Friday, June 6, 2014

SERIKALI YASHAURI WADAU WA MICHEZO KUJITOKEZA KUSAIDIA MICHEZO NCHINI

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kupokea msaada wa hundi ya milioni kumi kutoka Zantel kwa ajili ya Chama cha Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) leo jijini Dar es Salaaam, kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu Zantel Bw. Pratap Ghose.NGUMI 3Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara (kulia), Afisa Mtendaji Mkuu Zantel Bw. Pratap Ghose (kushoto) pamoja na viongozi kutoka Chama cha Ngumi Tanzania (BFT) wakiunganisha mikono kwa pamoja kuonyesha ushirikiano wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi Milioni kumi kama msaada kutoka Zantel kwa Chama cha Ngumi Tanzania (BFT).NGUMI 4Rais wa Chama cha Ngumi Tanzania Bw. Mutta Rwakatare akitoa shukrani kwa Zantel baada ya kukabidhiwa hundi ya shilingi milioni kumi kuinua mchezo wa ngumi, kushoto ni Katibu Chama cha Ngumi Tanzania Bw. Makole Mashaga na kulia ni Mjumbe wa Maendeleo ya Wanawake Bi. Aisha George Voniatis.
Picha na Genofeva Matemu

…………………………………………………………………
Na: Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini (WHVUM)
Wadau mbalimbali wa michezo nchini wameshauriwa kuwekeza katika vyama vya michezo ili kuinua michezo nchini na kuweza kuleta maendeleo ya kweli katika sekta ya Michezo.
Kauli hiyo imetolea na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara alipokuwa akipokea msaada wa hundi ya milioni kumi kutoka Zantel kwa ajili ya Chama cha Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) leo jijini Dar es Salaaam.
Dkt. Mukangara amesema kuwa sekta ya michezo inahitaji uwekezaji mkubwa hivyo serikali haiwezi kutegemewa katika kufanikisha maendeleo ya michezo bali kuwekeza katika kampuni nyingine kama ilivyo kwa Zantel.
“Kwa hakika Michezo ni sekta inayohitaji uwekezaji mkubwa kama ilivyo katika sekta nyingine yoyote ile ya maendeleo. Bila kuwekeza ipasavyo hatuwezi hata kidogo kupata maendeleo tunayoyatamani kama ilivyo kwa wenzetu waliopiga hatua kubwa katika Michezo duniani” amesema Dkt Mukangara.
Katika kuonyesha kuwa michezo ni afya Dkt. Mukangara alifafanua kuwa umuhimu wa kuwekeza katika Michezo siyo tu katika kushinda mashindano ya kimataifa ua ya ndani bali pia upo katika kutayarisha wachezaji wa kutoka ngazi mbalimbali na kuhakikisha kuwa afya za watu zinakuwa imara na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kulitumikia taifa lao.
Aidha Katibu Mtendaji Baraza la Michezo Tanzania BW. Henry Rihaya amewataka viongozi wa michezo kuwa na maadili mazuri na kusimamia matumizi mazuri ya fedha wanazopata ili kuiwezesha serikali kuwa nao bega kwa bega katika kuleta maendeleo ya michezo nchini.
Naye Rais wa Chama cha Ngumi Tanzania Bw. Mutta Rwakatare amemshukuru Waziri Mukangara pamoja na Zantel kwa ushirikiano waliouonyesha na kuahidi kuitangaza Boxing nchini na nje ya nchi huku wakiendelea kuinua vipaji kwa vijana wadogo katika mchezo wa Boxing.
Zantel imeamua kudhamini Chama cha Netibali, Chama cha Mchezo wa Ngumi za Ridhaa pamoja na Chama cha Mchezo wa Karate katika kufanikisha programme walizojiwekea wakiwa na lengo la kuleta maendeleo ya michezo nchini.

No comments: