A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa
iliyowasilishwa leo kwenye Bunge
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda
kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunipa nguvu ya
kutekeleza majukumu yangu na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu
kuwasilisha bajeti hii.
3. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima
nitumie fursa hii kuwapongeza Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wao thabiti ambao umeendelea kudumisha
amani na mshikamano wa Taifa letu. Tunajivunia pia matunda ya Waasisi wa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao mwaka 2014 umetimiza miaka 50. Uongozi
wao umetuwezesha kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tuliyonayo
hivi sasa.
4.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Makamu wa
Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb.), kwa
kazi nzuri wanazozifanya za ujenzi wa nchi yetu. Aidha, nikushukuru wewe
binafsi Mhe. Spika, Mhe. Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa
ushirikiano mnaonipa ambao unaniwezesha kutekeleza kikamilifu majukumu niliyokabidhiwa
ya kulitumikia Taifa letu.
5.
Mheshimiwa Spika, katika maandalizi ya hotuba hii, Wizara imezingatia maudhui
yaliyotolewa katika Bunge lako Tukufu kupitia Hotuba ya Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, hotuba yangu imezingatia pia maelekezo
na malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/2015.
6.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya
uongozi yaliyotokea, natumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri
wote walioteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali.
7.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba
kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kujadili, kuchambua na kuboresha Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni matumaini yangu kuwa baada ya
kukamilika wananchi watapata fursa ya kupiga kura za maoni kama ilivyopangwa
ili Taifa letu liweze kupata Katiba Mpya iliyo bora.
8.
Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuwapongeza
wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuishauri Wizara katika maeneo mbalimbali. Wizara itaendelea
kuzingatia na kutekeleza ushauri unaotolewa. Shukrani na pongezi zangu ziende
kwa viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza Kamati hii yaani, Mwenyekiti wa
Kamati, Mhe. Saidi Mtanda (Mb.) na Makamu Mwenyekiti, Mhe. John Damiano Komba
(Mb.). Nawapongeza pia wajumbe walioteuliwa kuunda Kamati hii. Ushauri wao ndio
umefanikisha maandalizi ya hotuba hii.
9.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Jenista Joachim Mhagama
(Mb.), kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Kamati hii.
10.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi
kwa Wabunge wapya waliochaguliwa hivi karibuni kwa ushindi wa kishindo ambao ni
Mhe. Yusuf Salim Hussein, (Mbunge wa Chambani), Godfrey William Mgimwa, (Mbunge
wa Jimbo la Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya
Kikwete, (Mbunge wa Jimbo la Chalinze).
11.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa
fadhila kama sitawapongeza wanahabari pamoja na wadau wote wa sekta ya habari kwa
kazi nzuri ya kutoa habari na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuuelimisha umma
wa Watanzania. Aidha, napenda kutambua mchango mkubwa wa vijana wote katika
kuinua uchumi kwa kuwa wao ni takriban asilimia
70 ya nguvu kazi ya Taifa letu. Vilevile, niwapongeze wanamichezo wote ambao
wameshiriki katika kuliletea heshima taifa kupitia mashindano ya michezo
mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kwa namna ya pekee nachukua fursa hii, kutoa
pongezi za dhati kwa Timu ya Mpira wa Miguu ya Watoto wanaoishi katika mazingira
magumu kutoka Mkoa wa Mwanza iliyotwaa Kombe
la Dunia la Watoto wa Mitaani nchini Brazili. Hali kadhalika nawapongeza
kwa dhati kabisa wasanii wote ambao wamekuwa kioo cha jamii katika kulitangaza
taifa letu ndani na nje ya nchi yetu.
Nawapongeza hasa kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu katika kuhamasisha
jamii kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.
12.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi
hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa familia na wananchi
wa Jimbo la Kalenga na Jimbo la Chalinze kwa kuondokewa na Wabunge wao,
Marehemu William Augustao Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, ambaye alifariki tarehe 01 Januari 2014 nchini
Afrika Kusini na Marehemu Said Ramadhani Bwanamdogo aliyefariki tarehe 22
Januari 2014. Aidha, ninawapa pole Watanzania wote waliopoteza ndugu zao
kutokana na ajali, majanga na maradhi mbalimbali. Tunamwomba Mwenyezi Mungu
aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina!
13.
Mheshimiwa Spika,
hotuba yangu imegawanyika katika maeneo makuu matano kama ifuatavyo: eneo la
kwanza ni Utangulizi, eneo la pili ni Majukumu ya Wizara, eneo la tatu linahusu Mapitio ya Utekelezaji
wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2013/2014, eneo la nne linahusu Mpango na Bajeti kwa
mwaka 2014/2015 na eneo la tano ni Hitimisho.
B.
MAJUKUMU YA WIZARA
14.
Mheshimiwa
Spika, Wizara inatekeleza majukumu ya msingi yafuatayo:-
i)
Kuandaa na
kusimamia utekelezaji wa Sera za Sekta za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo;
ii)
Kuratibu na
kusimamia masuala ya maendeleo ya vijana ili kuwawezesha kujiajiri, kuajirika
na kujitegemea;
iii) Kuwa Msemaji Mkuu
wa Serikali na kusimamia vyombo vya habari
nchini;
iv) Kuratibu na kusimamia maendeleo ya utamaduni nchini;
v)
Kuratibu na
kusimamia maendeleo ya michezo nchini;
vi)
Kusimamia utendaji
kazi wa Asasi, miradi na programu zilizo chini ya Wizara na
vii)Kuendeleza, kuwezesha na kuratibu masuala ya kuwajengea uwezo
watumishi wa Wizara.
C.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
Mapato na Matumizi
15. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2013/2014, Wizara ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 882,203,000 kutoka vyanzo mbalimbali. Hadi kufikia mwezi Aprili,
2014 jumla ya Shilingi 663,029,569 zilikusanywa ambazo ni
sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo kwa mwaka. Mchanganuo wa makusanyo upo kwenye Kiambatisho Na. I.
16.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014,
Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 17,628,045,000 kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida. Fedha hizo zilijumuisha Mishahara shilingi 9,257,125,000 (Wizara
ni Shilingi 2,617,598,000 na Asasi ni Shilingi 6,639,527,000). Matumizi Mengineyo (OC) shilingi 8,370,920,000
(Wizara ni Shilingi 4,941,920,000 na Asasi ni Shilingi 3,429,000,000). Hadi mwezi Aprili, 2014 jumla ya
Shilingi 13,292,539,498 za Matumizi ya Kawaida zilipokelewa na kutumika
ambapo kati ya fedha hizo Matumizi Mengineyo ni Shilingi 4,740,957,000
na Mishahara ni Shilingi 8,551,582,498.
Miradi ya
Maendeleo
17.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 12,700,000,000 kwa ajili ya
kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2014 jumla ya Shilingi 4,327,500,000 zilipokelewa ambazo
ni sawa na asilimia 34 na Shilingi 2,310,021,000 zilitumika. Miradi
iliyotekelezwa ni pamoja na Upanuzi wa Usikivu wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), Ujenzi wa Ofisi - BAKITA, Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara
la Afrika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
SEKTA YA HABARI
18.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea na utendaji wa kazi zake huku
ikikabiliana na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya
vyombo vya habari kukiuka sheria kwa
kuandika na kutangaza habari ambazo hazizingatii kanuni na maadili ya taaluma
ya uandishi wa habari. Aidha, kuongezeka kwa mifumo na njia za mawasiliano kama
mitandao ya kijamii kwenye “internet” kumeathiri maudhui ya habari zinazotolewa.
19.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto
hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana nazo, zikiwemo kutoa
onyo na kufungia baadhi ya vyombo vya habari vilivyokiuka maadili. Wizara pia
imeelekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutekeleza kikamilifu mpango
wa kusajili wamiliki wote wa mitandao hiyo. Vilevile, Wizara inaendelea kutoa
elimu na kuwaelekeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari kufuata sheria,
kanuni na miongozo iliyowekwa.
20.
Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara imekamilisha maandalizi ya
Muswada wa Sheria ya kusimamia Vyombo vya Habari na sasa uko katika hatua
nzuri. Kwa kuzingatia utaratibu uliopo,
Muswada huu utafikishwa katika Bunge lako Tukufu lijalo la kutunga Sheria.
21.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuimarisha njia za mawasiliano kati ya
Serikali na Wananchi wake, Wizara inafanya maboresho ya Tovuti ya Wananchi ili
kuweza kuimarisha mifumo na monekano wa Tovuti hiyo. Maboresho hayo
yakikamilika, yatawawezesha Wananchi popote walipo
kuwasiliana na Serikali kwa kutumia njia za kisasa. Aidha itawapunguzia
wananchi gharama za kuwasilisha kero,
hoja na maoni mbalimbali katika Taasisi za Serikali. Kazi ya kuijenga upya na
kuimarisha Tovuti hiyo ili kuwa na muonekano mpya unaokidhi mabadiliko ya sasa
ya Sayansi na Teknolojia inatarajiwa kukamilishwa mwisho wa mwaka wa fedha 2013/2014.
22.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea
kukusanya habari, kupiga picha za matukio mbalimbali ya Serikali na kuzihifadhi
katika maktaba; pamoja na kuzisambaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwa
lengo la kutoa habari na kuelimisha jamii. Wizara kama Msemaji Mkuu wa
Serikali, ilifafanua masuala na hoja mbalimbali zinazohusu Serikali.
23.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia Vitengo vya
Mawasiliano Serikalini kwa lengo la kutoa habari na kuelimisha umma juu ya
utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Wizara imetoa mwongozo ulioainisha
taratibu za kuendesha Vitengo hivyo na kuhimiza Wizara na Asasi zote za umma
kuajiri Maafisa Mawasiliano Serikalini. Hali kadhalika, Wizara imeratibu jumla
ya mikutano 255 ya wasemaji wa Asasi za Serikali na Vyombo vya Habari. Mikutano
hii imesaidia kuwaelimisha Wananchi kuhusu shughuli za Serikali zinazofanyika
kwa maendeleo yao.
24.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/2014,
Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa vyombo vya habari katika vikao vya Bunge
vilivyofanyika Dodoma na pia kuhakikisha inawapatia vitambulisho waandishi wa
habari wa ndani na nje wenye sifa za taaluma ya uandishi wa habari.
25.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa
kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kupitia TCRA, ilikamilisha awamu ya kwanza ya
uhamaji wa kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analoji kwenda dijiti. Baada ya zoezi hili tathmini imefanyika
ambayo ilionesha mwitikio mzuri wenye mafanikio. Hivi sasa zoezi hili limeingia katika awamu
ya pili iliyoanza tarehe 31 Machi 2014. Ni
matarajio yetu kwamba uhamaji huu utakamilika kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa
kabla ya tarehe 30, Juni 2015.
26.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Wizara kwa
kushirikiana na TCRA imesajili vituo nane (8) vya redio na vituo viwili (2) vya
televisheni na hivyo kuwezesha Tanzania kuwa na jumla ya vituo 93 vya redio na 28 vya
televisheni. Aidha uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analoji
kwenda mfumo wa dijiti umesadia kupanua wigo wa masafa na kuongeza ubora wa
matangazo.
27.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka 2013/2014, Kamati ya Maudhui ilipokea na kushughulikia malalamiko 7 ya
vituo vya televisheni na redio kutokana na kurusha vipindi ambavyo vilikiuka
maadili ya utangazaji. Kituo binafsi cha televisheni kilicholalamikiwa kwa
kurusha kipindi kilichokiuka kanuni na maadili ya utangazaji kilipewa onyo.
Aidha, vituo 6 vya redio vilivyolalamikiwa kwa kurusha vipindi vilivyokiuka
kanuni za utangazaji na maadili ya uandishi wa habari vilipewa onyo na vingine kutozwa
faini kati ya Shilingi 200,000 na Shilingi 5,000,000.
28.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, TBC imeendelea kuimarisha upanuzi
wa usikivu wa Redio na Televisheni ya Taifa. TBC pia ilirusha matangazo ya
vikao vya Bunge moja kwa moja. Aidha, TBC ilirusha matangazo ya Bunge Maalum la
Katiba kwa lugha za alama kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum. Pamoja na
kazi hizo, TBC inakabiliwa na tatizo la uchakavu
wa vifaa vya kurushia matangazo. Uchakavu huo wakati mwingine umesababisha tatizo
la kukatika kwa matangazo yakiwemo matangazo ya Bunge.
29.
Mheshimiwa Spika, naomba waheshimiwa
wabunge wawe wavumilivu kwani Wizara imejipanga katika kuendelea kutatua
changamoto hizo ili kuboresha huduma zitolewazo na TBC. Kupitia Bunge lako
Tukufu niwaombe Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono kufanikisha malengo
tuliyojiwekea.
30.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea
kutatua changamoto za TBC, mwezi Aprili, 2014 imepokea gari jipya la kisasa la matangazo
kutoka Serikali ya Watu wa China. Gari hili litasaidia sana kuongeza nguvu
katika kupunguza tatizo la uchakavu wa vifaa. Sambamba na hatua hizo, Wataalamu
watano (5) wa TBC walipelekwa nchini China kupata mafunzo maalum ya namna ya
kutumia gari hilo pamoja na vifaa husika.
31.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
wa 2013/2014, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imeendelea na mkakati wa
upanuzi wa kiwanda cha uchapaji. Katika mkakati huo, makubaliano na Benki ya
Rasilimali Tanzania (TIB) yamekamilika ambapo TIB itaipatia TSN mkopo wa Shilingi
bilioni 2.7 kwa ajili ya kujenga jengo la kitega uchumi.
32.
Mheshimiwa Spika, katika kupanua wigo wa mapato, TSN na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameingia mkataba wa ubia wa kuendeleza kiwanja
kilichopo Kitalu Na. 27, Central Business Park, Dodoma, kwa ajili ya kujenga
jengo la kupangisha. Maandalizi ya ujenzi yameanza.
33.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha
magazeti, TSN imeongeza kurasa za habari katika magazeti ya ‘Daily News’ na
Habari Leo. Vilevile, imeongeza weledi katika uhariri wa taarifa ndani ya
magazeti hayo. Uchapaji wa magazeti hayo unazingatia sera na maadili ya
uandishi wa habari.
34.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha usambazaji wa magazeti, Kampuni imepata pikipiki
20 toka Serikali ya Watu wa China kwa ajili ya usambazaji wa mijini. Aidha, TSN,
imeingia makubaliano na kampuni za
usafirishaji kusafirisha magazeti ndani na nje ya nchi ili kuwezesha
upatikanaji wa habari kwa wakati.
SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA
35.
Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia masuala ya vijana mwaka
2013/2014, Wizara imekabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo, baadhi ya
Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya kutokuajiri Maafisa Vijana, uelewa
mdogo wa vijana katika kubuni, kutayarisha maandiko ya miradi, kuanzisha na
kutekeleza miradi endelevu.
36.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni vijana
wengi kukosa ujuzi na maarifa ya ujasiriamali na biashara ikiwa ni pamoja na kukosa
ujuzi wa matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazopata kupitia Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana.
37.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizi, Wizara imeendelea
kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi kwa kuwapa mafunzo na ujuzi katika maeneo
ya ujasiriamali, uanzishaji wa miradi endelevu ya uzalishaji mali, uongozi,
stadi za maisha na matumizi sahihi ya mikopo. Mafunzo haya yametolewa kwa vijana 668 katika
ngazi ya Mikoa na Wilaya katika mwaka wa fedha 2013/2014.
38.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kupungua kwa nafasi za ajira katika
sekta rasmi ikilinganishwa na idadi ya vijana wanaoingia katika soko la ajira
kila mwaka, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya vijana imeendelea
kuhamasisha vijana kuunda makampuni binafsi ya biashara na vikundi vya kuzalisha
mali ili waweze kujiajiri. Mpango huu utasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa
ajira kwa vijana.
39.
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha na kuongeza mitaji katika miradi
na kampuni za vijana zinazoanzishwa, Wizara imeratibu mpango wa kuanzisha Benki
ya Vijana na tayari Mshauri Mwelekezi amepatikana. Mshauri huyo anaendelea na
upembuzi yakinifu wa uanzishwaji wa Benki hiyo.
40. Mheshimiwa Spika, kuhusu Mfuko wa Maendelo
ya Vijana, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwongozo wa kusimamia
Mfuko huu umeandaliwa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote tangu
mwezi Agosti 2013. Kulingana na Mwongozo huu, kila Halmashauri inahitajika
kuanzisha SACCOS ya Vijana ambayo itashughulikia utoaji wa mikopo hii. Hadi kufikia Aprili, 2014, Halmashauri 22 kati ya 151 zimeanzisha SACCOS za Vijana.
41.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi bilioni 6.1 zilitengwa kwa ajili ya Mfuko huu. Hadi
Aprili, 2014, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi 2,000,000,000. Kati ya fedha hizo zilizokopeshwa ni
Shilingi 172,609,000 kwa Miradi ya
vikundi vya vijana 25. Hata hivyo, Wizara inaendelea na uchambuzi wa maombi ya vikundi 1,178 yenye thamani ya Shilingi 8,421,906,750 ili kuweza kuvikopesha
vikundi vitakavyotimiza vigezo vilivyobainishwa kwenye mwongozo.
42.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza Programu ya “Elimu
ya Stadi za Maisha kwa vijana walio nje ya shule”. Katika kipindi hiki, Wizara
imeandaa mafunzo kwa waelimishaji 75 wa kitaifa ambao watatoa mafunzo kwa
waelimishaji rika kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Kata. Programu hii itawasaidia
vijana kujitambua na kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maisha yao.
43.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha maendeleo ya wananchi, kudumisha umoja,
amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru. Kwa
mwaka 2013, Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 5 Mei, 2013 katika
kijiji cha Chokocho, Mkoani Kusini Pemba ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Ali
Mohamed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Maadhimisho ya
kilele cha mbio hizo yalifanyika mkoani Iringa tarehe 14, Oktoba, 2013 na Mgeni
Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Kupitia mbio hizo, jumla ya miradi ya maendeleo 1229 yenye thamani ya Sh. 158,587,667,613.40 ilizinduliwa au kuwekewa mawe ya
msingi. Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2014 umefanyika tarehe 2, Mei
2014 Mkoani Kagera; na Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
44.
Mheshimiwa Spika, sambamba na
maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wizara iliratibu maadhimisho
ya Wiki ya Vijana kitaifa ambayo yalianza tarehe 8 Oktoba na kuhitimishwa
tarehe 14 Oktoba, 2013 mkoani Iringa. Lengo la maadhimisho hayo ni
kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini na kuwapa fursa ya
kubadilishana uzoefu, ujuzi, kuonesha vipaji na ubunifu wa kazi zao, pamoja na kujenga
mtandao na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana.
45.
Mheshimiwa Spika, Maonesho katika Wiki ya Vijana yalishirikisha
wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na ofisi za mikoa 10, Idara za Serikali 16,
Halmashauri za Wilaya 21, Asasi za Kiraia 14, Vikundi vya Vijana Wajasiriamali
53, Vyuo Vikuu vya Elimu 3 na Taasisi za Kibenki 3. Jumla ya watu waliotembelea
mabanda ya maonesho ya Wiki ya Vijana ilikuwa ni 39,361. Aidha, katika Wiki
hiyo, Vijana 300 kutoka makundi mbalimbali ya Vijana walishiriki katika
midahalo ambapo pia walipatiwa mafunzo ya aina tofauti yenye lengo la
kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali ya maendeleo ya vijana.
46.
Mheshimiwa
Spika, washiriki wa Wiki ya Vijana pia walipata fursa ya kupewa
huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU/UKIMWI kwa hiari kupitia taasisi
zinazojihusisha na afya zilizoshiriki katika maadhimisho hayo, kama vile
WAMATA, AMREF – ANGAZA, HOSPITALI YA RUFAA IRINGA na JHPIEGO - UHAI CT. Jumla
ya Vijana 613 walipima afya zao wakiwemo wanawake 397 na wanaume 216, kati yao
vijana 27 sawa na asilimia 4.4 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU. Vijana
waliogundulika kuwa na maambukizi walipatiwa huduma ya ushauri wa namna ya
kuishi vizuri na kwa matumaini na jinsi ya kuendelea kupata huduma za
afya.
SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI
47.
Mheshimiwa
Spika, athari za utandawazi na
maendeleo yenye kasi kubwa ya sayansi na teknolojia vimeendelea kuwa ni changamoto
kubwa inayokabili Maendeleo ya Utamaduni.
Mmomonyoko wa maadili ulio dhahiri nchini, sio tu miongoni mwa watoto na
vijana bali pia hata baadhi ya watu wazima, ni matokeo ya athari hasi za
utandawazi na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia yanayoambatana na matumizi
mapana ya televisheni na mitandao anuwai ya kijamii. Kwa upande mwingine,
upatikanaji kirahisi wa mitambo ya kurudufu kazi za wasanii, hasa wa filamu na
muziki, umeendeleza dhuluma ya kipato kwa wasanii wengi huku ukiwaneemesha
mapromota na wasambazaji wa bidhaa za filamu na muziki ambao sio wasanii.
Pamoja na changamoto hizi, Wizara kupitia Sekta ya
Maendeleo ya Utamaduni imetekeleza kazi zifuatazo katika mwaka wa fedha wa
2013/2014.
48.
Mheshimwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu za tasnia ya
utamaduni, Maofisa wawili walipata mafunzo ya namna ya kuainisha namba za
misimbo (code numbers) za sekta ya utamaduni ambazo zitatumika kitaifa na
kimataifa. Aidha, Wizara ilifanya tafiti za maktabani za lugha za jamii 10 na utafiti
wa uwandani katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ili kuhifadhi sarufi, misamiati
na istilahi za lugha ya Taifa - Kiswahili.
49.
Mheshimiwa Spika, mintaarafu utafiti wa mila na desturi, Wizara ilifanya utafiti wa kina kuhusu mila za jando
na unyago miongoni mwa jamii za Wamakonde, Wamakua na Wayao. Utafiti huo
umewezesha kukamilisha maandalizi
ya pendekezo la elementi ya urithi
usioshikika ambao hatimaye Serikali itaomba urithi huo uingizwe kwenye orodha
ya urithi wa utamaduni wa Dunia unaotambuliwa na UNESCO. Elementi hiyo ni ya
ngoma ya “Nankachanga” kutoka kijiji cha Namahonga, Wilaya ya Tandahimba, Mkoa
wa Mtwara.
50.
Mheshimwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na fursa
za ajira zinazotokana na nchi yetu kuteuliwa kuwa Makao Makuu ya Kamisheni ya
Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika hili, Wizara kwa kushirikiana
na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, iliratibu zoezi la kuwapata Watanzania wenye sifa stahiki za
kuajirika katika Kamisheni hiyo. Ajira katika Kamisheni zitashindaniwa na nchi
zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ni muhimu kwa Tanzania
kuwa na wagombea sadifu ili kuhimili vishindo vya kinyang’anyiro hicho.
51.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Programu ya Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika, kazi ya ukusanyaji wa kumbukumbu
za mapambano ya kupigania uhuru nchini iliendelea kufanywa kwa kushirikiana na
Maofisa Utamaduni wa Mikoa na Wilaya. Kwa kipindi cha mwaka 2013/2014, jumla ya
kumbukumbu 63 zimerekodiwa katika kanzi data ya Programu. Programu hii ni muhimu sana katika kutunza na
kuhifadhi kumbukumbu za Ukombozi wa Bara la Afrika. Wizara inaendelea kutafuta
ufadhili kufanikisha malengo ya Programu.
52.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo ni wadau wakuu
ili kujenga uelewa zaidi wa Programu. Aidha, washirika katika Programu hii
kutoka Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji walikuja nchini kujifunza namna
Tanzania inavyotekeleza shughuli za uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu za
historia ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.
53.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Kiswahili la
Taifa (BAKITA) liliandaa na kurusha vipindi 52 vya ‘Lugha ya Taifa’ kupitia TBC Taifa, vipindi 52 vya ‘Kumepambazuka’ kupitia Radio One
na vipindi 52 vya ‘Ulimwengu wa Kiswahili’ kupitia Televisheni ya Taifa-TBC1. Vilevile, Baraza lilisoma jumla ya miswada 24
ya vitabu vya taaluma na kuvipatia ithibati ya lugha.
54.
Mheshimiwa Spika,
Baraza limeratibu na kutoa huduma ya tafsiri kwa Asasi 14 za Serikali,
Mashirika ya Umma, pamoja na watu binafsi. Aidha, huduma ya ukalimani ilitolewa
kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika huko Addis
Ababa, Ethiopia, mwezi Julai, 2013 na mwezi Januari, 2014. Vilevile, ukalimani ulifanyika kwenye Mkutano
wa Bunge la Afrika nchini Afrika Kusini mwezi Novemba, 2013 na Machi, 2014.
55.
Mheshimiwa Spika,
Baraza limeendelea kufuatilia matumizi ya Kiswahili na kubaini jumla ya makosa
75 yaliyofanywa na vyombo vya habari na watumiaji wengine wa Kiswahili kwa
kusahihisha na kutoa ushauri wa matumizi stahiki. Baraza katika kujiimarisha,
limeongeza wigo wa kiutendaji kwa kuandaa Kamusi Kuu ambapo fafanuzi za maneno
(utomeshaji) zimeingizwa na warsha tatu za kuhakiki zimefanyika.
56.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) limeendesha midahalo 52 ya Jukwaa la Sanaa kwa wasanii, waandishi wa
habari na wadau wa sanaa 3,850. Vilevile, Baraza kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa sanaa, limeendesha mafunzo ya utambaji wa hadithi, ngoma za asili
kwa watoto 200 wa shule za msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam kati ya Februari
na Machi, 2014 kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vyao katika fani
husika.
57.
Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo na
kuhamasisha watumishi 34 wa Baraza, wasanii na wadau 98 kupitia Jukwaa la Sanaa
kuhusu umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya VVU na UKIMWI. Baraza limeendelea kuingiza taarifa muhimu za
wasanii na wadau wa sanaa za muziki katika mfumo wa kielektroniki unaounganisha
Taasisi za TRA, COSOTA, Bodi ya Filamu na BASATA. Hii itaimarisha urasimishaji
wa tasnia ya muziki. Aidha, Baraza limeendelea na hatua za awali za uandaaji wa
mfumo wa kanzi data za wasanii mahiri na kukusanya taarifa zao muhimu.
58.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha
2013/2014, Bodi ya Filamu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Filamu
na Michezo ya Kuigiza pamoja na Kanuni zake. Bodi, kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea kuhimiza matumizi ya stempu za kodi. Hadi sasa,
jumla ya wadau 86 wamechukua Stempu 4,380,000 zilizotolewa kwa upacha
(duplicate) kwa ajili ya kuweka kwenye kazi za filamu na muziki. Kati ya hizo 3,810,000
ni kwa kazi za filamu na 570,000 ni za muziki.
59.
Mheshimiwa
Spika, Bodi imepitia miswada 139
ya kutengenezea filamu kwa watengenezaji wa ndani na nje ya nchi. Hadi kufikia Aprili, 2014, jumla ya filamu
1,206 sawa na CD 2,412 zilikaguliwa na kuwekewa madaraja. Kati ya filamu hizo,
127 zilifanyiwa marekebisho. Filamu 7 hazikuruhusiwa kuonyeshwa hadharani.
Aidha, kati ya filamu 215 za nje zilizowasilishwa, filamu 2 zilielekezwa
kufanyiwa marekebisho. Jumla ya filamu 5 za nje zilizowasilishwa zilizuiliwa
kuonyeshwa hadharani. Aidha, Bodi imekagua na kuidhinisha maeneo 13 ya
uzalishaji wa filamu.
60.
Mheshimiwa
Spika, Bodi imeendelea kutoa
elimu kuhusu urasimishaji wa tasnia ya filamu kupitia matangazo kwenye
magazeti, vipeperushi, mabango ya barabarani, maadhimisho na sherehe mbalimbali,
vipindi mbalimbali vya TV na Redio na vikao vya wadau.
61.
Mheshimiwa Spika, Bodi ilihamasisha
wadau kushiriki katika tuzo mbalimbali za filamu kitaifa na kimataifa ambapo
hadi kufikia Aprili 2014, jumla ya filamu 10 ziliingia katika tuzo mbalimbali
na filamu ya Mdundiko ya Kitanzania ilishinda katika tuzo ya kimataifa huko
Marekani.
62.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) iliendesha mafunzo ya stashahada kwa
wanachuo wapatao 238 na mafunzo ya muda mfupi kwa wasanii 255 walio kazini.
Vilevile, inaendelea na kazi ya kukamilisha
mitaala ya shahada ya kwanza ya sanaa za maonyesho na ufundi.
63.
Mheshimiwa Spika, TaSUBa ilisimamia na
kuendesha tamasha la 32 la Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania ambapo vikundi 40
vya sanaa za maonyesho na vikundi 12 vya sanaa za ufundi vya ndani na nje ya
nchi vilishiriki. Aidha, TaSUBa ilishiriki mikutano ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyoitishwa kujadili mustakabali wa vituo vya Jumuiya vyenye ubora
uliotukuka (Centre of Exellence), ambapo TaSUBa ni kimojawapo cha vituo hivyo.
SEKTA
YA MAENDELEO YA MICHEZO
64.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara imeendelea kukabiliana na
changamoto mbalimbali zikiwemo uchache wa wataalamu waliobobea katika fani
mbalimbali za michezo, upungufu wa miundombinu inayokidhi mahitaji ya sasa,
mwamko mdogo wa jamii kushiriki katika michezo na udhaifu wa uongozi katika
baadhi ya vyama mbalimbali vya michezo.
Pamoja na changamoto hizo, Wizara katika kipindi cha
mwaka wa fedha wa 2013/2014 imetekeleza kazi zifuatazo.
65.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya Stashahada ya Elimu
ya Ufundishaji Michezo na Stashahada ya Uongozi na Utawala kwa wanachuo 40
katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo, Malya, mkoani Mwanza. Aidha, Wizara
imeendesha Mafunzo ya muda mfupi ya fani mbalimbali za michezo kwa vijana 200,
walimu 100 wa shule za Msingi, walimu 100 wa shule za Sekondari, Viongozi wa
Michezo na Makocha 102 katika Vituo vya Michezo vya Kanda ya Kaskazini (Arusha)
na Kusini (Songea). Hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya walimu ambao hushiriki
katika uendeshaji na ufundishaji wa michezo kwa ajili ya mashindano ya shule za
msingi (UMITASHUMTA) na shule za sekondari (UMISETA) ni wahitimu wa Chuo cha
Maendeleo ya Michezo Malya, Vituo vya Michezo na Mpango wa Michezo kwa Jamii.
66.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea
kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano wa kimataifa na kufuatilia utekelezaji wa
Mikataba kati ya nchi marafiki na Tanzania katika Sekta ya Michezo. Kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China, Wizara imekamilisha hatua za awali za kujenga miundombinu ya
Mchezo wa kupanda Majabali (Rock Climbing) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara iliendesha Kongamano la
Kimataifa la Viongozi Wanawake wa Michezo lililofanyika Dar es Salaam tarehe 16
– 18 Desemba, 2013 na kushirikisha jumla ya nchi 17 za Bara la Afrika na Ulaya.
67.
Mheshimiwa Spika, Wizara, kwa kushirikiana na Vyama vya Michezo,
imeendelea kufanya maandalizi ya timu za Taifa zitakazoshiriki kwenye michezo
ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland, mwezi Julai, 2014. Timu za Michezo ya Riadha, Ngumi, Kuogelea,
Mieleka, Baiskeli, Judo, Paralimpiki na Mpira wa Meza zinatarajiwa kushiriki
katika mashindano hayo. Aidha, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, timu sita za Taifa za mchezo wa Riadha, Ngumi, Kuogelea,
Judo, Kunyanyua Vitu vizito na Mpira wa Meza zimepata fursa ya kuweka kambi za
mazoezi nchini China, Uturuki, Ethiopia na New Zealand kwa ajili ya maandalizi
ya michezo ya Jumuiya ya Madola.
68.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea
kusimamia ukamilishaji wa ukarabati wa Uwanja wa Uhuru ambao ni sehemu ya eneo
Changamani la Michezo lililoko Dar es Salaam. Ukarabati huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014.
69.
Mheshimiwa Spika,
Wizara ilitoa huduma ya Kinga na Tiba kwa wanamichezo na wadau wa michezo
108,000 wa timu za michezo mbalimbali. Vilevile, Wizara imeendelea na upimaji
na utoaji wa elimu kwa wanamichezo kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu
haramu za kuongeza nguvu katika michezo.
70.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupambana na dawa na mbinu haramu za kuongeza nguvu
michezoni, Wizara imeendelea kutumia matukio ya michezo kama vile Ligi Kuu ya
Vodacom, Kambi za Timu za Taifa na Mashindano ya Riadha na Ngumi ya Kitaifa na
Kimataifa, kuchukua sampuli mbalimbali (damu, mate, jasho n.k) za wanamichezo
kwa ajili ya vipimo vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu katika michezo kwa
uchunguzi zaidi kwenye maabara zilizoko nchini Afrika Kusini. Hadi kufikia
Aprili, 2014 wanamichezo 27 walichukuliwa vipimo. Hata hivyo, hakuna
aliyegundulika kutumia dawa na mbinu haramu baada ya majibu ya maabara.
71.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
kwa kushirikiana na “UK Sport” na “British Council”, kupitia mradi wa
“International Inspiration”, limekamilisha uandaaji wa mifumo rasmi ya Elimu na
Ithibati ya Ufundishaji wa Michezo Nchini; Michezo Shirikishi kwa Jamii;
Ufuatiliaji na Tathmini ya Maendeleo ya Michezo Nchini; na Utambuzi na Ukuzaji
wa Vipaji vya Michezo Miongoni mwa Vijana. Mifumo hiyo inalenga kuinua
maendeleo ya michezo nchini na inaendelea kufanyiwa majaribio kwa ajili ya
utekelezaji.
72.
Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo ya utawala bora kwa vyama vya michezo 17, na
kusimamia uchaguzi kwa vyama na mashirikisho ya michezo 14. Aidha, kwa
kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Baraza, limeendesha mafunzo ya
michezo kwa jamii kwa walimu 76 wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya
ya Mtwara Vijijini.
73.
Mheshimiwa Spika, Baraza liliandaa na kuendesha Kongamano la Kimataifa
kuhusu Mfumo wa Elimu ya Michezo kwa Jamii kwa Nchi za Kanda ya V ya Michezo
Barani Afrika. Kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuangalia namna ya kuwa na
mfumo mmoja wa utoaji wa Elimu ya Michezo kwa Jamii miongoni mwa nchi wanachama. Kongamano hilo lilifanyika mwezi Novemba,
2013 huko Arusha na kuhudhuriwa na nchi saba ambazo ni Uganda, Kenya, Rwanda,
Ethiopia, Misri, Zimbabwe na Tanzania.
74.
Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo ya uamuzi na ukocha kwa walimu na wanafunzi
761, kati ya hao walimu ni 421 na wanafunzi ni 340. Mafunzo haya, yaliyo katika
majaribio ya mradi wa “International Inspiration” yamefanyika katika mikoa ya
Dar es salaam, Arusha, Ruvuma, Mwanza na Mjini Magharibi, Zanzibar.
75.
Mheshimiwa Spika, Baraza, kwa kushirikiana na
Asasi ya Kimataifa ya “Tackle Africa” inayojishughulisha na utoaji wa elimu ya
kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kutumia mchezo wa soka, liliendesha mafunzo kwa wanawake 140 na
wasichana 8,000 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Lindi.
UTAWALA NA MENEJIMENTI YA RASILIMALI WATU
76.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
2013/2014, watumishi 51 wamehudhuria mafunzo katika fani mbalimbali. Kati ya hao, watumishi thelathini na wawili (32),
wamehudhuria mafunzo elekezi ambayo yaliandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na
Taasisi mbalimbali za Serikali. Aidha,
watumishi kumi na saba (17) wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi na
watumishi wawili (2) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi.
77.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha Utawala Bora na ushirikishwaji watumishi sehemu za kazi,
Wizara imeandaa na kuendesha vikao viwili vya Baraza la Wafanyakazi pamoja na
kusimamia uendeshwaji wa vikao mbalimbali vya kiutawala katika kuimarisha
utendaji kazi.
78.
Mheshimiwa Spika, katika usimamizi wa haki na
maslahi ya watumishi, Wizara imewapandisha vyeo watumishi 32 wanaostahili kwa
kuzingatia miundo ya kada zao, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa
Umma toleo la mwaka 1999 na 2008 pamoja na taarifa za Upimaji Kazi wa Wazi
(OPRAS).
D: MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014 /
2015
79.
Mheshimiwa Spika, Mpango
na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2014/2015 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016;
Malengo ya Taifa ya MKUKUTA II; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2010
– 2015; Mpango Mkakati wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo 2011/2012
– 2015/2016; Maagizo ya Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, aliyoyatoa kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kwa nyakati tofauti; Mwongozo wa Utayarishaji wa Mpango na Bajeti kwa
mwaka 2014/2015 na ushauri uliotolewa na Bunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa nyakati tofauti.
SEKTA YA HABARI
80.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara imepanga
kutekeleza yafuatayo:-
(i)
Kuisemea Serikali katika masuala muhimu yanayohitaji
ufafanuzi kwa wananchi;
(ii)
Kukusanya habari mbalimbali za matukio ya kiserikali na
kuyasambaza kwa wananchi;
(iii)
Kuratibu Vitengo vya Mawasiliano Serikalini;
(iv)
Kusajili magazeti na machapisho;
(v)
Kuandaa jarida la Nchi Yetu na kulisambaza;
(vi)
Kuratibu waandishi wa habari katika shughuli za kitaifa
na kimataifa na
(vii)
Kuratibu utekelezaji wa Mradi wa Habari kwa Umma.
81.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015,
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linakusudia:-
(i)
Kurusha matangazo ya vikao vya Bunge;
(ii)
Kulipia huduma ya kukodi “satellite” kwa ajili ya
matangazo ya moja kwa moja ya televisheni;
(iii)
Kuhamisha na kujenga mitambo miwili (2) ya FM katika
maeneo ya StarMedia (T) Ltd ili kuboresha usikivu wa matangazo ya redio. Maeneo
yatakayohusika na zoezi hilo la uhamishaji wa mitambo yake ya FM ni Iringa na
Dodoma;
(iv)
Kujenga mtambo mpya mmoja (1) wa FM redio kwa ajili ya
kuboresha usikivu wa matangazo katika eneo la Ngorongoro mkoani Arusha na
(v)
Kujenga studio mbili (2) za redio katika Mikoa ya Dar es
Salaam na Dodoma pamoja na kufunga vifaa vya kisasa.
82.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa mwaka 2014/2015
imepanga kutekeleza yafuatayo:-
(i) Kukamilisha
mradi wa upanuzi wa kiwanda cha uchapaji na
(ii) Kuendelea na mchakato wa kuendeleza kiwanja
kilichopo Kitalu Na. 27, Central Business Park, Dodoma, kwa ubia na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA).
83.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Wizara kupitia
Kamati ya Maudhui ya Utangazaji imepanga kutekeleza yafuatayo:-
(i)
Kupitia na kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria na
Kanuni za Utangazaji;
(ii)
Kutengeneza rasimu ya kanuni ndogo za maudhui ya
Utamaduni wa Mtanzania;
(iii) Kutengeneza mwongozo wa udhamini wa matangazo (Codes of Advertising
and Sponsorship);
(iv) Kuanzisha utaratibu
wa kutoa motisha (Incentive scheme) kwa watengenezaji na vituo vya utangazaji
vitakavyorusha vipindi vyenye maudhui bora ya Mtanzania;
(v)
Kuendesha warsha za mashauriano na wadau wa maudhui wa
kujitegemea na
(vi)
Kusimamia awamu ya pili ya uhamaji kutoka mfumo wa
analoji kwenda mfumo wa dijiti katika miji yote ambayo haijafikiwa na mfumo huu
mpya.
SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA
84.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2014/2015 Wizara imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
(i)
Kuratibu mafunzo ya Ujasiriamali; Uanzishaji na
Uendeshaji wa Miradi na Kampuni Endelevu, Uongozi na Stadi za Maisha kwa
viongozi wa vikundi vya vijana vya uzalishaji mali na asasi za vijana ili
kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika, hivyo kujikimu kiuchumi na kijamii;
(ii)
Kuratibu Mbio za Mwenge wa Uhuru ili kuhamasisha wananchi
kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Aidha, Wizara itaratibu
maadhimisho ya Wiki ya Vijana ili kuwapa fursa za kubadilishana uzoefu, ujuzi,
kuonesha vipaji na kazi zao za
uzalishaji mali, ubunifu pamoja na kuwawezesha kujenga mitandao baina yao na
wadau mbalimbali;
(iii) Kuendelea na
maandalizi ya uanzishwaji wa Benki ya Vijana ili kuwezesha vijana pamoja na
SACCOS za vijana kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi;
(iv)
Kuendelea kuwezesha Vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo
yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waweze kujiajiri
wenyewe na hivyo kupunguza tatizo la ajira miongoni mwao na umaskini kwa ujumla
na
(v)
Kuimarisha vituo vitatu vya mafunzo ya vijana ili viweze
kutumika ipasavyo katika kutoa mafunzo ya ujasiri, ujasiriamali, uongozi na
stadi za maisha.
SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI
85.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha
2014/2015, Wizara itatekeleza majukumu yafuatayo:-
(i)
Kuratibu mjadala wa Kitaifa kuhusu maadili ya Mtanzania;
(ii)
Kukuza na kuendeleza matumizi sanifu na fasaha ya lugha
ya Kiswahili na kufanya utafiti wa msamiati wa lugha za jamii;
(iii) Kuratibu mikutano,
matamasha ya sanaa na ushiriki wa wasanii katika Sherehe za Kitaifa;
(iv) Kuratibu
utafiti, uhifadhi na uorodheshaji wa urithi wa utamaduni na
(v)
Kuratibu utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa Jumba la
Utamaduni na Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.
86.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la
Kiswahili la Taifa (BAKITA) limepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
(i)
Kuandaa na kurusha vipindi 52 vya ‘Lugha ya Taifa’
katika TBC Taifa, vipindi 52 vya ‘Kumepambazuka’ katika Radio One na
vipindi 52 vya ‘Ulimwengu wa Kiswahili’ katika Televisheni ya Taifa (TBC1)
ili kuhamasisha na kuelimisha matumizi sahihi ya Lugha ya Kiswahili;
(ii)
Kusoma Miswada ya vitabu vya taaluma na kuipatia ithibati
ya lugha;
(iii)
Kuratibu na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani katika
mikutano ya kitaifa na kimataifa, shughuli za mashirika, makampuni na watu
binafsi;
(iv)
Kuchunguza makosa ya Kiswahili yanayofanywa na vyombo vya
habari na watumiaji wengine na kufanya masahihisho ya makosa hayo;
(v)
Kuandaa Kamusi Kuu ya Kiswahili Sanifu;
(vi)
Kuchapisha Kitabu cha Furahia Kiswahili (Kiswahili kwa
Wageni) na
(vii)
Kukarabati majengo ya ofisi yaliyonunuliwa kutoka Shirika
la Bima la Taifa.
87.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) limepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
(i)
Kuendesha mafunzo ya utambaji hadithi, ngoma za asili na
uigizaji kwa watoto 200 wa shule za msingi 5 za Mkoa wa Dar es salaam kwa lengo
la kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto katika fani husika;
(ii)
Kuendesha mafunzo ya sanaa na ujasiriamali kwa wasanii
100 katika mkoa wa Tabora;
(iii)
Kuendesha midahalo 30 kwa wasanii, waandishi wa habari na
wadau wa sanaa 3,000;
(iv)
Kusajili wasanii na wadau wanaojishughulisha na shughuli
za sanaa katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro na Mbeya;
(v)
Kusanifu, kuboresha na kuhifadhi maelezo ya wasanii katika
kanzi data ya BASATA;
(vi)
Kutoa elimu ya urasimishaji wa tasnia ya muziki kwa wadau
wa sanaa na
(vii)
Kuendelea na ujenzi wa Ukumbi wa Wazi wa sanaa na
mafunzo.
88.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Bodi ya
Filamu imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo;
(i)
Kuendelea na Urasimishaji wa Tasnia ya Filamu;
(ii)
Kukagua
na kuweka madaraja ya filamu 600;
(iii)
Kupitia
miswada 150 ya kutengeneza filamu na kutoa vibali 150 vya kutengeneza filamu
kwa waombaji wa ndani na nje ya nchi;
(iv)
Kuendelea
kutoa elimu ya kulinda Maadili ya Mtanzania kupitia tasnia ya filamu na
(v)
Kufanya
utafiti wa masuala ya filamu na kuendesha mafunzo ya kujenga weledi kwa wadau
150 wa filamu.
89.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
(i)
Kuendesha mafunzo
ya stashahada kwa washiriki 250 na mafunzo ya muda mfupi kwa wasanii 270 walio
kazini;
(ii)
Kusimamia na kuendesha Tamasha la 33 la Sanaa na
Utamaduni wa Mtanzania na
(iii)
Kuboresha studio ya picha jongefu na kununua vifaa vya
muziki.
SEKTA YA
MAENDELEO YA MICHEZO
90.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara
itatekeleza yafuatayo:-
(i)
Kuratibu ushiriki
wa timu za Taifa kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow,
Scotland, mwezi Julai 2014;
(ii)
Kutoa mafunzo ya
Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji wa Michezo na Stashahada ya Utawala na
Uongozi wa Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya;
(iii)
Kutoa huduma ya
tiba na kinga kwa wanamichezo na kuendelea na juhudi za kudhibiti matumizi ya
dawa na mbinu haramu za kuongeza nguvu katika michezo;
(iv)
Kuendesha mafunzo
ya muda mfupi ya fani mbalimbali za michezo kwa wadau 200 katika Vituo vya Michezo
vya Kanda ya Kusini (Songea) na Kaskazini (Arusha);
(v)
Kusajili Vyama na Vilabu
vya Michezo;
(vi)
Kuimarisha
uendeshaji wa michezo shuleni na ubora wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA
kwa kutoa nafasi zaidi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kupata
mafunzo ya ufundishaji wa michezo mbalimbali katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo
Malya, Vituo vya Michezo vya Arusha na Songea na fursa nyingine kwa kadri
zitakavyopatikana;
(vii)
Kuratibu
ukamilishaji wa Uboreshaji wa Uwanja wa Uhuru na
(viii)
Kuratibu uendeshaji
wa Uwanja wa Taifa na uboreshaji wa miundombinu katika Chuo cha Maendeleo ya
Michezo Malya.
91.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) litatekeleza yafuatayo:-
(i)
Kuandaa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa walimu 200
wa michezo kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za serikali za mitaa kupitia
Mpango wa Michezo Jumuishi kwa Jamii “Integrated Community Sports”;
(ii)
Kutoa mafunzo ya Utawala Bora katika Sekta ya Michezo kwa
viongozi wa Mashirikisho na Vyama Vya Michezo katika ngazi mbalimbali;
(iii)
Kuratibu na kusimamia chaguzi za Vyama Vitano (5) vya Michezo
na
(iv)
Kuhamasisha wadau mbalimbali wa Michezo kushiriki katika
majaribio ya kutumia mifumo rasmi ya michezo katika kutekeleza Programu zao za Maendeleo
ya Michezo nchini.
UTAWALA NA MENEJIMENTI YA RASILIMALI WATU
92.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo:-
(i)
Kuendelea
kuwajengea uwezo watumishi kwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa kuzingatia
makundi ya kada zao. Mafunzo hayo
yatalenga katika kuimarisha utendaji kazi. Aidha, Wizara itatoa elimu ya
maadili kwa watumishi ili kuimarisha nidhamu ya kazi;
(ii)
Kuendelea kuhamasisha
watumishi kukubali kupimwa UKIMWI ili kutambua hali zao. Aidha, Wizara itaendelea kutoa msaada wa
chakula na lishe kwa watumishi wanaoishi na VVU na UKIMWI ambao wamejitokeza;
(iii)
Kuhakikisha
watumishi wanaostahili wanapandishwa vyeo kwa kuzingatia miundo ya kada zao,
Sera ya Menejimenti katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 na 2008 pamoja na
taarifa za Upimaji Kazi wa Wazi (OPRAS) na
(iv)
Kuendelea
kuimarisha utawala bora na ushirikishwaji watumishi sehemu za kazi kwa
kuendesha vikao vya Baraza la Wafanyakazi pamoja na vikao vingine vya kiutawala
ili kuimarisha utendaji kazi.
E: HITIMISHO
93.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
itaendeleza
mafanikio yaliyopatikana katika Sekta inazozisimamia ili ziweze kuchangia zaidi
katika maendeleo ya nchi yetu. Hii ni pamoja na kuongeza ajira, kipato, kulinda
mazingira, kudumisha amani na mshikamano katika jamii. Wizara itaendelea
kukabiliana na changamoto zilizoainishwa katika hotuba hii ili zipatiwe
ufumbuzi ili fursa zinazopatikana katika Sekta za Wizara ziweze kutumika
ipasavyo katika kuleta maendeleo ya nchi. Napenda kuwahakikishia wananchi ya kwamba
Wizara ina nia thabiti ya kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo hatua kwa
hatua kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
SHUKRANI
94.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani za dhati kwa
wote walioshirikiana nasi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 katika
kutimiza malengo yetu. Ushirikiano huu utaendelezwa na kuimarishwa zaidi kwa
manufaa ya Taifa ili kuhakikisha kuwa
umma wa Watanzania unapata taarifa za kina na za uhakika, vijana wanaendelea kujiajiri
na kuajirika, maadili na utamaduni wa Mtanzania unazingatiwa, pamoja na kuwa Taifa lenye ufanisi kupitia michezo. Mafanikio
ya utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara yamewezekana kutokana na
ushirikiano uliopo miongoni mwa viongozi na watumishi wa Wizara na wadau
wengine walio nje ya Wizara.
95.
Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za pekee ziende
kwa Mhe.
Alhaji Juma Suleiman Nkamia (Mb.), Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwangu, Bibi Sihaba Nkinga, Katibu
Mkuu na Prof. Elisante Ole Gabriel,
Naibu Katibu Mkuu. Ninawashukuru kwa uchapakazi wao mahiri na ushirikiano
mkubwa walionipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru
Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo, Watendaji Wakuu wa Asasi, Wataalamu na Watumishi
wote wa Wizara kwa juhudi walizofanya kuhakikisha kwamba tunatimiza ipasavyo
majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa.
96.
Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru Wenyeviti na
wajumbe wa Bodi za Asasi zilizo chini ya Wizara kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa
kushirikiana na Wizara. Asasi hizo zimefanya kazi kwa karibu sana
na mimi na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa ili
kuhakikisha Wizara yetu inafikia malengo yake.
97.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nitumie fursa
hii tena kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo ambao wametuunga mkono wakati
wote wa kutekeleza majukumu ya Wizara.
Shukrani hizi ziwaendee wahisani waliotusaidia, nikitarajia kuwa
wataendelea na moyo huo. Siyo rahisi kuwataja wote lakini nitaje wachache ambao
ni Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Finland, Uingereza, Denmark, Japan, Sweden, Norway,
Iran, Cuba, Ethiopia, New Zealand, Turkey, Korea ya Kusini, Marekani na Ujerumani pamoja na Mashirika ya Kimataifa ya UNESCO, UNICEF, UNFPA, IYF, UNDP, ILO, Forum - SYD, BRAC,
Balton Tanzania Limited, JICA, CYP, ESAMI, RALEIGH INTERNATIONAL, VSO, AMREF,
Restless Development na BRITISH COUNCIL.
98.
Mheshimiwa Spika,
napenda kuvishukuru vyombo vyote vya habari nchini ambavyo vimefanya kazi nzuri ya kuhabarisha,
kuelimisha na kuburudisha umma. Ninaamini kuwa vyombo hivyo vitaendelea na kazi
hiyo kwa kuzingatia maadili na weledi. Aidha, ninamshukuru sana Mpiga Chapa
Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati, bila kuvisahau vituo vya
Televisheni na Redio ambavyo kwa namna ya pekee vinarusha hotuba hii hewani
moja kwa moja.
MAKADIRIO YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
Mapato
99.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara imepanga kukusanya jumla
ya Shilingi 1,149,008,000 kutoka
katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato. Mchanganuo wa makusanyo kifungu kwa kifungu kwa mwaka 2013/2014 na
Makadirio kwa mwaka 2014/2015 upo katika Kiambatisho Na. I.
Matumizi ya
Kawaida
100.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2014/2015 Wizara imetengewa
jumla ya Shilingi 20,371,844,000 kwa
ajili ya Matumizi ya Kawaida (Matumizi Mengineyo na Mishahara), fedha hizo
zinajumuisha:-
(i)
Mishahara ya Wizara Sh. 3,151,654,000
(ii) Mishahara
ya Asasi Sh. 7,849,270,000
(iii) Matumizi
Mengineyo
ya Wizara
- Sh. 5,830,920,000.
(iv)
Matumizi Mengineyo
ya Asasi
Sh. 3,540,000,000.
Mchanganuo wa makadirio ya Matumizi ya Kawaida ya
Wizara na Asasi upo katika Kiambatisho Na. II. Matumizi ya Kawaida kwa Wizara peke yake rejea Kiambatisho Na. III na kwa Asasi rejea Kiambatisho Na. IV.
Miradi ya
Maendeleo
101.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa
fedha 2014/2015 Wizara
imetengewa jumla ya Shilingi
15,000,000,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Mchanganuo
kamili upo katika Kiambatisho
Na. V.
MAOMBI YA FEDHA KWA AJILI YA
KUTEKELEZA MPANGO WA MWAKA 2014/2015.
102.
Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza
majukumu na malengo yake ya mwaka wa fedha 2014/2015, naomba sasa Bunge lako
Tukufu liidhinishe bajeti
ya jumla ya Shilingi 35,371,844,000
ambapo kati ya hizo, fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi 20,371,844,000 na Fedha za
Miradi ya Maendeleo ni Shilingi
15,000,000,000. Mchanganuo wa fedha
hizi upo katika viambatisho vilivyotajwa hapo awali ambavyo ni sehemu ya Hotuba
hii.
103.
Mheshimiwa Spika, napenda nitoe tena shukrani
zangu za dhati kwako binafsi na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba
hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya: www.habari.go.tz na www. tanzaniangovernment.blogspot.com
104.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
Kiambatisho Na. I
MAKUSANYO YA MAPATO MWAKA 2013/2014 NA
MAKADIRIO YA MWAKA 2014/2015 (Sh)
Idara ya
Utawala na Rasilimali Watu
Na
|
Code ya Mapato
|
Maelezo
|
Makisio ya
Mapato 2013/2014
|
Makusanyo
Julai hadi Aprili, 2014
|
Makadirio
ya 2014/2015
|
1.
|
140283
|
Mauzo ya Zabuni
|
200,000
|
-
|
1,000
|
2.
|
140368
|
Mapato kutoka vyanzo mbalimbali
|
1,000
|
-
|
1,000
|
3.
|
140370
|
Marejesho ya fedha za Umma
|
1,000
|
-
|
1,000
|
JUMLA
NDOGO
|
202,000
|
-
|
3,000
|
||
Idara ya
Utamaduni
|
|||||
1.
|
140312
|
Ukaguzi wa filamu
|
10,000,000
|
45,847,725
|
50,000,000
|
2.
|
140370
|
Marejesho ya fedha za Umma
|
-
|
-
|
-
|
3.
|
140368
|
Mapato kutoka vyanzo mbalimbali
|
-
|
-
|
-
|
4.
|
140386
|
Vibali vya kutengeneza filamu
|
243,000,000
|
265,947,894
|
400,000,000
|
JUMLA
NDOGO
|
253,000,000
|
311,795,619
|
450,000,000
|
||
Idara ya
Michezo
|
|||||
1.
|
140259
|
Mapato ya
viwanja vya Michezo (Uhuru na Taifa)
|
550,000,000
|
273,173,300
|
560,000,000
|
2.
|
140315
|
Ada za Mafunzo
|
35,000,000
|
-
|
35,000,000
|
3.
|
140370
|
Mapato kutoka vyanzo mbalimbali
|
-
|
-
|
1,000
|
4
|
140370
|
Marejesho ya fedha za Umma
|
-
|
-
|
1,000
|
JUMLA
NDOGO
|
585,000,000
|
273,170,300
|
595,002,000
|
||
Idara ya
Habari
|
|||||
1.
|
140202
|
Machapisho ya picha, mabango na majarida
|
8,000,000
|
26,470,000
|
35,000,000
|
2.
|
140264
|
Usajili wa magazeti
|
20,000,000
|
15,500,000
|
25,000,000
|
3.
|
140265
|
Ada ya kujiunga
|
-
|
-
|
1,000
|
4.
|
140265
|
Ukumbi wa mikutano
|
10,000,000
|
15,900,000
|
24,000,000
|
5.
|
140310
|
Ada ya mwaka ya Magazeti
|
1,000
|
-
|
1,000
|
6.
|
140368
|
Mapato kutoka vyanzo mbalimbali
|
-
|
-
|
1,000
|
7.
|
140370
|
Marejesho ya fedha za Umma
|
-
|
-
|
1,000
|
8.
|
140387
|
Vitambulisho vya Waandishi wa Habari
|
6,000,000
|
20,193,650
|
20,000,000
|
JUMLA
NDOGO
|
44,001,000
|
78,063,650
|
104,003,000
|
||
JUMLA KUU
|
882,203,000
|
663,029,569
|
1,149,008,000
|
Chanzo: Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo – Kitengo cha Fedha na Uhasibu
Kiambatisho Na. II
MUHTASARI WA BAJETI YA MATUMIZI YA
KAWAIDA 2014/2015 WIZARA NA ASASI
IDARA/KITENGO
|
MAKISIO
2014/2015
|
||
MISHAHARA
(PE)
|
MATUMIZI
MENGINEYO (OC)
|
JUMLA
MATUMIZI YA KAWAIDA (3+4)
|
|
(1)
|
(3)
|
(4)
|
(5)
|
1001 - UTAWALA NA
RASILIMALI WATU
|
1,029,566,000
|
2,974,258,000
|
4,003,824,000
|
1002 –
FEDHA NA UHASIBU
|
164,478,000
|
122,454,000
|
286,932,000
|
1003 –
SERA NA MIPANGO
|
195,889,000
|
299,110,000
|
494,999,000
|
1004
– MAWASILIANO SERIKALINI
|
43,438,000
|
85,022,000
|
128,460,000
|
1005- UNUNUZI NA UGAVI
|
106,055,000
|
116,200,000
|
222,255,000
|
1006- UKAGUZI WA NDANI
|
67,206,000
|
131,294,000
|
198,500,000
|
1007- TEHAMA
|
30,919,000
|
56,500,000
|
87,419,000
|
1008
- SHERIA
|
15,588,000
|
70,000,000
|
85,588,000
|
6001 – MAENDELEO YA
UTAMADUNI
|
2,151,089,000
|
746,888,000
|
2,897,977,000
|
6002 – MAENDELEO YA
VIJANA
|
281,012,000
|
714,222,000
|
995,234,000
|
6004 – MAENDELEO YA
MICHEZO
|
777,723,000
|
2,237,960,000
|
3,015,683,000
|
7003 – HABARI
|
6,137,961,000
|
1,817,012,000
|
7,954,973,000
|
JUMLA KUU
|
11,000,924,000
|
9,370,920,000
|
20,371,844,000
|
Chanzo: Wizara ya Fedha – Januari, 2014
Kiambatisho
Na. III
MUHTASARI WA BAJETI YA MATUMIZI YA
KAWAIDA 2014/2015 – WIZARA
IDARA/KITENGO
|
MAKISIO
2014/2015
|
||
MISHAHARA
(PE)
|
MATUMIZI
MENGINEYO (OC)
|
JUMLA MATUMIZI
YA KAWAIDA (2+3)
|
|
(1)
|
(2)
|
(3)
|
(4)
|
1001- UTAWALA NA RASILIMALI WATU
|
1,029,566,000
|
2,974,258,000
|
4,003,824,000
|
1002 – FEDHA NA UHASIBU
|
164,478,000
|
122,454,000
|
286,932,000
|
1003 – SERA NA MIPANGO
|
195,889,000
|
299,110,000
|
494,999,000
|
1004- MAWASILIANO SERIKALINI
|
43,438,000
|
85,022,000
|
128,460,000
|
1005- UNUNUZI NA UGAVI
|
106,055,000
|
116,200,000
|
222,255,000
|
1006- UKAGUZI WA NDANI
|
67,206,000
|
131,294,000
|
198,500,000
|
1007- TEHAMA
|
30,919,000
|
56,500,000
|
87,419,000
|
1008 - SHERIA
|
15,588,000
|
70,000,000
|
85,588,000
|
6001 –UTAMADUNI
|
342,173,000
|
286,888,000
|
620,061,000
|
6002 - VIJANA
|
281,012,000
|
714,222,000
|
995,234,000
|
6004 – MICHEZO
|
436,107,000
|
657,960,000
|
1,094,067,000
|
7003 – HABARI
|
439,223,000
|
317,012,000
|
756,235,000
|
JUMLA
|
3,151,654,000
|
5,830,920,000
|
8,982,574,000
|
Chanzo: Wizara ya Fedha – Januari, 2014
Kiambatisho
Na. IV
J MUHTASARI WA MATUMIZI YA KAWAIDA
2014/2015 – ASASI
TAASISI/MASHIRIKA
|
MAKISIO
YA 2014/2015
|
||
MISHAHARA
(PE)
|
MATUMIZI
MENGINEYO (OC)
|
JUMLA
MATUMIZI YA KAWAIDA (2+3)
|
|
(1)
|
(2)
|
(3)
|
(4)
|
6001-280514 BODI YA FILAMU.
|
-
|
190,000,000
|
190,000,000
|
6001-
280515
BARAZA LA
SANAA LA TAIFA (BASATA)
|
603,624,000
|
90,000,000
|
693,624,000
|
6001-280516
BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA (BAKITA)
|
537,012,000
|
90,000,000
|
627,012,000
|
MFUKO
WA UTAMADUNI
|
34,200,000
|
-
|
34,200,000
|
280328 – TaSUBa
|
634,080,000
|
90,000,000
|
724,080,000
|
6004 –
280518
BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (BMT)
|
341,616,000
|
90,000,000
|
431,616,000
|
6004 – 280518
BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA (MAKOCHA)
|
-
|
1,230,000,000
|
1,230,000,000
|
6004 – 270380
CHUO CHA MAENDELEO YA
MICHEZO-MALYA
|
-
|
220,000,000
|
220,000,000
|
6004 – 270839
KITUO CHA MICHEZO –ARUSHA
|
-
|
20,000,000
|
20,000,000
|
6004 – 270840
KITUO CHA MICHEZO- SONGEA
|
-
|
20,000,000
|
20,000,000
|
7003 – 280577
SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
|
5,698,738,000
|
1,500,000,000
|
7,198,738,000
|
JUMLA
|
7,849,270,000
|
3,540,000,000
|
11,389,270,000
|
Chanzo: Wizara ya Fedha – Januari, 2014
Kiambatisho Na. V
BAJETI YA MAENDELEO 2014/2015
MRADI
|
MAKADIRIO
YA 2014/2015
|
||
FEDHA ZA
NDANI
|
FEDHA ZA
NJE
|
JUMLA
|
|
1003 –
IDARA YA SERA NA MIPANGO
|
|||
6260- Maendeleo ya Taasisi
|
150,000,000
|
-
|
150,000,000
|
Jumla
|
150,000,000
|
-
|
150,000,000
|
6001 – IDARA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI
|
|||
4353-
Ukarabati wa TaSUBa.
|
450,000,000
|
-
|
450,000,000
|
6343- Ujenzi
wa Ofisi (BAKITA).
|
300,000,000
|
-
|
300,000,000
|
6293- Programu ya Ukombozi wa
Bara la Afrika.
|
250,000,000
|
-
|
250,000,000
|
6355- Ujenzi
wa Ukumbi wa Wazi wa MaonyeSho ya Sanaa.
|
450,000,000
|
-
|
450,000,000
|
6356 - jenzi wa Jumba la Utamaduni.
|
70,000,000
|
-
|
70,000,000
|
Jumla
|
1,520,000,000
|
-
|
1,520,000,000
|
6002 – IDARA YA MAENDELEO YA VIJANA
|
|||
4945
- Mfuko wa Maendeleo
wa Vijana
|
4,000,000,000
|
-
|
4,000,000,000
|
6380 - Ukarabati wa Vituo vya Vijana
|
600,000,000 -
|
-
|
600,000,000 -
|
Jumla
|
4,600,000,000
|
-
|
4,600,000,000
|
6004 – IDARA YA MAENDELEO YA MICHEZO
|
|||
6385 - Ujenzi wa Chuo cha Michezo Malya.
|
500,000,000
|
-
|
500,000,000
|
6523 - Ujenzi wa Eneo Changamani la Michezo.
|
6,780,000,000
|
-
|
6,780,000,000
|
Jumla
|
7,280,000,000
|
-
|
7,280,000,000
|
7003 – IDARA YA HABARI
|
|||
6567 - Habari kwa Umma.
|
450,000,000 -
|
-
|
450,000,000
|
4279
- Upanuzi na Usikivu wa TBC
|
1,000,000,000 -
|
-
|
1,000,000,000
|
Jumla
|
1,500,000,000
|
-
|
1,500,000,000
|
JUMLA KUU
|
15,000,000,000
|
-
|
15,000,000,000
|
Chanzo: Wizara ya Fedha – Januari, 2014
No comments:
Post a Comment