Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA SC imezidi kujisogeza karibu na taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 43, baada ya kucheza mechi 20- ikifuatiwa na Azam FC, ambayo baada ya sare ya 1-1 na Mbeya City leo, inafikisha pointi 37, baada ya mechi 19.
Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sean Sherman ‘amefuta mkosi’ leo, akifunga bao moja na kutoa pasi za mabao matatu- wakati Mrundi Amisi Tambwe amepiga ‘hat trick’.
Amisi Tambwe aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya tisa, akimalizia pasi ya Sherman, baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Oscar Joshua.
Dakika ya 34, Tambwe akaifungia Yanga SC bao la tatu akimalizia pasi ya Juma Abdul. Tambwe tena akafunga bao lake la tatu katika mchezo wa leo na la nne kwa Yanga dakika ya 48, akimalizia pasi ya Sherman.
Sherman akaifungia Yanga SC bao la tano dakika ya 50 akimalizia pasi ya Tambwe. Mliberia huyo alimwaga machozi baada ya kufunga bao hilo na Mbuyu Twite akaenda kukipangusa kiatu chake kwa jezi yake.
Msuva akaifungia Yanga SC bao la sita dakika ya 87 akimalizia pasi ya kichwa ya Tambwe. Msuva sasa ana mabao 13 katika Ligi Kuu akiwa anaongoza katika mbio za ufungaji bora, akifuatiwa na Didier kabumbangu wa Azam FC na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar, wote wana mabao 10 kila moja.
Salum Telela akaifungia Yanga SC bao la saba dakika ya 88 kwa shuti kali akimalizia pasi ya Msuva, kabla ya Tambwe kufunga la nane dakika ya 90.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Edward Charles dk77, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite/Hassan Dilunga dk67, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Kpah Sherman/Nizar Khalfan dk70 na Simon Msuva.
Coastal Union; Bakari Fikirini, Juma Hamad, Abdallah Mfuko, Yussuf Chuma, Bakari Mtama, Abdulhalim Humud, Mohamed Ally, Yahya Ayoub, Rajab Mohamed/Mohammed Shekuwe dk57, Ike Bright Obinna/Mohamed Mtindi dk64 na Rama Salim/Abbas Athuman dk46.
MABINGWA watetezi, Azam FC wamekwaa kisiki nyumbani, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Matokeo hayo yanawafanya Azam FC sasa wawe wanazidiwa pointi sita na vinara, Yanga SC wenye pointi 43 baada ya ushindi wa 8-0 dhidi ya Coastal Union leo. Azam FC walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Kipre Michael Balou dakika ya 61 kwa shuti la umbali wa zaidi ya mita 25. Haikuchukua muda mrefu, Mbeya City wakasawazisha kupitia kwa Raphael Alpha kwa penalti dakika ya 64, kufuatia Erasto Nyoni kumuangusha Deus Kaseke. Baafa ya hapo, timu hizo zilishambuliana kwa zamani na kipyenga cha mwisho, hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao zaidi. Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Serge Wawa, Mudathir Yahaya, Himid Mao, Kipre Bolou/Gaudence Mwaikimba dk80, Frank Domayo/Amri Kiemba dk56, John Bocco na Brian Majwega/Farid Mussa dk74. Mbeya City; Hannington Kalyesebula, Peter Richard, Hassan Mwasapili, Juma Nyosso, Christian Sembuli, Kenny Ally, Deus Kaseke/Hamad Kibopile dk84, Paul Nonga/Peter Mapunda dk70, Raphael Alpha, Themi Felix na Peter Mwilanzi. |
No comments:
Post a Comment