Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa
habari,leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar
es Salaam, kutoa tathmini ya matokeo ya awali uchaguzi wa Serikali za
mitaa uliofanyika juzi nchini kote.
Baadhi ya Wanahabari Wakimsikiliza Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa
habari,leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar
es Salaam, kutoa tathmini ya matokeo ya awali uchaguzi wa Serikali za
mitaa uliofanyika juzi nchini kote.
======= ===== =======
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka watendaji wote waliosababisha kuharibika
kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika baadhi ya maeneo nchini
wachukuliwe hatua kali.
Kimesema, watendaji hao wanastahili
kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kilichotokea ni uzembe wa hali ya juu
uliofanyika huku ikifahamika wazi kwamba tukio la uchaguzi huo ni kubwa
na muhimu sana kwa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,
katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam,
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (pichani) amesema,
kulingana na kosa lililojitokeza kuwa la wazi hakuna haja ya kupoteza
fedha na muda kufanya uchunguzi kabla ya kuwachukulia hatua waliohusika.
"Kwa
mfano, Mkurugenzi wa Halmashauri ana kila kitu na alijua mapema kuwa
uchaguzi utafanyika lini kwa kuwa halikuwa jambo la dharura, inakuwaje
anaruhusu karatasi ziende kwenye vituo zikiwa zimechapishwa hovyo au
mahali pengine vifaa viwe vichache?" alihoji Nape na kuongeza "Sasa hapa
unahitajika uchunguzi gani tena kubaini aliyevurunda?".
"Mahali
pengine zimefika karatasi za kupigia kura jina la mgombea wa CCM nembo
ya CUF, au mgombea wa CUF nembo ya CCM! huu ni uzembe wa hali ya juu
sana na adhabu yake haistahili kusubiri uchunguzi", alisema Nape.
Akizungumzia
matokeo ya awali ya Uchaguzi huo, Nape alisema licha ya vyama vya
upinzani kuwa na umri wa miaka 22 sasa, huku vikifanya harakati za
kujaribu kuungana katika umoja wanaouita Ukawa, bado CCM imewagaragaraza
vibaya.
Nape amesema, katika uchaguzi huo, CCM imepata zaidi ya
asilimia 80 ya ushindi kwa nchi nzima, huku Dar es Salaam, ikiwa na
asilimia zaidi ya 70 licha ya kwamba Chadema wanao wabunge wawili katika
mkoa huo.
"Katika mazingira ya sasa ambayo vyama vya upinzani
vina miaka 22, na vinafanya hata harakati za kujaribu kuungana, asilimia
80 si ndogo kwa CCM, na tunaamini huu ni mwanzo mzuri, na hatuoni namna
ambavyo asilimia hii itabadilika katika uchaguzi mkuu mwakani, maana
uchaguzi huu ni kama kura za maoni", alisema Nape.
"Wanaosema,
asilimia ya CCM imeshuka, wajue kwamba tuliposema tunataka mfumo wa
vyama vingi maana yake tulitaka ushindani katika demokrasia, katika
demokrasia ya ushindani ni vema kuruhusu vyama vya upinzani vikakua ili
ushindani huo uonekane", alisema Nape nakuongeza.
"Hata hivyo
inasikitisha kwamba licha ya vyama vya upinzani kuwa na umri wa miakaa
22 sasa, bado havijaweza kujenga imani ya kutosha kwa Watanzania kuwa
vinaweza kuongoza, lazima wapinzania wazidi kujijenga ili Watanzania
wawaamini, asilimia hii 14 waliyopata karika uchaguzi huu wa serikali za
mitaa bado ni ndogo sana kwa uhai wa miaka hiyo".
Amesema,
asilimia iliyopata CCM wakati matokeo mengine yakisubiriwa ambako
uchaguzi uliahirishwa, ni dalili za wazi kwamba, Ukawa bado ni muungano
wa mashaka kwa sababu kama wangeungana na kuachiana maeneo ni kweli
wangeweza kufika mbali.
"Hebu jiulizeni na ninyi, kama kweli
UKawa ulitumika vema, ni kwa nini kwenye karatasi za matokeo ya uchaguzi
huu, kila chama kina mtu wake na idadi ya kura alizopata? Kwa nini
zisiwe za mgombea mmoja wapo wa Ukawa?... Hii inamaanisha ndoa hii ya
ukawa bado sana", alisema Nape.
Nape aliwashukuru wananchi nchini
kote kwa kuendelea kuiamini CCM, na kuchagua wagombea wake, huku
akivipongeza vyama vya upinzani kwa maeneo waliyochaguliwa, akiwataka
kuchapa kazi vinginevyo siku za baadaye wananchi watawahukumu kwa
kuwatosa.
No comments:
Post a Comment