Tuesday, December 16, 2014

HALI HALISI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA TANZANIA NDIO HII

Wafuasi wa Chadema mjini Nansio Wilaya ya Ukerewe, Mwanza wakishangilia ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi.  
Dar/Mikoani. Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi, yanaonyesha kuimarika kwa upinzani nchini baada ya kupata viti vingi vya uenyekiti wa mitaa na vijiji, pamoja na mamia ya wajumbe wa Serikali husika.
Hayo yanaonyesha kuwa vyama hivyo vimeanza kuimarika katika ngazi za chini, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2009, katika uchaguzi ambao CCM kilipata ushindi wa kishindo wa asilimia 91.72, huku wapinzani wakigawana asilimia 8.28 zilizobaki.
Licha ya uchaguzi wa juzi kugubikwa na kasoro lukuki, upinzani umeonekana kuchomoza huku katika baadhi ya mikoa ukipata ushindi maradufu hasa katika ile ambayo una nguvu kubwa wakati katika maeneo ambayo ulikuwa na viti vichache au kutokuwa navyo kabisa, umeibuka na kuipokonya CCM baadhi ya mitaa na vijiji.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa); Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimejizolea viti vingi tofauti na awali, huku chama kipya cha ACT kikichomoza na kupata ushindi katika maeneo kadhaa ya mikoa ya Kigoma na Katavi.
Mikoa ambayo upinzani umeonekana kuzoa viti vingi ni Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Kigoma, Mara, Kagera na Dar es Salaam, hali ambayo wachunguzi wa mambo wameielezea kuwa siyo dalili njema kwa CCM.
Nguvu ya upinzani inaonekana kuongezeka siku hadi siku ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 1995 wakati ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa.
Hii ni mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani kuonyesha ushindani mkubwa katika uchaguzi wa chini, hali ambayo inaweza kuwa ni jibu la ukosoaji ambao umekuwa ukifanywa kwamba vyama hivyo vimejikita mjini tu na kusahau kufanya siasa kwa wananchi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Iringa, Profesa Gaundence Mpangala alisema matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa, yanadhihirisha kuwa CCM itaendelea kukabiliwa na upinzani mkubwa hata kwa Uchaguzi Mkuu ujao mwakani.
Licha ya mafanikio hayo, kwa upande wa upinzani, matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa bado CCM inaelekea kushinda kwa kupata mitaa na vijiji vingi ikilinganishwa na upinzani.
CCM kinaendelea kuweka mizizi katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Dodoma, Pwani na baadhi ya wilaya katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Mwanza.

Nguvu ya upinzani

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Chadema kinaongoza upinzani kwa kupata viti vingi mfano halisi ukiwa mkoani Mbeya ambako kimeshinda viti 74 ikilinganishwa na viti tisa kilivyopata katika uchaguzi wa 2009.
Mkoani Arusha, chama hicho kimeshinda viti 75, kutoka saba kilivyopata katika uchaguzi uliopita, wakati katika Manispaa ya Shinyanga kimeibuka kidedea baada ya kujizolea mitaa 29. CCM ikiambulia mitaa 26.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Rashid Juma Idd alisema jana kuwa katika uchaguzi huo, licha ya Chadema kupata vivi hivyo 75, CCM kilipita bila kupingwa katika mitaa sita na kufanya kiwe na viti vya wenyeviti 78 hadi jana.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na kwamba katika maeneo mbalimbali, kura zimezidi watu waliojiandikisha.
Lema alisema katika moja ya vituo Kata ya Unga Ltd wapigakura walikuwa 800 lakini kura zimezidi na kufikia 1,200. Alisema kwa ujumla, Chadema kinaamini kwamba kimeshinda viti 104 kwani kuna mitaa ambayo wajumbe wote wa Serikali na viti maalumu wanatoka chama hicho na wenyeviti pekee ndiyo wanaotoka CCM.
Chadema pia kimefanya vizuri katika Mji wa Kahama ambako Mkurugenzi Mtendaji wake alisema kimeshinda katika mitaa 18 kati ya 32 wakati CCM kilishinda mitaa 14.
Katika Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, CCM kimeshinda mitaa 35 na upinzani viti 31. Katibu Msaidizi wa CCM, Abdul Kambuga alisema chama chake hakikufanya vizuri katika uchaguzi huo na kuwa ilihujumiwa wakati wa maandalizi ya kupiga kura.
Mwenyekiti wa Chadema katika Manispaa hiyo, Victor Sherejei alisema ushindi huo mkubwa kwa upinzani unatoa somo kuwa wananchi wamekata tamaa baada ya kusubiri mabadiliko kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, CUF kimeviongoza vyama vya upinzani kuikaba koo CCM katika Manispaa ya Mtwara (Mikindani) ambako vyama hivyo vimepata viti 53 na kubakiza 58 mikononi mwa chama tawala. CUF kimeshinda mitaa 36, Chadema mitaa 16, NCCR Mageuzi minne na TLP mmoja.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wameonekana kufurahia matokeo hayo na kwamba kama si kasoro ambazo wanadai kwamba zilipangwa na chama tawala, yangekuwa mazuri zaidi.
“Licha ya vikwazo vilivyolenga kuhujumu upinzani, Ukawa imepata mafanikio makubwa,” alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu alisifu kile alichokiita mafanikio hayo ya upinzani katika uchaguzi huo. “Hii inaonyesha tumefanikiwa kulingana na tulikotoka ambako CCM ilikuwa inashinda kwa asilimia 96 na wapinzani kugawana asilimia 4 tu,” alisema.

Kasoro ambazo ziliathiri uchaguzi huo ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kupigia kura, vituo kuchelewa kuanza kazi, wizi wa karatasi za kupigia kura, wapiga kura kukuta majina yao yameshatumika kupiga kura, wananchi kuzuiwa na wengine kutokuta majina yao kwenye vituo vya kupigia kura.
Kadhalika, kulikuwa na matukio yaliyoashiria kuvunjika kwa amani yakiwamo wananchi kupigana, polisi kurusha risasi na mabomu ya machozi na tukio la uchomaji wa ofisi ya mtendaji katika moja ya Kata za Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa.
Kutokana na kasoro hizo, uchaguzi uliahirishwa katika maeneo kadhaa na umepangwa kufanyika kati ya kesho na Jumapili ijayo.
Hali halisi
Msimamizi wa Uchaguzi katika Jiji la Mbeya, Musa Zungiza alisema CCM hadi jana ilikuwa imepata mitaa 103, Chadema 74 na NCCR-Mageuzi ilipata mitaa miwili. Mitaa miwili ya Kata za Itiji na Mwansekwa, ilitarajia kurudia uchaguzi.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kata ya Igurusi CCM imeshinda vijiji saba, Chadema viwili na katika Wilaya ya Rungwe, Kata ya Kiwira yenye vijiji vitano, Chadema imeshinda vitatu CCM viwili. Chadema pia imeshinda viti vitatu katika Kata ya Ndato yenye vijiji vinne na CCM ina kijiji kimoja.
Vijiji sita vya Kata ya Isongole vimechukuliwa na CCM pamoja na vijiji vingine vitano vya Kata ya Suma, huku wapinzani wakiambulia patupu. Kata ya Kyimo yenye vijiji vitano, Chadema imeshinda vitatu na CCM viwili.
Matokeo Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Kata ya Maendeleo yenye vijiji vitano CCM, imeshinda vinne na Chadema kimoja, wakati katika Wilaya Ileje CCM imeshinda vijiji sita vya Kata ya Ikunga, Chadema imeambulia viti viwili.
Imeandikwa na Mussa Juma, Lauden Mwambona, Amanyisye Ambindwile, Bakari Kiango, Justa Musa, Godfrey Kahango, Albert Msole, Phinias Bashaya, Suzy Butondo, Haika Kimaro.

No comments: