VIJANA WAZALENDO WA
VYUO VYA ELIMU YA JUU DAR ES SALAAM
TAMKO LA KULAANI VURUGU ZINAZOJITOKEZA KATIKA
BUNGE MAALUM LA KATIBA.
Sisi wanafunzi wasomi katika vyuo vikuu mbalimbali vilivyoko
Dar es Salaam (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU);
Dar es Salaam University College of Education (DUCE); USTAWI WA JAMII; Chuo
Kikuu cha Mtakatifu John (St. John); Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM); Open
University of Tanzania (OUT); Kampala International University (KIU); Dar es
Salaam Institute of Technology (DIT); Institute of Adult Education (IAE);
Tanzania School of Journalism (TSJ); College of Business Education (CBE) na
Chuo cha kumbukumbu ya Mwl JK Nyerere.
Sisi sote tunalaani mwenendo
uliyojengeka kwa wanasiasa wanaojiita “UKAWA“ kuvuruga Bunge Maalum la Katiba
kwa sababu ambazo si za msingi.
Kwanza walianza kudhalilisha wanazuoni wanaoonekana
kutofautiana nao kimawazo kuhusu msimamo wao wa kutaka serikali tatu. Wanazuoni
ambao wamekuwa wakidhalilishwa na kutungiwa uongo ni pamoja na Profesa Issa
Shivji, Profesa Teddy Malyamkono, Profesa Nehemia Osoro, Dk. Francis Michael,
na Dk. Kitila Mkumbo.
Tungependa kuwataarifu kuwa wanataaluma wana uhuru wa kutoa
mawazo yaani academic freedom na kamwe hawawezi kukaa kimya wanapoona kuna
jambo linaloweza kuifanya nchi ikaangamia na kusambaratika. Wanazuoni huamini
katika “no research, no data, no right to speak” kwani data zao za kiuchumi,
kihistoria, kisiasa na kidiplomasia zinakataa muundo wa serikali tatu. Hoja ya
kimsingi ni kuwa “UKAWA” imeanza juzi, je tafiti (research) wamezifanya lini za
kuzipa nguvu hoja zao za kutaka serikali 3?
Tatizo lingine tunaloliona kwa “UKAWA” ni kujaribu kuwadhalilisha
waasisi wa taifa letu hasa Mwl JK Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume. Je
tusipomuamini Mwl Nyerere na Sheikh Karume tumuamini nani kati ya hawa ambao
hatuna ushahidi wa uzalendo wao? kwani wapo wanasiasa ya aina yao ambao
wametumika na mataifa ya kibeberu kuvuruga nchi zao na mpaka leo wananchi wao
wanataabika mfano hai ni Misri, Tunisia, Morocco, Sudan Kusini, Somalia, Libya,
Mali Na Afrika ya Kati.
Heshima walionayo waasisi wetu Mwl Nyerere na Sheikh Karume
ndani na nje ya Tanzania, sio ya kupuuzwa wala kufananishwa hata kidogo na
yeyote yule miongoni mwa waliounda “UKAWA” zaidi ya kutumika kama mfano na
kielelezo.
Tunawashangaa baadhi ya wanasiasa wa “UKAWA” kuwakejeli
waasisi wa taifa letu. Wanasiasa hawa ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahim Haruna
Lipumba, Mh. Tundu Lissu na Halima Mdee kwani wamesoma katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam kilichoasisiwa na waasisi wakuu wa taifa letu, Mwl JK Nyerere na
Sheikh Karume.
Hata
wale wanasiasa wengine ambao hawakupata bahati ya kusoma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam wamesoma kwenye shule za awali na vyuo vya elimu ya juu ambavyo vina
msingi wa utawala bora wa waasisi hawa wakuu wa taifa letu. Hivyo tunaona sio
busara hata kidogo kukejeli mchango wao katika harakati za kuliendeleza taifa
letu. Tunapenda kuwathibitishia watanzaia kuwa mawazo ya waasisi wa taifa letu
hajachakaa na wala hayapitwa na wakati hata mara moja.
Sisi kwa mtazamo wetu kama vijana wasomi wazalendo wa vyuo
vya elimu ya juu tunashauri yafuatayo;
• Katiba bora haiwezi kupatikana kwa kususia vikao halali vya
bunge maalum la katiba na maandamano, hivyo tunawasihi warejee bungeni ili
waendelee na mchakato kutengeneza katiba. Hatua hii ya kurejea bungeni
ikishindikana, warejeshe posho za vikao ambavyo hawajahudhuria.
• Kutofautiana kimawazo kwa njia ya kujenga hoja ndio
demokrasia pevu yenye dhana ya “wachache wasikilizwe na wengi wapewe” ambayo ni
moja ya misingi mikuu ya demokrasia itakayotupatia “Katiba Bora” ya sasa na
vizazi vijavyo.
• Lazima wafahamu kuwa maridhiano ndio njia pekee ya kupata
“Katiba Bora” yenye kuleta “Elimu Bora”; “Kilimo Bora”; “Afya Bora”; “Uchumi
Bora” na “Utawala Bora” kwa maisha bora ya mtanzania na pia kuifanya Tanzania
kuendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu ili kupigiwa mfano na kuwa kimbilio
la waafrika wenzetu wengi wanaotaabika kwa kuzikimbia nchi zao kwa machafuko
yanachochewa na mabeberu wa siasa na uchumi duniani.
• Tunawasihi wenzetu wazingatie umuhimu wa kulinda, kudumisha,
kustawisha na kuiendeleza amani katika kipindi cha kutengeneza katiba na baada
ya mchakato. Tusipojiangalia tutakuwa kama wenzetu Misri, Tunisia, Morocco,
Sudan Kusini, Somalia, Libya, Mali na Afrika ya Kati. Tunaamini kwa kuangalia
hali za kisiasa za nchi nyingi za Afrika tunaamini kuwa siasa ya Tanzania ni
safi na hakuna haja ya kuhamasisha chuki, uzandiki, uzushi, uongo maandamano na
uasi ambao ni sumu kali ya umoja (muungano), amani na uhai wa taifa letu tukufu
la Tanzania.
• Watanzania na wanasiasa wafahamu kwamba mataifa kama
Marekani na Uingereza yametawala dunia kwa sababu ya umoja wao. Tunaomba
tujifunze kwa yaliyotokea Urusi, leo hii imeona umuhimu wa kuzirudisha nchi
ambazo zilisambaratika kutoka kwenye serikali ya umoja wa nchi za kijamaa za
kisovieti (USSR). Sisi vijana wa kizazi kipya tunawashauri wenzetu waulinde
muungano kwa gharama yeyote na muungano huwa haupitwi na wakati. Tunajiuliza
kwa wenzetu wa Ulaya na Marekani ambayo miungano yao imedumu kwa karne zaidi ya
tano na sita. Je huko hakuna vijana wa vizazi vipya? Sisi tunaona kuwa wanaodai
Utanganyika na Uzanzibari ni wakabila na wabaguzi wanaotaka kuturudisha enzi za
ukoloni.
• Tunamuomba Mwenyekiti wa Bunge Maalum azingatie kwamba
Bunge Maalum la Katiba si la “UKAWA” ni la watanzania. Hivyo basi liendelee kwa
kasi na ufanisi zaidi na lisiyumbishwe na hasira za wachache wanaojiita “UKAWA”
kutokana na ukweli kwamba gharama, muda na nguvu kubwa vimetumika mpaka sasa.
Tunaomba bunge liendelee ili kuwapatia watanzania katiba iliyo bora.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Imetolewa na Gulatone Masiga, Mwanafunzi
UDSM
Kwa niaba vijana wazalendo wa Vyuo vya elimu ya
juu Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment