Tuesday, October 21, 2014

RAIS KIKWETE YUPO CHINA KWA SIKU SITA

1a
2a
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe
Raymond Mushi wakati akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo tayari kuanza
 ziara rasmi ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko
wa Rais Xi Jinping.
3a
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagwa na maafisa wa Ubalozi wa China
nchini Tanzanioa  wakati akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo tayari
kuanza  ziara rasmi ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa
mwaliko wa Rais Xi Jinping.

PICHA NA IKULU
………………………………………………………………………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete leo, Jumanne, Oktoba 21, 2014, anaanza ziara rasmi ya siku
sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping,
ikiwa ni ziara yake ya pili nchini humo akiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano.
Baada ya China, Rais Kikwete atafanya ziara rasmi ya siku tatu nchini
Vietnam kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo.
Wakati wa ziara yake nchini China, Rais Kikwete ambaye aliondoka
nchini usiku wa jana, Jumatatu, Oktoba 20, 2014, atatembelea majimbo
matatu ya nchi hiyo, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa China,
atashuhudia utiaji saini mikataba muhimu ya shughuli za maendeleo,
atatunukiwa shahada za heshima na atashiriki katika sherehe za miaka
50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na
China.
Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji
wake, Rais Xi Jinping; Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang pamoja na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Zhang Dejiang.
Rais Kikwete pia atashuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya
maendeleo ya Tanzania ambayo inasaidiwa ama inagharimiwa na fedha
kutoka China na pia atakutana kwa mazungumzo na wakuu wa taasisi
muhimu zinazogharimia baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo katika
Tanzania zikiwamo China-Africa Development Fund (CADB) na China
Development Bank (CDB).
Akiwa Beijing, Rais Kikwete atakutana na Mabalozi wa Afrika
wanaoziwakilisha nchi zao katika China, atafungua Mkutano wa Tatu wa
Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na China na atazindua rasmi
Kijiji cha Kiafrika.
Aidha, Rais Kikwete atatunukiwa uprofesa wa heshima na Chuo Kikuu cha
Kilimo cha China cha China Agricultural University na Chuo Kikuu cha
East China Normal University na pia atakuwa mwenyeji wa hafla maalum
ya kusherehekea miaka 50 ya uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na
China. Uhusiano huo ulitimiza miaka 50, Aprili 26, mwaka huu, siku
ambako Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ilitimiza miaka 50 ya
kuzaliwa kwake.
Baada ya kumaliza ziara yake Beijing, Rais Kikwete atatembelea Jimbo
la Jinan ambako atashuhudia maonyesho rasmi ya kijeshi ya Jeshi la
Ukombozi la Wananchi wa China la Chinese People’s Liberation Army
(PLA) lililoandaliwa rasmi kwa heshima yake. Hiyo itakuwa mara ya
kwanza katika historia kwa heshima ya namna hiyo kutolewa kwa kiongozi
wa nchi yoyote duniani, nje ya China.
Akiwa Jimbo la Jinan, Rais Kikwete pia atakutana na viongozi wa Jimbo
hilo na pia atakutana kwa mazungumzo na madaktari wa Kichina ambao
wamefanya kazi katika Tanzania katika miaka 50 iliyopita.
Baada ya Jimbo la Jinan, Rais Kikwete atakwenda  Jimbo la Shenzhen
ambako atatembelea makao makuu ya taasisi na makampuni makubwa ya
China ya Shenzhen Economic Zones Authority, China Merchants Holdings
International (CMHI), Huawei na ZTE. Shenzhen ndiko Watanzania wengi
wanaonunua bidhaa kutoka China hufanyia biashara zao.
Mara ya mwisho, Rais Kikwete alitembelea China mwaka 2008 wakati
alipoliwakilisha Bara la Afrika katika Mkutano wa Kwanza wa
China-Afrika katika nafasi yake wakati huo kama Mwenyekiti wa Umoja wa
Afrika (AU).
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Oktoba,2014

No comments: