasha haya yafanyike kwa mzunguko kila Mkoa ili Watanzania kujua mila na Desturi zetu za kila Mkoa na kila pembe ya Tanzania, pia kuandaa mashindano yatakayoshindaniwa na Mikoa yote ambapo mshindi atapata tuzo.

“Maelekezo hayo tunayatekeleza kwa vitendo,” amesema.

Akizungumzia kushusu usiku wa Taarabu, Waziri Mchengerwa amesema utafanyika Julai 3 mwaka huu kuanzia saa 8:00 alasiri hadi saa 6:00 usiku na utapambwa na wasanii mbalimbali nguli akiwemo Khadija Kopa, Patrcia Hilary, Sabaha Salum Mchacho na Abdul Misambano.

Wengine ni Mzee Yusuph na wengine, pia kutakuwa na vikundi mbalimbali kutoka Safina Modern Taarabu, First Class, Wana Nakshi, Rahat Zamani, Nandi Ikhwan Safaa, Chama cha Wasanii wa Muziki wa Taarabu Zanzibar pamoja na vikundi vya muziki huo kutoka nchi za Burundi, Kenya na Visiwa vya Comoro na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azan Zungu.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mikoa ya jirani na wananchi wote kwa ujumla bila kusahau ndugu, jamaa na marafiki na watu wote duniani watakaoshiriki.

No comments: