Tuesday, October 28, 2014

HUYU NDIYE MCHEZAJI BORA WA MWEZI HUU LIGI KUU TANZANIA BARA


Kiungo wa timu ya Azam, Salum Abubakar amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Abubakar ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) aliwashinda wachezaji wengine 20, huku wanne kati ya hao wakichuana naye kwa karibu.

Wachezaji hao ni Joseph Mahundi wa Coastal Union, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar) na Najim Magulu wa JKT Ruvu Stars.

Kwa kuibuka mchezaji bora, Abubakar atazawadiwa kikombe na fedha taslimu sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.



No comments: