PR JOHN NKOMA MKURUGENZI WA TCRA |
Mamlaka ya Mawasiliano
imepokea matokeo ya tathmini ya zoezi la uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa
analojia kwenda kidijiti. Zoezi hili lilifanyika kwenye miji saba kama
ilivyotajwa kwenye taarifa iliyotolewa na wataalamu wa Chuo kikuu cha Dar e
salaam waliofanya tathmini ya Uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya
Kwanza.
Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) ilifanya kamisheni kwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufanya tathmini
ya uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya Kwanza, ikitambua kuwa Chuo
Kikuu Cha Dar es Salaam kuna wataalamu wenye uzoefu mkubwa wa kufanya tathmini
za aina mbalimbali, na kwamba uzoefu huo utasaidia sana kuhakikisha kuwa
tunapata taarifa ya uhakika itakayotuwezesha kuboresha zoezi hili kwenye awamu
inayofuata.
Nachukua nafasi hii
kuwapongeza wataalamu waliohusika katika tathmini hii kwa weledi wao kwenye
kazi hii muhimu kwa taifa letu kulingana na matokeo yaliyowasilishwa kitaalamu
mbele yenu waandishi wa habari leo hii.
Tanzania ni nchi ya
kwanza kuzima mtambo ya analojia Barani Afrika. Uamuzi wa kufanya hivyo, na
matokeo yake, umeiletea sifa kubwa nchi yetu kwa jinsi ambavyo Tanzania ilijipanga
na kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kimataifa kwa wakati na weledi mkubwa. Hii
imeonyesha wazi jinsi Serikali ilivyoweza kushirikiana na taasissi zake pamoja
na wadau wote katika kutimiza azma hii iliyoafikiwa kimataifa tangu 2006.
Zoezi la uzimaji
mitambo kwa awamu ya kwanza iliyoanza tarehe 31 disemba 2013 halikuwa rahisi
kama wengi wetu tunavyoweza kufikiria, kwani liligusa nyanja nyingi zikiwemo za
kijamii, kibiashara, kiufundi na Kisiasa. Mamlaka kama mdhibiti wa sekta ya
Mawasiliano, ilibidi kuzingatia matakwa ya nyanja zote na wadau mbalimbali bila
kuathiri utoaji wa habari nchini. Inakadiriwa kuwa mpaka kumaliza zoezi hili,
mitambo ya kurushia matangazo kwa mfumo wa analojia isiyopungua 60 itakuwa
imezimwa. Hali hii imefanya Tanzania kuwa nchi ya pekee na kuifanya nchi yetu
kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi nyingi ambazo sasa zimekuwa zikifika kujifunza
hapa nchini.
Uamuzi wa kufanya
mkutano wa nchi za SADC na ule wa nchii za Jumuiya ya Madola kuhusu Mfumo mpya
wa utangazaji wa kidijiti kwa sekta ya utangazaji hapa nchini hivi karibuni, ni
matokeo ya mafanikio makubwa tuliyo yapata kwenye zoezi hili lililoendeshwa
kitaalamu na Serekali yetu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
UPELEKAJI WA MKONGO WA TAIFA KWENYE VITUO VYA KURUSHIA
MATANGAZO
Mamlaka
ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara na Kampuni ya Simu ya TTCL tuko
kwenye mchakato wa kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kurushia matangazo
vinafikiwa na mkongo wa Taifa (Optic fiber cable).
Madhumuni
ya jitihada hizi, ni kuona kuwa mbali na huduma ya msingi ya kurusha matangazo
ya televisheni, vituo vya utangazaji vinatoa huduma za ziada zipatikanazo
kwenye mfumo wa kidijiti. Kwa lugha ya kitaalam ni “interactive services”. Napenda
kuchukua nafasi hii kuvitaka vituo vya utangazaji vyote nchini kuwa wabunifu na
kutumia fursa zilizopo kwenye teknolojia hii ya kidijiti ili wananchi waweze
kuona tofauti kubwa kati ya mfumo wa zamani wa analojia na huu mpya wa
kidijiti.
UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA AWAMU YA PILI
Baada ya kupokea
matokeo ya tathmini Awamu ya Kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano inajipanga kuzima
mitambo kwa awamu ya pili na ya mwisho. Katika awamu hii, inategemewa miji 12
itahusika na uzimaji wa mitambo ya analoja. Lakini kama maafikiano yalivyofanyika
awali, uzimaji utafanyika tu pale ambapo huduma za utangazaji wa kidijiti
umefika. Vigezo vyote vitano
tulivyokubaliana na wadau vitahakikishwa kuwa vinatimizwa kabla ya kuzima
mitambo hiyo.
Ni matarajio ya Mamlaka
kuwa wasimikaji wa mitambo ya kidijiti (Multiplex Operators) wataendelea kwa
kasi ufungaji wa mitambo hiyo hasa kwenye maeneo ambayo mfumo wa analojia
unatumika. Mpaka sasa miji mingine 7 inapata huduma ya matangazo ya kidijiti
nayo ni Morogoro, Singida, Tabora, Musoma, Kigoma, Bukoba na Kahama. Mchakato
wa kufunga mitambo ya kidijiti kwenye miji iliyobaki inaendelea vizuri. Tunatarajia
kuwa vituo vya utangazaji vitatoa ushirikiano mkubwa kama ule tulioupata kwenye
awamu ya kwanza.
Mamlaka imeyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa
kwenye ripoti hii na tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale yaliyo nje ya uwezo
wetu tutayafikisha mahali panapohusika kwa utekelezaji zaidi.
Mwisho, napenda
kuwafahamisha kuwa Mamlaka imependekeza rasimu ya ratiba ya uzimaji mitambo
awamu ya pili na ya mwisho itakayotangazwa na Waziri mwenye dhamana ya sekta ya
Mawasiliano hivi karibuni.
Katika mapendekezo ya
Mamlaka, tunakusudia kuanza awamu ya pili katika miji ya Singida na Tabora
mnamo mwishoni wa mwezi Machi 2014. Miji mingine katika awamu ya pili itakuwa
Musoma, Bukoba, Morogoro, Kahama, Iringa, Songea na Lindi. Awamu ya pili
inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014.
Nia ya Mamlaka ni kuona
zoezi hili la uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa
kidijiti linakamilka katika nchi yetu kabla ya kufikia ukomo wa matangazo ya
analojia kama ilivyoelekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia
Mawasiliano Duniani (ITU) siku ya tarehe 17 Juni 2015.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO
TANZANIA
19 February 2014
No comments:
Post a Comment