MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemtaka mbunge mwenzake, Leticia Nyerere, aache ubunge na akajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuliko kuendelea kukipigia debe chama hicho akiwa upinzani.
Kauli hiyo ameitoa jana alipokuwa akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2014/2015 ambapo alisema matendo anayofanya Leticia ya kujipendekeza kwa CCM yatamgharimu kama ilivyotokea kwa wenzake.
Juzi wakati akichangia bajeti hiyo, Leticia alisema serikali ikifanya vizuri, lazima ipongezwe kwakuwa imepeleka maendeleo katika jimbo analotoka.
“Serikali yangu imefanya mambo mengi, imeniletea maji, walimu katika jimbo langu la Kwimba, ni lazima tuipongeze si
kila wakati tunailaumu humu ndani,” alisema.
Katika mchango wake jana, Mdee, alisema jukumu kubwa la upinzani ni kuikosoa serikali na kuonyesha mbadala katika masuala mbalimbali na si kuisifia kwa kutekeleza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.
“Serikali inapata fedha kutokana na kodi za wananchi, inalazimika kupeleka maji, barabara na huduma mbalimbali kwa lazima si hiyari, tunapoikosoa tunatimiza wajibu wetu kama yenyewe inavyotekeleza inapowahudumia wananchi.
“Leticia Nyerere anaweza kwenda CCM, kwakuwa Rais Kikwete ana nafasi mbili za uteuzi wa wabunge, lakini lazima ajue waliojipendekeza CCM wamepigika sana hivi sasa, aachie ubunge aende huko kwakuwa ana mapenzi nao,” alisema.
Mdee alisema kuwa Leticia anaiaibisha kambi ya upinzani inayofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha serikali inaboresha huduma inazozitoa kwa wananchi.
“Upinzani si lelemama, kama anafikiria CCM ni kuzuri zaidi ni vema akaenda huko kuliko kubakia hapa pasipomfaa,” alisema
No comments:
Post a Comment