Tuesday, June 2, 2015

CHADEMA WAMLILIA MBUNGE MWAIPOSA WA UKONGA ALIYEFARIKI LEO

SALAAM ZA POLE NA RAMBIRAMBI MSIBA WAEUGENE MWAIPOSA (MB)

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibroad Slaa ametuma salaam za pole kwa familia, ndugu, jamaa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa msiba wa Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa aliyefariki akiwa mjini Dodoma alikokuwa akiendelea kuhudhuria vikao vya Bunge.


Katibu Mkuu Dk. Slaa ambaye amepata taarifa za msiba huo akiwa njiani kwenda mkoani Katavi akiendelea na ziara ya kikazi akiwa ametokea mikoa ya Mbeya na Rukwa, amesema;
"Nimestushwa na kusikitishwa sana na taarifa ya kifo cha ghafla cha Mhe. Eugene Mwaiposa, Mbunge wa CCM Jimbo la Ukonga kilichotokea akiwa Dodoma."
"Ni kweli Mwenyezi Mungu anafanya kazi zake na kumleta duniani binadamu na au kumchukua kwa namna, wakati na au njia anayotaka yeye, lakini anapomchukua ghafla inaleta simanzi kubwa."
"Tunatoa pole za dhati kwa familia, ndugu na jamaa wa Mwaiposa kwa kuondokewa na mpendwa wao. Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa uvumilivu katika wakati huu wa mgumu na majaribu kwa majonzi ya kuondokewa na mwanafamilia na mpendwa wao," amesema Katibu Mkuu.
Aidha Dk. Slaa ametoa salaam za pole kwa wananchi wa Ukonga kwa kumpoteza mbunge wao aliyekuwa bungeni Dodoma akiwawakilisha.
Salaam hizo za pole alizozitoa leo pia amezielekeza kwa uongozi wa Bunge na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpoteza mbunge mwenzao wakati huu ambapo walikuwa pamoja kwenye vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.
Halikadhalika Katibu Mkuu ametuma salaam kwa wanachama wa CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, kwa kumpoteza mmoja wa wanachama mwenzao.
"Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, na awatie moyo wa ustahimilivu wote walioguswa na msiba huu mzito," amesema Katibu Mkuu Dk. Slaa katika salaam hizo za pole kufuatia taarifa za msiba huo wa Mbunge Mwaiposa uliotokea usiku wa kuamkia leo Jumanne, akiwa usingizini kwa matatizo ya shinikizo la damu.
Imetolewa leo Jumanne; Juni 2, 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano-CHADEMA

No comments: