Tuesday, April 1, 2014

TAARIFA MUHIMU KUTOKA TFF

Kikosi cha watu 27 wakiwemo wachezaji na benchi la ufundi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) kinatarajia kuondoka keshokutwa (Aprili 3 mwaka huu) kwenda Nairobi, Kenya.
 
Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko ipo kambini tangu Machi 23 mwaka huu kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya (U20). Mechi hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo itachezwa Jumapili (Aprili 6 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Machakos ulioko kilometa 80 kutoka jijini Nairobi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo (Aprili 1 mwaka huu), Kocha Simkoko amesema wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, na nia ni kupata matokeo mazuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini wiki tatu baadaye.

Kikosi cha Ngorongoro Heroes chenye wachezaji 20 na viongozi saba kitaondoka saa 4.30 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways. Msafara wa timu hiyo utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi Abdoulkarim Twagiramukiza, Ambroise Hakizimana, Raymond Bwiliza na Louis Hakizimana wote kutoka Rwanda wakati Kamishna ni Maxwell Mtonga wa Malawi.

Ngorongoro Heroes itaagwa kesho (Aprili 2 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.

No comments: