Thursday, September 19, 2013
exclusive--HUYU NDIYE MAMA MUUZA UNGA MKENYA ALIYENASWA TANZANIA
MWANAMKE raia wa Kenya, Naima Mohamed Nyakiniywa ambaye pia anatumia pasiport ya kusafiria ya Tanzania ikiwa na jina la Mwanaidi Ramadhani Mfundo maarufu kama Mama Leila, ni adui mkubwa wa Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama kutokana na madai kwamba amebobea kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Obama, ambaye pia baba yake mzazi alikuwa Mkenya, mwaka 2011 alimtaja Naima katika orodha ya watu saba yeye akiwa wa 6 kuwa ni hatari kwa biashara hiyo haramu ya ‘unga’ ambapo pia aliamuru mali zake na wenzake hao zilizoko Marekani kutaifishwa, pia wasiruhusiwe kukanyaga ardhi ya taifa hilo kubwa duniani.
Septemba 16 na 17, mwaka huu, Mama Leila (na wenzake nane) alifikishwa katika Mahakama
Kuu ya Tanzania kwa mashitaka ya kukutwa na madawa ya kulevya aina ya heroin, Juni Mosi, 2011 Mbezi Beach jijini Dar.
Rekodi zinaonesha kuwa mwanamke huyo alizaliwa Septemba 2, 1962, Majengo, Nairobi, Kenya. Ingawa ni maarufu maeneo mengi ya mji huo mkuu wa nchi jirani, Pumwani, Majengo, Kariokor, Kaloleni, Biafra na Bahati, lakini katika hali ya usiri mkubwa, mwanamke huyo hafahamiki kwa majina ya Mama Leila, Naima au Nyakiniywa, isipokuwa anafahamika kama Kanyanya.
Kanyanya anayedaiwa kuwa mama wa watoto watano, katika eneo analoishi la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam anajulikana ni Mtanzania kutoka kabila la Wadigo na majirani wanasema ni mtu mwema, mwenye moyo wa kusaidia walio na shida, akiwa pia ni mfanyabiashara wa magari, saluni na ‘internet cafes’.
Nchini Kenya, inadaiwa Kanyanya alikuwa mtu mwema katika eneo la Majengo huku majirani wakisema hakukuwa na njaa katika eneo lolote ambalo Naima alikuwepo na kila mtu alipata alichokihitaji.
Kutajwa kwake na Rais Obama kunadaiwa kuwashtua wakazi wengi wa Nairobi ambako kama ilivyo Mombasa na Dar es Salaam, anamiliki mali mbalimbali, yakiwemo majumba ya kifahari.
Hata hivyo, mwaka 2009, Polisi wa Kenya walidaiwa kuwakamata vijana watatu wakiwa na madawa ya kulevya na wote walimtaja Naima kama ndiye mwenye mzigo lakini ilikuwa vigumu kwao kumuunganisha kutokana na kukosa ushahidi.
Chanzo chetu kimethibitisha kwamba wakati mmoja Naima aliwahi kukamatwa akiwa na madawa ya kulevya na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani jijini Nairobi lakini shinikizo kutoka ‘juu’ lilisababisha mwanamama huyo kuachiwa bila kufunguliwa mashitaka.
Inadaiwa kuwa hata alipokamatwa Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika na biashara hiyo, kulikuwa na idadi ya simu za kutosha kutoka ofisi ‘kubwa’ jijini Nairobi zilizotaka aachiwe lakini polisi wa Bongo ‘walikomaa’ naye ili kumfahamu zaidi.
Naima anamiliki zaidi ya hati sita za kusafiria zenye majina na sura tofauti ili kufanikisha safari zake za mara kwa mara nje ya nchi na mojawapo ni ya Tanzania ambayo haifahamiki ilipatikana kutoka ofisi gani ya uhamiaji hapa nchini.
Katika orodha ya Rais Obama ya watu hao kutakiwa kufilisiwa mali zao na kutokanyaga
Marekani, pia yupo mbunge wa zamani wa Jimbo la Kilome, John Harun Mwau kutoka chama cha siasa cha Party of Independent Candidates of Kenya (PICK).
Wengine katika orodha hiyo ni Manuel Torres Felix wa Mexico, Gonzalo Inzunza Inzunza (Mexico) Haji Lal Jan Ishaqzai (Afghanistan), Kamchybek Asanbekovich Kolbayev (Kyrgyzstan) na Javier Antonio Calle Serna wa Colombia.
SOURCE http ://www.masainyotambofu.com/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment