Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na
Polisi Mkoa wa Pwani linaendesha oparesheni kali ya aina yake ya kuwasaka watu
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliowavamia, kuwauwa askari wawili na
kumjeruhi mmoja na kisha kupora bunduki aina ya SMG.
Tukio hilo limetokea tarehe 30/03/2015 majira ya saa mbili usiku huko
barabara ya Kilwa Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani. Katika
tukio hilo majambazi wapatao 8 hadi 10 wakiwa na mapanga na silaha zingine
waliwavamia ghafla askari watatu waliokuwa kazini katika eneo la kizuizi cha
Polisi kilichopo kijiji cha Kipara mpakani Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga
Mkoa wa Pwani. Majambazi hao wakiwashambulia ghafla askari hao kisha kupora
silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 30 ndani ya magazine na kutokomea
kusikojulikana.
Majina ya askari wa Wilala ya Kipolisi ya Mbagala waliouawa ni kama
ifuatavyo:
1. D.2865 SGT FRANCIS,
2. E.177 CPL MICHAEL,
Askari mwingine mwenye namba D.5573 D/SGT ALLY amejeruhiwa kwa risasi
kwenye paja la mguu wa kushoto na amelazwa katika hospitali ya Temeke kwa
matibabu. Askari huyu kabla ya kujeruhiwa alipambana vikali na majambazi hayo
kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo aina ya SMG ambayo pia walishindwa kumpora
hivyo wakatokomea kuelekea pori la vikindu.
Katika oparesheni hiyo, nguvu na mbinu zote za kipolisi zitatumuika
ambapo vikosi vya Dar es Salaam na Pwani vilianza kufanya oparesheni hiyo mara
baada ya tukio ili kuhakikisha kwamba majambazi hao wanapatikana haraka
iwezekanavyo.
Pamoja na oparesheni hiyo kali inayoendelea, Jeshi la Polisi
linachunguza ili kubaini kama tukio hili linaashilia vitendo vya ugaidi au ni ujambazi wa kutumia silaha.
Natoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kupitia (dhana
ya polisi jamii) kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa hali na mali kwa kutoa
taarifa sahihi.
Matukio haya ambayo yamekuwa yakitokea mkoa wa Pwani mara kwa mara ni
lazima yakomeshwe ili kuhakikisha kwamba havijirudii.
No comments:
Post a Comment