Monday, January 13, 2014

TLP,NA NCCR WAMGOMBEA ZITTO,MREMA ASEMA ZITTO NI JEMBE AJE KWETU



MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ambaye ana mgogoro na chama chake, sasa anaonekana kugombewa na baadhi ya vyama vya siasa nchini. Hali hiyo imekuja baada ya baadhi ya wenyeviti wa vyama hivyo, kuzungumza na MTANZANIA Jumatatu na kumtaka kwa nyakati tofauti ajiunge na vyama vyao.ENDELEA HAPO---------


          Katika mazungumzo yake, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema Zitto ana kila sababu ya kuhamia TLP ili aandaliwe kwa ajili ya kukiongoza chama hicho cha upinzani.

       Kwa mujibu wa Mrema, Zitto akihamia TLP hatakuwa amepotea njia kwani chama hicho kina uzoefu wa siasa za upinzani.
“Zitto ni kifaa, ni jembe, ni mali inayouzika, ana soko na ni mti wenye matunda ndiyo sababu unapopolewa mawe kwa maana hana haja ya kujinadi.

      “Akiamua kufanya uamuzi sahihi kwa kujiunga na TLP, hapa atakuwa amefika kwa sababu mimi nitakuwa wa mwisho kumnyanyasa Zitto.

     “Tatizo kubwa linalomponza Zitto ni pale anapoamua kunyemelea uenyekiti wa watu, hilo ndilo kosa lake.

        “Namwambia Zitto aje TLP na kama atakuja basi aje na watu wote wanaomuunga mkono huko Chadema.

         “Kuna muda fulani niliacha biashara ya jumla nikaanza ya rejareja, ambayo nayo inalipa lakini Zitto akija, tutaanza kufikiria kufanya ile ya jumla maana anaiweza,” alisema Mrema.

       Kwa upande mwingine, Mrema alisema Chadema wajifunze kutoka kwake kwani alipokuwa NCCR-Mageuzi, kuna wakati alitaka kuuawa kwa kisingizio kwamba alikuwa kibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

      “Dhambi ya usaliti ndiyo itaiua Chadema, kwa sababu baada ya kuona wanakubalika kwa wananchi, sasa wakataka kuvidhoofisha vyama vyote vya upinzani ili wabaki wao tu na sasa wanaona matokeo yake,” alisema Mrema.

         Naye, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema Zitto ana vigezo vyote vya kuwa mwanachama wa chama hicho, kwa kuwa anakubalika kwa wananchi.

        “Sura ya tatu, ibara ya tisa ya Katiba yetu inaeleza masharti ya kujiunga na chama ambayo ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania, mhusika kuwa na umri wa miaka 18 na pia awe na akili timamu.

      “Zitto ni Mtanzania na sifa zote hizo anazo, kwa hiyo, kama atatekeleza hayo basi anunue kadi ya chama chetu na tunamkaribisha NCCR.

“Lakini kuhusu kinachoendelea huko Chadema, kwa bahati mbaya siwezi kukizungumzia kwa sababu mimi siyo msemaji wao,” alisema Mbatia.

        Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema kwa kifupi kwamba kinachoendelea Chadema ni kukua kwa demokrasia.

      “Hilo siyo jambo jipya, ni jambo la kawaida katika vyama vikubwa kama Chadema, kwa hiyo watu wasishangae, waone hali hiyo kama ya kawaida kisiasa,” alisema Profesa Lipumba.

       Wakati hao wakisema hayo, Peter Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha PPT-Maendeleo, alisema Zitto anatakiwa kuondoka Chadema kwa kuwa hakubaliki tena.

      Kutokana na hali ilivyo, alisema Zitto hatakiwi kung’ang’ania demokrasia ndani ya chama hicho, kwani atawafanya watu waanze kujiuliza anataka nini katika chama hicho.

“Kwa jinsi ninavyoona, makosa yake hayasameheki, ni kama anaonekana amepindua nchi ambapo adhabu yake ni kifungo. Zitto hajapindua nchi bali anaonekana anataka kupindua chama na adhabu yake ni kufukuzwa.

“Ni vigumu, Zitto kuachwa salama kwa sababu yanayomhusu ndani ya chama chake ni mengi na yale aliyoyapeleka mahakamani na kushinda ni zuio tu siyo kesi ya msingi.

“Pamoja na hayo, taarifa nilizonazo ni kwamba, ule muhtasari wa kikao kilichomfukuza ambao aliuomba, anaweza akapatiwa ili akate rufani kwa sababu ni haki yake ya msingi ya kikatiba, lakini anaweza asishinde.

“Katika suala la kujiunga katika chama chetu, akitaka kuja suala la kumkubalia au kumkatalia ni suala la mazungumzo, kwa sababu yeye ni mwanasiasa kijana, anahitaji kujifunza.

“Pia anahitaji kubadilika na Chadema inahitaji kubadilika kwa sababu haya mambo yao yanatuchelewesha wanamageuzi. Hivi mambo kama ni haya, nchi tutaishika lini kwa mtindo huu,” alihoji Mziray.        

No comments: