WAANDISHI KUNOLEWA VITA DHIDI YA UPANGAJI MATOKEO
Taasisi moja kutoka Uingereza inayohusika na kampeni dhidi ya upangaji matokeo kwenye mpira wa miguu (match fixing) itafanya uwasilishaji (presentation) juu ya suala hilo kwa waandishi wa habari za michezo nchini.
Uwasilishaji huo utafanyika kesho (Julai 5 mwaka huu) saa 11 jioni kwenye hoteli ya Accomondia iliyopo Barabara Nkrumah jijini Dar es Salaam.
Wataalamu hao wa kupiga vita upangaji matokeo ambao pia wataelezea jinsi matokeo yanavyopangwa, jana (Julai 3 mwaka huu) walifanya uwasilishaji wao kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys).
Taasisi hiyo yenye kibali kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) katika utoaji elimu ya kubaini upangaji matokeo, vilevile inatoa elimu juu ya athari zinazopatikana kutokana na upangaji matokeo.
MAFUNZO YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI MBEYA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeendesha mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki kwa wadau wa mpira wa miguu mkoani Mbeya.
Mafunzo hayo yamefanyika jana na leo (Julai 4 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Sokoine, na kushirikisha wasimamizi wa mechi, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na makatibu na maofisa habari wa klabu za Tanzania Prisons na Mbeya City.
Wengine walioshiriki mafunzo hayo ni Meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, wasimamizi wa milangoni (stewards) na waandishi wa habari wa mkoani Mbeya.
Mafunzo hayo yanahitimishwa kesho (Julai 5 mwaka huu) kwa mechi kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City itakayochezwa Uwanja wa Sokoine kuanzia saa 10 kamili jioni. Kiingilio ni sh. 3,000, na tiketi zilianza kuuzwa Julai Mosi mwaka huu kupitia M-Pesa, CRDB Simbanking na maduka ya Fahari Huduma.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment