Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) akijibu maswali ya waandishi wa magazeti ya Mwananchi Communications Limited nje ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma. |
Kwa ufupi
Jaji Werema alisema Sheria namba 8
ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa
maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia
kundi la wajumbe 201.
Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kisheria
wa kuwafukuza au kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Werema alisema Sheria namba 8
ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ipo kimya kuhusu suala hilo na kwamba kwa
maana hiyo Rais hana mamlaka ya kutengua hata ubunge wa wale aliowateua kupitia
kundi la wajumbe 201.
“Umesoma Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba? Kaisome maana ili mtu afukuzwe ubunge lazima apungukiwe sifa za nafasi
hiyo, lakini kama sheria iko kimya maana yake ni kwamba hana (Rais) uwezo wa
kuwafukuza,” alisema Jaji Werema.
Jaji Werema alikuwa akijibu maswali
ya gazeti hili kuhusu hatima ya wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) ambao Jumatano jioni waliondoka bungeni kwa madai ya
kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge Maalumu.
Wajumbe waliotoka nje ni wanaotokana
na vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi, NRA, NLD na baadhi kutoka kundi la
201. Alhamisi asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema
utafiti uliofanywa na ofisi yake ulibaini kuwa katika kundi la 201, ni wajumbe
25 tu ambao walitoka nje pamoja na Ukawa.
Baada ya wajumbe hao kutoka nje,
Mjumbe wa Bunge hilo, Mwigulu Nchemba ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara,
aliomba mwongozo akihoji iwapo Ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu haiwezi
kumwandikia Rais Kikwete ili ateungue uteuzi wa wajumbe katika kundi la 201
ambao waliungana na Ukawa kususia vikao.
“Ningependa Rais atengue hadhi zao
ili kuingiza watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi hata bure, sisi
tunalipwa fedha nyingi, lakini tunaleta mzaha, watu hawana maji, dawa,
madawati, ada za elimu ya juu watu wamekosa, hizi fedha zingetumika huko,”
alisema Nchemba mwenye wadhifa mwingine wa Naibu Waziri wa Fedha.
Matakwa ya Sheria
Jaji Werema alisema: “Ili mtu aondolewe
katika nafasi yake ni lazima akose sifa za kuwa mjumbe, mathalan kuugua ugonjwa
wa akili au kichaa, kuumwa muda mrefu kiasi cha kushindwa kutimiza majukumu
yake na kadhalika, lakini sifa hizo kama hazipo kwenye sheria sasa unaanzia
wapi?”
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya
2011 pamoja na marekebisho yake ya 2012 na 2013 inawataja Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa nafasi zao.
Kadhalika sheria hiyo inampa Rais
mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali, lakini
haitaji sifa wanazopaswa kuwa nazo wajumbe hao.
Jaji Werema alisema hata kama sheria
ingekuwa inaruhusu kufukuzwa au kusitishwa kwa ujumbe wa wabunge hao, hakuna
sababu ya msingi ya kuwachukulia hatua hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment