Idadi ya watuhumiwa wa
tukio la kulipua bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya
Olasiti, mkoani Arusha Jumapili iliyopita, imeongezeka kutoka tisa hadi
12. Watuhumiwa hao wametajwa
na Jeshi la Polisi kuwa ni Victor Ambrose Kalisti (20) na Joseph Yusuph Lomayani
(18), ambao wote ni waendesha bodaboda wakazi wa Kwa Mrombo, mkoani
Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas,
akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, aliwataja watuhumiwa
wengine wanaoshikiliwa kuwa ni George Batholomeo Silayo (23), ambaye ni
mfanyabishara na mkazi wa Olasiti; Mohamed Sulemani Said (38) mkazi wa Ilala,
mkoani Dar es Salaam, ambaye polisi imemtaja kuwa ni mwenyeji wa watuhumiwa raia
wa Uarabuni na kwamba ndiye aliyewafuata kwa gari binafsi uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Dar es Salaam na kuwachukua hadi Arusha katika hoteli moja iliyoko
karibu na kituo kikuu cha mabasi yaendayo mkoani humo na nje ya
mkoa.
Wengine wanaoshikiliwa ni Said Abdallah Said
(28), ambaye ni raia wa Falme za Kiarabu, katika mji wa Abudhabi; Abdulaziz
Mubarak (30), ambaye ni mkazi wa Saudi Arabia; Jassini Mbarak (29), ambaye ni
mkazi wa Bondeni Arusha; Foud Saleem Ahmed (28), ambaye ni raia wa Falme za
Kiarabu na Said Mohsen, ambaye ni mkazi wa Najran Falme za Kiarabu.
IGP ATOA BINGO YA SH. MILIONI
50
Aidha, Jeshi la Polisi nchini kupitia Mkuu
wake, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, limetangaza donge nono la Sh. milioni
50
kwa mtu yeyote atakayefanikisha kufichua
mtandao wa kigaidi nchini.
Kamanda Sabasi alisema hayo alipokuwa akitoa
taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa tangu kutokea kwa mlipuko wa bomu hilo
Jumapili saa 4.30 asubuhi kwenye kanisa hilo.
Kamanda huyo ambaye jana alizungumzia tukio
hilo kwa mara ya kwanza, alisema siku ya tukio kulikuwa na uzinduzi wa kanisa
hilo na mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco
Padilla, na alipokuwa akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi, ghafla
mtu mmoja aliyejificha kwenye choo cha jirani, upande wa Kaskazini, alirusha
kitu kizito.
Kamanda Sabas alisema kitu hicho kilirushwa
umbali wa mita 20 na kilikuwa na ukubwa wa ngumi ya mtu mzima, kuelekea kwenye
mkusanyiko wa waumini na kilipotua chini ulitokea mlipuko mithili ya bomu na
kusababisha watu 66 kujeruhiwa, ambao kati yao watatu walipoteza
maisha.
Alisema watuhumiwa hao bado wanaendelea
kuhojiwa na tayari jalada la mashtaka dhidi yao limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), kwa ajili ya maamuzi ya kisheria.
Kamanda Sabas alisema uchunguzi wa awali
umebaini kuwa bomu hilo siyo la kienyeji na pia wageni hao walikuwa na VISA
halali ya kukaa nchini, kwa madai kuwa walikuja harusini.
“Watuhumiwa hawa wa Falme za Kiarabu
tulipowahoji, walidai wamekuja harusini, lakini tunaendelea nao,”
alisema.
Alisema watuhumiwa watatu wanaendelea kuhojiwa
na kwamba kutokana na hali hiyo, majina yao hayawezi kutajwa.
MAZISHI KUFANYIKA
LEO
Alisema ulinzi umeimarishwa katika kanisa
lilikotokea mlipuko ili kuhakikisha hakitokei kitu chochote kabla na baada ya
mazishi ya watu waliuawa na bomu hilo.
Ibada ya mazishi inatarajiwa kufanyika leo saa
2:00 asubuhi kwenye kanisa hilo na itahudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
na viongozi wa dini mbalimbali, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Arusha, Josephat Lebulu.
Pia ibada hiyo itaanza kwa maandamano kutoka
eneo la Burka kwenye makazi ya Askofu Lebulu hadi eneo la Olasiti kanisani na
itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini.
HALI ZA WALIOHAMISHIWA
MUHIMBILI
Majeruhi saba waliohamishiwa Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam baada ya kujeruhiwa na mlipuko wa bomu
hilo, wameanza kupatiwa matibabu.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es
Salaam, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Jeza Waziri, alisema hali za majeruhi,
ambao wamelazwa kwenye wodi namba 10 kwenye Jengo la Kibasila zinaendelea vizuri
na mara walipowasili walifanyiwa uchunguzi.
“Ni kweli tuliwapokea na mara walipowasili
madaktari wetu walianza kuwapatia matibabu, huku wakiangalia jinsi ya kuvitoa
vipande vya chuma vilivyopo kwenye miili yao na hali zao kwa ujumla ni nzuri,”
alisema Waziri.
Majeruhi hao ni Faustine Shirima, Gabriel
Godfrey, Abeid Njau, Jennifer Joaquim, Athanasia Reginald, Fatuma Tarimo na
Apolinari Malamsha.
habari na CYNTHIA
MWILOLEZI
chanzo:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment