Friday, April 11, 2014

UCHAGUZI WA CHALINZE--HII NDIO SABABU YA WATU KUTOJITOKEZA KWA WINGI KUPIGA KURA



     
picha na maktaba yetu
CHANGAMOTO zinazowakabili wananchi kutopatiwa ufumbuzi ama kupewa kipaumbele na viongozi wa kisiasa zimeelezwa kuwa chanzo cha wananchi kususia uchaguzi na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
          
           Hayo yameelezwa jana katika tathmini ya mwenendo wa uchaguzi mdogo wa ubunge Chalinze uliomalizika hivi karibuni, tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Mtandao wa Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRiNGON).
          
         Akisoma taarifa ya tathmini hiyo mbele ya waandishi wa habari, Mratibu wa Taifa wa SAHRiNGON, Martina Kabisama, alisema katika uchaguzi huo uliofanyika msimu wa kilimo, wananchi walionekana wakitumia muda wao kwenda mashambani kuliko kupiga kura.

         
           “Tume wakati ikitoa matangazo ya kuhamasisha watu kwenda kupiga kura wananchi walionekana wakibeza waziwazi huku wengine wakisema mnaacha kututangazia habari za maji, mnatutangazia habari za uchaguzi,” alisema.
          
         Mapungufu mengine yaliyoonekana kwenye uchaguzi huo, kwa mujibu wa Kabisama ni  wasimamizi kutumia meza iliyokuwa na sanduku la kupigia kura kutokana na ufinyu wa nafasi.
        
            Kuwepo kwa kituo cha uchaguzi katika makazi ya watu, chini ya mti na jengo la polisi kumechangia pia wananchi kutokwenda kupiga kura  kutokana na uelewa mdogo wa kazi na majukumu ya polisi.
        
            Hata hivyo alisema kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma wakati wa kampeni, ambapo viongozi wakubwa wanapohudhuria kampeni hizo inabidi waambatane  na wakuu wa wilaya (DC) na mkoa (RC) ambao nao huambatana na wasaidizi wao ambao ni watumishi wa serikali.
      
          Kutokana na upungufu huo, asasi hizo zimetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusimamia sheria na kanuni za uchaguzi ili kutoruhusu vituo vya kupiga kura kuwepo katika vituo vya polisi, makazi ya watu  au chini ya mti ili kuepuka ushawishi siku za uchaguzi.
   
            Pia wametaka kuandaliwa kwa utaratibu mzuri wa usafiri na malazi kwa wasimamizi na walinzi wakati na baada ya uchaguzi.

No comments: