Friday, April 12, 2013

TAARIFA YA JUKWAA LA KATIBA JUU YA UCHAGUZI WA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA KATIKA VIJIJI, MITAA NA KATA AMBAKO KUMEKUMBWA NA DOSARI URUDIWE!




TAARIFA KWA UMMA



JUKWAA LA KATIBA TANZANIA (JUKATA) tunapenda kuchukua fursa hii kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuendesha zoezi la uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba katika ngazi ya vijiji, mitaa na Kata ambao umefanyika kote nchini hivi karibuni hata pamoja na kukumbwa na mapungufu yake makubwa.



Kama sehemu ya kazi na wajibu wetu, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumefanya tathmini ya mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba katika ngazi ya vijiji, mitaa na Kata ambao umefanyika mwanzoni mwa mwezi Aprili 2013. Kutokana na tahmini hiyo, pamoja na maoni kadhaa toka kwa wananchi wa kawaida wa mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na visiwani, JUKATA tunapenda kutoa maoni/mapendekezo kuhusu mchakato wa uchaguzi huo ulivyofanyika, huku tukibainisha dosari zilizojitokeza katika kuwachagua wajumbe wa mabaraza ya katiba katika ngazi ya vijiji, mitaa na Kata. Baadhi ya dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo ni kama ifuatavyo:


1.O DOSARI MBALIMBALI ZILIZOJITOKEZA KATIKA UCHAGUZI WA WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA


1.1 Itikadi za udini katika Uchaguzi wa Mabaraza


Katika maeneo kadhaa, uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba uligubikwa na hisia za kuwepo kwa upendeleo kwa itikadi za udini hivyo kupelekea wananchi kuwachagua wajumbe kwa misingi ya dini zao. Jukwaa la katiba limepokea taarifa kutoka kwa waangalizi wake walio katika mikoa yote nchini Tanzania kuwa mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba katika ngazi ya vijiji, mitaa na Kata uligubikwa na itikadi za kidini. Kwa mfano, makundi mbalimbali ya dini yalijipanga kuwapigia kura wagombea wa dini zao na si kuchagua kwa kuangalia uwezo wa mgombea wa nafasi hiyo na vigezo vya sifa vilivyowekwa katika Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba uliotolewa na Tume. Hali hii imetokea katika mikoa na wilaya nyingi hapa nchini. Mfano, waangalizi wa Jukwaa la Katiba katika Mkoa wa Dar es Salaam walibaini kuwa viongozi wa juu kabisa walitoa agizo la kuhamasisha waumini wao kuchagua wagombea wao dhidi ya wale wa dini nyingine. Kutokana na hilo, kulikuwa na malalamiko katika Kata za Kitunda, Ndumbwi na Kivukoni kuwa baadhi ya waombaji walio na sifa za chini walipitishwa katika ngazi ya Kata kwa kuwa tu walikuwa wa dini moja na Diwani au wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Taarifa kama hiyo imepokelewa pia kutoka wilaya za Biharamulo, Bukoba vijijini, Misenyi, Karagwe na Kilolo. Aidha kulikuwa na taarifa za ujumbe mfupi wa simu uliokuwa ukijaribu kueleza haja ya dini fulani kuingia kwa wingi katika Mabaraza ya Katiba. Jambo hili limetia doa mchakato huu na nchi yetu ambayo kwa miaka mingi ilikuwa mfano wa kuigwa katika kutenda haki bila kujali dini, rangi, kabila au itikadi ya mtu.



1.2 Itikadi za Kisiasa na vyama katika kuchagua wajumbe wa Mabaraza


Jukwaa la Katiba limebaini kuwa mbali na uchaguzi huo kugubikwa na itikadi za kidini pia itikadi za kisiasa zilitawala katika uchaguzi huo. Wagombea wengi wamechaguliwa kwa misingi ya uanachama wa vyama vya siasa watokavyo. Suala hilo lilijitokeza maeneo mengi ukivihusisha vyama hasa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF). Vyama hivi kila kimoja kilihamasisha wanachama wake kuchagua wagombea kutoka katika vyama vyao dhidi ya wagombea wa vyama vingine. Jukwaa la Katiba lina taarifa kuwa wafuasi wa vyama vya siasa walipita nyumba hadi nyumba kuomba kura kwaajili ya wagombea wao. Katika maeneo mengine viongozi wa kada mbalimbali za kisiasa katika vyama waliendesha kampeni za wazi kuhimiza kuchaguliwa kwa wagombea kutoka vyama vyao kinyume kabisa na nia nzuri ya Tume kuwa mchakato huu usitawaliwe na itikadi za vyama. Kwa mfano, katika mtaa wa Mwigobero “B” Manispaa ya Musoma mkoani Mara kulitokea vurugu kati ya wafuasi wa CCM na CHADEMA zilizosababishwa na tuhuma za kila chama kuleta mamluki wa kupiga kura. Pia waangalizi wa JUKWAA LA KATIBA waliopo Dar es Salaam wamethibitisha kuwa wagombea waliofika katika uchaguzi sehemu nyingi walifika na wapiga kura wao kutoka katika vyama vyao. Katika maeneo ya Mbezi Beach, wagombea waliwezesha wapiga kura kuja katika magari na malori kwa makundi makubwa. Aidha, zipo sehemu ambako “wasimamizi wa uchaguzi waliwauliza wagombea, kama wamekuja na wapiga kura wao” kama ilivyotokea Mtaa wa Kingugi kata ya Kiburugwa manispaa ya Temeke. Hii ilisababishwa pia na ukiukwaji wa mwongozo kwa vile majina ya wagombea na nafasi zao hayakubandikwa katika mbao za matangazo na maeneo ya wazi kabla ya uchaguzi. Katika kata ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, uchaguzi wa wajumbe ulilalamikiwa kufanyika kwa itikadi za kisiasa ambapo wagombea walichaguliwa kwa misingi ya ufuasi wa chama zaidi kuliko sifa na uwezo.


1.3 Vurugu katika Uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba


Uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba katika ngazi ya vijiji, mitaa na Kata ulitawaliwa na fujo, vitimbi na vurugu. Katika maeneo mengi kuliripotiwa vurugu hadi kupelekea mapigano. Jukwaa la Katiba limebaini sababu zilizochangia kutokea kwa vurugu hizo kuwa ni pamoja na kutofahamika kwa taratibu zilizoainishwa katika mwongozo wa uundwaji wa mabaraza kwa viongozi na wananchi kwa ujumla, viongozi kukiuka mwongozo kwa kutojua au kwa makusudi na jeshi la polisi kushindwa kutoa ulinzi madhubuti wakati wa uchaguzi au kwa kuombwa na wakurugenzi wa halmashauri, miji na manispaa ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi huu au kwa jeshi la polisi lenyewe kutumia intelijensia yake kutambua kwamba hili ni eneo mojawapo linalohitaji ulinzi kwakuwa ni tete kiusalama. Maeneo mengi yameripotiwa na waangalizi wetu kuwa na vurugu. Kwa mfano katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara katika mtaa wa Mtakuja kata ya Mwisenge vurugu zilizuka baada ya wananchi kukataa kuendelea na uchaguzi kwasababu usiku umeingia. Hii ilitokana na ucheleweshaji usio wa lazima wa kuanza kwa zoezi lenyewe la uchaguzi wa wajumbe. Hata katika Jiji la Dar es Salaam, maeneo ya Mwananyamala na Kinondoni yalikumbwa na vurugu hadi uchaguzi kuahirishwa tarehe 4 April na jaribio la kufanya tarehe 5 April nalo likashindikana kutokana na wananchi kupinga uonevu na ukiukaji wa taratibu uliokuwa ukifanywa na Mtendaji wa Mtaa.


1.4 Kukataliwa Barua za Maombi za Baadhi ya waombaji


Katika baadhi ya maeneo, Jukwaa lilibaini kuwa waombaji wa nafasi za uwakilishi katika mabaraza ya katiba barua zao zilikataliwa. Kuna taarifa kuwa Masheha kadhaa huko Pemba na Unguja visiwani Zanzbar walikataa kupokea barua za maombi ya wajumbe wakidai kuwa wao wana watu wao ambao watakuwa wajumbe wa mabaraza. Hii ilitokana na viongozi wa serikali za vijiji na mitaa kuanzisha utaratibu mwingine kinyume na ule uliotolewa na Tume. Utaratibu katika mwongozo wa mabaraza unawataka wagombea kuandika barua ya maombi ya kugombea nafasi zilizotangazwa na kuziwasilisha kwa mtendaji, ambaye anapaswa kupokea na kuweka majina yote ya waombaji katika sehemu za wazi na katika mbao za matangazo. Katika baadhi ya maeneo kumetokea malalamiko kuwa watendaji walitoa fomu maalumu kwaajili ya waombaji kujaza badala ya barua. Fomu hizi zilitolewa kiitikadi ya kichama na CCM inatuhumiwa kuendesha zoezi hilo la kuandaa fomu. Kwa mfano, katika kijiji cha namagondo Kata ya ya Namagondo tarafa ya mbumbuga wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza, Wananchi walilalamikia kutoona majina yao katika nafasi walizoomba na walipouliza sababu za majina yao kutokuwapo waliulizwa kama walijaza fomu maalum na kama hawakujaza basi hiyo ndio sababu majina yao hayakuwapo. Zipo taarifa pia kuwa baadhi ya Wananchi waliamua kuwasiliana na Tume ya Katiba kwa ufafanuzi wa jambo hilo na wakajibiwa kuwa hakukuwa na fomu maalum za kujaza.Vilevile, baadhi ya wananchi walikataliwa maombi yao kwa madai kuwa nafasi zimekwisha jaa wakati tume katika mwongozo wake haijaeleza kiwango au idadi ya mwisho ya wagombea.




1.5 Mkanganyiko wa Tarehe za uchaguzi wa Mabaraza


Tume ya uchaguzi katika mwongozo ilipanga muda wa uchaguzi kuwa ni kati ya tarehe 30 machi mpaka April 3 kwa wajumbe wa vijiji na mitaa. Hata hivyo tume ilitangaza muda wa nyongeza wa siku mbili nje ya Mwongozo wa tume. Taarifa hii haikuweza kuwafikia wananchi wote kwa wakati muafaka pamoja na tume kujitahidi kutangaza katika vyombo kadhaa vya habari. Pili, taarifa hii iliwakanganya wananchi na viongozi hasa katika ngazi ya kijiji na mitaa hivyo kupelekea kuvunjwa kwa mwongozo. Kwa mfano, katika kijiji cha Ikula kata ya Ruaha Mbuyuni wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ngazi ya kijiji ulifanyaka tarehe 16 Machi 2013 badala ya tarehe 30 Machi hadi 5 Aprili 2013. Vilevile, uchaguzi wa wajumbe ngazi ya kata katika Kata hiyo ulifanyika tarehe 4 Aprili 2013 badala ya tarehe 5-9 Aprili kinyume na utaratibu uliowekwa na tume katika mwongozo wa Mabaraza ya Katiba na hivyo kuwanyima fursa baadhi ya wagombea na hata wajumbe wa Kamati za Maendeleo za Kata. JUKWAA LA KATIBA tunaona kuwa Tume ilichangia sana kuwachanganya wananchi na watendaji kutokana na kuongeza tarehe za uchaguzi katika vijiji na mitaa katika dakika za mwisho na pia kutokana na mianya iliyomo katika Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba. Inasikitisha kuwa hata wagombea waliokuwa wakihangaika kutimiza wajibu wao wa kukata rufaa waliishia kubabaishwa na kupelekwa huku na huko pasipo majibu ya kuridhisha.


1.6 Uandikishaji bandia na wa kipotoshaji wa Wapiga Kura


Kasoro nyingine iliyojitokeza ni uandikishaji wa wapiga kura. Katika maeneo mengi ambako zoezi la uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza lilifanyika, viongozi wa serikali za vijiji na mitaa waliamriwa kuandikisha majina ya wapiga kura masaa machache kabla ya upigaji kura wenyewe. Kitendo hiki ni kinyume na mwongozo wa uundwaji wa mabaraza haya kama ulivyotolewa na Tume. Ifahamike kuwa wanaoruhusiwa kupiga kura ni wajumbe wote wa mkutano mkuu wa kijiji au wajumbe wa mkutano mkuu wa mtaa ambao kimsingi ni wanakijiji au wakazi wote wa mtaa wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea. Uandikishwaji huu ulikuwa ni upotoshaji wa hali ya juu na uliwanyima wananchi wengi haki ya kupiga kura kwani ulifanyika siku ya uchaguzi na kulikuwa na muda mchache sana wa kuandikisha hivyo wale waliochelewa walinyimwa haki yao. Kwa mfano, katika Manispaa ya Kinondoni Jijini Dare es Salaam muda uliopangwa kuandikisha ni kuanzia saa 2 mpaka saa 4 asubuhi. Wananchi waliofika baada ya muda huo hawakuruhusiwa kupiga kura. Tume ingeweza kutumia orodha katika daftari la wakazi na likatumika katika kupiga kura pale mkazi husika anapoonyesha kitambulisho chake, pasi ya kusafiria au kitambulisho cha upigaji kura. Hili si ngeni katika michakato ya upigaji kura kwani imetumika hivi karibuni katika upigaji kura ya katiba “referendum” nchini Zimbabwe ambapo wapiga kura walitakiwa kutumia ama kitambulisho cha utaifa (ZimCard), au pasi ya kusafiria. Hii ingeepusha vurugu na malalamiko yaliyojitokeza hivyo kumpa mwananchi haki yake ya kuchagua. Kuhusu uchaguzi katika ngazi ya Kata, mambo mawili yalileta utata. Kwanza hapakuwa na uwazi juu ya wajumbe halisi wa Kamati ya Maendeleo ya Kata watakaoweza kupiga kura. Kwa mfano, ziko sehemu ambazo zilikataza wataalam kupiga kura na ziko kata ziliwaruhusu. Aidha, ziko sehemu nchini zilichagua pasipo kuwasikiliza wagombea wakati ziko kata ziliwaalika na kuwasikiliza waombaji wote ndipo wawachague. Zaidi ya hayo, kulikuwa na utata uliotokana na wenyeviti wa Mitaa na vijiji walioingiza majina yao katika orodha ya waombaji huku wakihusika katika kupitisha majina hayo katika ngazi ya Kata kama wajumbe wa Kamati ya aendeleo ya Kata (WDC). Yote haya hayana majibu hadi leo!




1.7 Ubaguzi dhidi ya Watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji Maalum


Mwongozo wa uundwaji wa mabaraza ya katiba unataja makundi mbalimbali ya wajumbe katika Mabaraza. Wajumbe hao wanatakiwa wawakilishe makundi mbalimbali katika jamii yetu. Hivyo kuna wawakilishi wa vijana, wanawake, wazee na kundi jingine linalaotajwa kama “mtu yeyote”. Katika makundi haya hakuna kundi la wenye ulemavu na mahitaji maalum licha ya ushauri wa namna hii wa JUKWAA katika hatua za kutolea maoni Mwongozo. Hivyo kundi hili limekosa uwakilishi katika mchakato huu muhimu wa uundwaji wa katiba mpya. Tume imewabagua moja kwa moja kwa kutowashirikisha katika hatua hii. Haijafahamika kwamba hili limetokea kwa bahati mbaya au makusudi hasa ikizingatiwa kuwa kasoro hii iliibuliwa na JUKWAA LA KATIBA wakati wa kutoa maoni ya rasimu ya Mwongozo wenyewe. Kwa mujibu wa taarifa za waangalizi wetu mikoa yote Tanzania imelalamikia jambo hili. Watu wengi wamekuwa na pendekezo kuwa nafasi ya 4 ya wajumbe katika ngazi ya kijiji na Mtaa Mikoani na ile ya 7 na 8 kwa jiji la Dar es Salaam ingepaswa kuwa ni nafasi ya uwakilishi wa kundi hili la walemavu na watu wenye mahitaji maalum. Katika uwakilishi kwa misingi ya usawa wa kijinsia uwakilishi wa wanawake pia umekuwa finyu sana kwani ni wanawake wachache sana wamechaguliwa. Wanawake wamechaguliwa kutoka nafasi ya mshiriki mwanamke tu katika vijiji na mitaa wale waliogombea katika makundi mengine walikuwa wachache na hawakuchaguliwa. Kwa mfano, katika kata ya Soweto mtaa wa Wireless Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, kulikuwa na wagombea watatu (3) wanawake kati ya 19 na alichaguliwa 1 tu kutoka katika kundi la wanawake.




1.8 Kutokuwapo kwa orodha ya majina ya Wagombea katika Mitaa na Vijiji


Katika maeneo mengi ulikofanyika uchaguzi Jukwaa la katiba limebaini kuwa hakukuwa na orodha yoyote ya majina ya wagombea iliyobandikwa katika mbao za matangazo ili wapiga kura waweze kuwatambua na kuwapima uwezo wao. Hilo lilienda sambamba na kutotoa fursa ya wagombea kujieleza na kuulizwa maswali ili wapigakura waweze kupima uwezo wa kila mgombea. Hii iliwapa ugumu wapiga kura kuwakumbuka wagombea wakati wa upigaji kura. Pili, jambo hili lilipelekea wagombea kuwa na wapiga kura wao kama ilivyoelezwa awali hivyo kuongeza mpasuko mkubwa kwa misingi ya kiitikadi ya vyama na dini ya mgombea. Katika mikoa mingi kasoro hii ilijitokeza na mifano ni kama Sengerema, Dodoma na Tunduma ambako kulitokea ubishani mkubwa juu ya endapo kulihitajika wagombea wajieleze au la. Hata katika maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam ambako wagombea walipewa fursa ya angalau kuwasalimia wapiga kura, fursa hiyo ilikuwa finyu sana kiasi kwamba wagombea wengi walilalamikia kutoweza kupata fursa ya kutosha kuonyesha uwezo wao wa kupembua , kupambanua na kufafanua mambo kitu ambacho ndicho kigezo kilichowekwa katika Mwongozo wa Tume ya Katiba.


1.9 Upungufu na mapungufu ya vifaa vya uchaguzi


Kumekuwapo na malalamiko pia juu ya upungufu na mapungufu ya vifaa vinavyotakiwa katika upigaji kura. Katika maeneo mengi vifaa kama masanduku ya kupigia kura, peni na karatasi havikuwepo kabisa. Kikubwa zaidi mapungufu yaliyokuwa katika vifaa vyenyewe hususani karatasi ndilo lililoathiri zaidi zoezi zima la upigaji kura. Karatasi za kupigia kura katika maeneo mengi kwa mujibu wa waangalizi wetu hazikuwa na alama yeyote kuonyesha uhalali wake wa kutumika ili zisiweze kughushiwa au kutumika nje ya utaratibu na malengo yaliyokusudiwa. Hii inatokana na Tume ya katiba kutotoa mwongozo wowote juu ya uhalisi na uhalali wa karatasi zinazotakiwa kutumika. JUKWAA LA KATIBA tunadhani kuwa kungeweza kutolewa maelekezo kuwa karatasi za kura ziwe na muhuri wa serikali au ya kijiji au mtaa au halmashauri. Ingewezekana pia kutumia rangi mfano nyekundu au kijani n.k kamarangi maalum. Jambo hili limepelekea malalamiko kutoka katika maeneo mengi kuwa viongozi wa serikali za vijiji na mitaa wamejiongezea kura kuweza kupata ushindi. Katika wilaya ya Kilolo kijiji cha Uhambingeto mwenyekiti amelalamikiwa kwa kujiongezea kura huku wananchi wengine wakikamatwa na kura walizokuwa wanataka kupiga kabla ya uchaguzi. Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Manispaa ya Moshi, kata ya Majengo kwa mtei mtaa wa Mji Mpya kumekuwa na madai kuwa watu walipiga kura mara mbili mbili au tatu kwani hakukuwa na udhibiti wa karatasi za kupigia kura. Utaratibu uliotumika kugawa karatasi za kura haukuwa mzuri. Karatasi ziligawiwa hovyo na wakati mwingine mtu mmoja alichukua karatasi zaidi ya tatu na hivyo kumpigia mtu mmoja kura zaidi ya tatu. “Mtu anachukua karatasi anazunguka kidogo anachukua nyingine anaenda chini ya mti anapiga kura zaidi ya mbili”, tuliambiwa!




1.10 Muda wa mchakato, tarehe za Uchaguzi na mwitikio duni


Jukwaa la katiba limebaini kuwa muda uliowekwa wa siku za mchakato mzima wa uchaguzi kuwa ni mchache kuweza kuufanya uchaguzi huo kuwa huru na haki. Kwa mujibu wa mwongozo wa mabaraza, mchakato mzima kuanzia maombi mpaka uchaguzi ulipewa mwezi mmoja tu. Muda huu ni kidogo sana kulinganisha na umuhimu wa jambo lenyewe ndio maana hata tume ililiona hilo na kuamua kuongeza muda nje ya ule uliowekwa katika mwongozo ingawa taarifa za kuongezwa kwa muda huo hazikufika katika maeneo mengi kwa wakati na zilikofika kwa wakati zilisababisha mikanganyiko na hatimaye malalamiko. Vilevile tarehe ya uchaguzi ilikuwa siku ya kazi jambo lililosababisha watu wengi hasa mijini kushindwa kushiriki katika uchaguzi. Mitaa mingi ya jiji la Dar es Salaam wapiga kura walijitokeza kwa uchache sana. Kwa mfano, katika kata ya kipawa yenye wakazi wapatao 60,000 ni wakazi 1,181 tu ndio waliojitokeza kupiga kura huku kukiwa na jumla ya wagombea 148, wanawake wakiwa wachache sana. Hii inatoa taswira ya kwamba wawakilishi hao waliochaguliwa wanawakilisha kundi dogo sana la wananchi wa eneo hilo. Aidha, huko Dodoma katika mtaa wa Mlimwa wenye wakazi zaidi ya 1000 ni wapiga kura 40 tu ndio waliojitokeza kupiga kura.


1.11 Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kutumbukiza majina yao


Wenyeviti wa Mitaa na vijiji wengi waliingiza majina yao katika orodha ya


wagombea. Hii imefanya wasiwe wasimamizi zaidi bali wagombea. Hatari yake


ni kwamba kuna watu wamekuwa na hisia kuwa kulikuwa na upendeleo katika


kupitisha majina ya wenyeviti. Aidha kuna watu wanahisi hata kuzuia


wagombea kujieleza ilikuwa ni woga wa wenyeviti kuulizwa maswali. Pia,


wenyeviti kugombea inaleta mgongano wa kimaslahi ikizingatiwa kuwa


wenyeviti ni wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambayo ndio inakaa


kujadili na kupitisha wagombea waliotoka katika ngazi ya Mitaa na Vijiji.






1.12 Kura kutokuwa ya Siri na kupigwa kiholela


Kura kutokuwa ya Siri ni Kinyume cha Mwongozo wa Tume. Katika maeneo


mengi kura iliyopigwa ilikuwa ya wazi na sio ya siri kama ilivyotamkwa


katika Mwongozo wa mabaraza ya Katiba kama ulivyotolewa na Tume ya


Mabadiliko ya Katiba. Katika maeneo mengi ikiwemo Usangi na Ugweno mkoani


Kilimanjaro na Sumbawanga mkoani Rukwa, kura hazikupigwa kwa siri na


hili limeleta malalamiko kuwa baadhi ya watu walipiga kura kwa kuwaonea


aibu au kuwaogopa baadhi ya wagombea hasa viongozi.




1.13 Dosari katika Uchaguzi wa Wajumbe ngazi ya Kata


Katika ngazi ya mchujo wa wagombea ngazi ya Kata kulikuwa na matatizo


mawili. Kwanza, kulikuwa na taarifa kutoka maeneo mbalimbali kuwa wataalam


walizuiwa kuwa sehemu ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC). Katika maeneo


mengine, wataalam nao walikuwa sehemu ya upigaji kura kuchagua wajumbe wa


mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Mkanganyiko huu umefanya nchi moja itumie


mifumo tofauti katika kupata wajumbe kupitia Kamati za Maendeleo ya Kata


(WDC). Aidha, tatizo la Pili katika ngazi ya mchujo katani lilikuwa ni


utata wa ama kuwaita waombaji wote waje wajieleze na kuonwa na wapiga kura


au kuwachagua bila wao kuwepo (in absentia). Utata huu nao umeathiri zoezi


la uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza katika mikoa katibu yote ya Tanzania.




1.14 Tume Kushindwa kutoa mwongozo kwa maeneo yaliyoshindwa kufanya uchaguzi katika tarehe zilizotangazwa


Tume ya katiba imeshindwa kutoa mwongozo kwa wakurugenzi wa wilaya na manispaa juu ya nini kifanyike na hatua gani zichukuliwe pale uchaguzi unaposhindwa kufanyika. Kwa mfano, kama uchaguzi umeshindwa kufanyika katika tarehe zilizopangwa kutokana na matatizo au mapungufu yanayoweza kutokea, je ni hatua gani inapaswa kuchukuliwa?. Je uchaguzi unaweza ukafanyika tena na ni utaratibu gani na hatua zipi za kufuata ili wananchi waweze kufanya uchaguzi na kupata haki yao ya uwakilishi katika mabaraza ya katiba. Kwa hali ilivyo sasa maeneo ambayo wameshindwa kufanya uchaguzi au yale ambayo uchaguzi umefanywa kwa mizengwe na kasoro lukuki hatma yake haijulikani. Ni vema utaratibu huo ukawekwa ili kunusuru wananchi kukosa haki yao na kuepusha jambo hilo kujirudia katika hatua zinazofuata katika mchakato huu hususani uchaguzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba utakaokuja baadaye mwaka huu. Aidha ni vema kuweka bayana utaratibu utakaofuatwa na wagombea kukata rufaa wasiporidhishwa.


1.15 Tume ya Katiba na uhamasishaji hafifu


Sote tumeshuhudia jitihada za Tume ya katiba katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika hatua mbalimbali za mchakato wa katiba. Aidha tumeona vyombo vya habari vikihamasisha umma katika kushiriki mchakato na tunawapongeza kwa jitihada hizo. Pamoja na pongezi hizi, Jukwaa la katiba limebaini kuwa jitihada hizo bado ni hafifu. Tume inatakiwa kuongeza kasi ya uhamasishaji kwani mwitikio hafifu wa wananchi katika mchakato wa uundwaji wa mabaraza ya Katiba unaonyesha ni jinsi gani wananchi hawana uelewa na hamasa hivyo hawajui umuhimu wa mabaraza na katiba kwa taifa lao. Katika maeneo mengine hata waliojitokeza kuomba kugombea nafasi hizo hawakujitokeza siku ya uchaguzi. Huko katika manispaa ya Moshi kulikuwa na gari moja tu la matangazo siku moja kabla ya kupiga kura hata matangazo yaliyotolewa kujiandikisha kuwa mjumbe wa Baraza la katiba yalikuwa ni hafifu kwani matangazo mengi yalibandikwa kwenye mbao za matangazo za Ofisi ya Kata tu. Maeneo haya wananchi huyatembelea mara chache sana na hivyo kusababisha wananchi kutofahamu vizuri namna ya kutuma maombi. Hivyo tume inatakiwa kuongeza juhudi katika uhamasishaji huku ikihamasisha asasi mbalimbali kusaidia kazi hii ya uhamasishaji wa Wananchi.


2.0 HITIMISHO


Kutokana na kasoro nyingi zinazofikia 15 kwa uchache zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba, Jukwaa la Katiba Tanzania linapenda kutangaza rasmi kuwa uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya katiba katika maeneo mengi nchini haukuwa HURU wala wa HAKI na ni BATILI. Kwa sababu hiyo, JUKWAA LA KATIBA tunapendekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na taifa kwa ujumla mambo yafuatayo:


Mosi, dalili zilizojionyeha katika uchaguzi huu, hususani suala la itikadi za vyama na udini, rushwa, uchakachuaji na upendeleo, ubaguzi wa makundi ya watu wenye ulemavu, kukosekana kwa mwongozo timilifu wa uchaguzi huu na uhamasishaji duni kwa ujumla wake, mchakato wa kupata katiba inayokubalika na watanzania walio wengi na ambayo kwayo wangeweza kujiona kama wamiliki wa mustakabali wa taifa lao umeingia doa. Dalili kama hizi zinaweza kukwamisha hatua zijazo katika kupata katiba Mpya hivyo ni bora zikatibiwa sasa kuliko kusubili zituathiri. Tunapendekeza kuwa uchaguzi katika maeneo yote yaliyokumbwa na kasoro hizo urudiwe na Tume itangaze tarehe za Marudio!


Pili, Jukwaa linaona kwamba Tume ya katiba inawaburuza watanzania katika mchakato wa katiba kwa kuukimbiza kasi huku kukiwa na mapungufu mengi yanayoathiri kimsingi ushiriki wa wananchi katika uundwaji wa katiba yao. Jukwaa linaona kuwa kwa mwenendo huu wananchi hatimaye wanaweza kupiga kura ya hapana wakati wa kura ya maoni yaani “referendum”. Hii itakuwa ni sawa na upotevu wa fedha za watanzania kwa mabilioni, muda na nguvu za wananchi walipa kodi na inaweza kusababisha mgogoro mkubwa wa kitaifa na mdororo zaidi wa kiuchumi. TUME ya Katiba inaaswa kubadili mwenendo wake au la JUKWAA LA KATIBA tutakwenda mahakamani kusitisha mchakato wa Katiba Mpya mpaka tukubaliane namna bora ya kuepeka ratiba yake.


Tatu, Imedhihirika wazi kuwa Tume ya Katiba haina uzoefu wa kuendesha uchaguzi wa aina yoyote. JUKWAA tunapendekeza kuwa chombo chenye uzoefu katika uendeshaji wa Uchaguzi yaani Tume ya Uchaguzi ndiyo muafaka kuratibu na kusimamia mazoezi yote yanayohusisha upigaji kura katika siku za baadaye. JUKWAA LA KATIBA tunaitaka Tume ya Katiba kuacha kujihusisha na mazoezi yanayohusisha upigaji kura ili Tume ya uchaguzi ichukue nafasi yake!


Mwisho. Mapungufu na dosari zilizojitokeza Katika uchaguzi huu wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba zimeonyesha wazi haja ya kufanyia marekebisho sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuondoa kasoro zote zilizomo humo kuhusu mazoezi ya uchaguzi na mengine mengi. Itakuwa jambo la fedheha kuendelea kukaa na sheria yenye kasoro na mapungufu ya makubwa kiasi hiki!


Imetolewa na JUKWAA LA KATIBA TANZANIA

No comments: