Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 ambao umepanda hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 kwa mwezi Septemba, 2015.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 ambao umepanda hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 kwa mwezi Septemba, 2015. Kulia kwake ni Mtakwimu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Muhdin Mtindo. (PICHA NA VERONICA KAZIMOTO)
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam.
MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii,Ephraim Kwesigabo amesema kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kumesababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma zingine za kijamii ikiwemo chakula na nishati.
“Kupanda kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2015 kumechangiwa na ongezeko la bei za vyakula kama vile Mchele ambao umeongezeka bei kwa asilimia 0.8, unga wa muhogo umeongezeka hadi asilimia 0.7, nyama kwa asilimia 0.8, samaki kwa asilimia 5.5, ndizi za kupika asilimia 0.7 na choroko kwa asilimia 0.9”, amesema Kwesigabo.
Bidhaa zisizokuwa za vyakula kama vile vitambaa kwa ajili ya nguo za kike zimepanda kwa asilimia 1.6, viatu vya kiume asilimia 1.1, mkaa asilimia 1.4 na gharama za kupata ushauri kwa daktari pia zimepanda hadi kufikia asilimia 1.4.
Kwa upande Mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.1 ambao ni ongezeko sawa na mwezi Septemba, 2015. Fahirisi za bei pia zimeongezeka kutoka 159.04 hadi kufikia 159.17 kwa mwezi Oktoba, 2015.
“Fahirisi za bei za vyakula vya nyumbani na migahawani iliongezeka kidogo hadi kufikia asilimia 10.0 kutoka asilimia 9.4 kwa mwezi Septemba, 2015 ambapo bidhaa zisizokuwa za vyakula zimepungua kidogo kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 1.7 kwa mwezi Oktoba, 2015,” amefafanua Kwesigabo.
Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Oktoba, 2015 umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.2 kwa mwezi Septemba, 2015.
No comments:
Post a Comment