Monday, February 10, 2014

UDAKU HUO SOMA------ROSE MUHANDO MBARONI KWA UTAPELI

Rose Muhando.
  STAA wa nyimbo za Injili Bongo, Rose Muhando yamemkuta ya kumkuta ambapo Ijumaa iliyopita alishikiliwa na Polisi wa Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam kwa madai ya kuingia mitini na shilingi milioni 6 alizolipwa kwa ajili ya kwenda kufanya shoo ya kiroho, Mombasa, Kenya Novemba 3, 2013 lakini hakutokea. Kwa mujibu wa chanzo chetu, Rose alidakwa jijini Dar es Salaam saa sita mchana huku mlalamikaji wake akiwa ni mtu aliyejulikana kwa jina la Nathan Wami.
Nathan amewahi kuwa meneja wa kazi za Rose Muhando. Kwa sasa Rose anaratibiwa na Kampuni ya Sony.



                            MADAI YA JALADA LA KESI

ENDELEA HAPA-----------

Kwa mujibu wa chanzo, jalada la kesi hiyo lilifunguliwa Dodoma likisomeka; DOM/RB/1129/2014 KUJIPATIA MALI KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa Rose aliachiwa kwa dhamana akitakiwa kurudi kituoni hapo Februari 8, 2014 huku mkononi akiwa ameshika kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumlipa mlalamikaji huyo.

WIKIENDA LATINGA POLISI MSIMBAZI
Baada ya kuinyaka nyeti hiyo, Ijumaa Wikienda lilipiga hodi kituoni hapo na kuulizia kama ni kweli nyota huyo wa wimbo wa Utamu wa Yesu alishikiliwa.
“Sisi si wasemaji wakuu wa polisi, hatuna mamlaka hayo. Hatuwezi kusema ni kweli au si kweli,” afande mmoja alilijibu gazeti hili.

MADAI NYUMA YA PAZIA
Wakati madai ya Rose yakiwa hayo, nyuma ya pazia kuna mlolongo wa matukio ya kushangaza kati ya mwimbaji huyo na Nathan.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja, Rose amekuwa akiingia kwenye madai ya kupokea fedha za shoo na kutokwenda lakini Nathan akielekezewa lawama zote.

PESA APOKEE MENEJA, LAWAMA ABEBESHWE ROSE
“Jamani mimi nataka kuwaambia ukweli, Rose hahusiki na hiyo tabia. Wengi wanasema ana mchezo wa kuchukua fedha za watu halafu haendi kwenye tukio lakini ukweli si huo,” kilisema chanzo hicho.
Wikienda: “Ukweli ni upi? Funguka basi.”
Chanzo: “Ukweli ni kwamba, Nathan amekuwa akimnyanyasa sana Rose kwa muda wote aliokuwa meneja wake.
“Ilifika mahali, Nathan ndiye alikuwa akipokea pesa kutoka kwa watu wanaomhitaji Rose bila kuwasiliana na mwenyewe. Wakati mwingine Rose hajulishwi mapema.
“Siku akiambiwa, pengine anaumwa au yupo mbali na eneo la tukio, sasa hapo waandaaji wanamsema Rose kwamba amechukua fedha na kuingia mitini,” chanzo kilizidi kuweka wazi.

ROSE HANA CHA KUFANYA
Kwa mujibu wa chanzo, hali hiyo imekuwa ikimsumbua sana Rose kwani ni kweli wengi wanaamini hivyo lakini ukweli ni kwamba anasingiziwa tu, Rose hawezi kupokea fedha halafu asiende kuimba ila kwa sababu Nathan ni meneja wake aliyemtoa kisanii anajikuta hana la kufanya.

“Mbona kwenye matamasha ya Pasaka na Krismasi yanayoandaliwa na Msama Promotion hatujawahi kusikia Rose kaingia mitini? Ni kwa sababu Msama mwenyewe anawasiliana naye moja kwa moja,” kiliendelea chanzo.

NATHAN ALIISHI NA ROSE KWA UBABE
Ikazidi kudaiwa na chanzo chetu kwamba katika kipindi chote, Nathan amekuwa akiishi na Rose kwa ubabe wa hali ya juu, jambo ambalo lilimuathiri Rose kisaikolojia bila kujijua.
“Kuna mengi sana, tena yale ya ndani zaidi, sipendi kuyasema lakini Nathan mwenyewe anayajua, siku ikifika nitayalipua kama atapinga,” kilisema chanzo.

ROSE MUHANDO HUYU HAPA
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Rose kwa lengo la kutaka kumsikia atakachokisema juu ya madai yote hayo kuhusu yeye na Nathan, lakini zaidi ya yote tukio la kuwekwa mahabusu ya Msimbazi Polisi, msikie:
“Kusema ule ukweli mimi namwachia Mungu, yeye anajua ukweli uko wapi na uongo uko wapi!”

NATHAN SASA
Baada ya hapo, gazeti hili lilimtafuta Nathan Wami na kumsomea mashitaka yote.
Nathan: “Hayo madai si ya kweli. Kama kasema yeye siyo kweli. Nimeishi na Rose karibu miaka kumi na mbili, nilikuwa namchukulia kama mtoto wangu.
“Nimekuwa nikiona kwenye magazeti kwamba eti alisaidiwa na mfuko wa kanisa wakati mimi ndiye niliyemtoa.”

Wikienda: “Kwa hiyo madai kwamba umekuwa ukiishi naye kibabe, hukuwa unamtendea haki si ya kweli?”
Nathan: “Si ya kweli hata kidogo.”

MSAMA ANAMLIPA NANI?
Gazeti hili liliwasiliana na muandaaji wa matamasha ya Pasaka na Krismasi, Alex Msama kuhusu malipo ya Rose Muhando.
Msama: “Mimi huwa namalizana na Rose.”
Wikienda: “Kuna mwaka umewahi kumlipa pesa halafu hakutokea kwenye tamasha lako?”
Msama: “Hapana, hata Tamasha la Pasaka mwaka huu atakuwepo panapo uzima maana tumeshamalizana.”

KUTOKA KAMPUNI YA SONY
Habari zilizopatikana kutoka Kampuni ya Sony ambayo inamratibu Rose kwa sasa, zinasema kuwa wakati wa kuingia makubaliano na nyota huyo walikutana na masuala hayo ya madeni lakini walipofanya uchunguzi wakagundua mambo ambayo hawakutaka kuyaweka wazi lakini kimsingi walimhurumia Rose.

“Ila mabosi wa Sony waliamua kuwa yale madeni yaliyopita watayalipa wao, yale ambayo tarehe za Rose kuimba bado, wamemwambia akaimbe ili kumalizana na wahusika,” kilisema chanzo hicho na kuomba kutotajwa jina gazetini.
-GPL

No comments: