Wednesday, November 4, 2015

Rais MKAPA ni mzima wa Afya


Na Georgina


Misama-MAELEZO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari
Bw. Assah Mwambene amekanusha taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye baadhi ya
vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Rais mstaafu wa
Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa.

Akiongea katika mkutano
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Bw. Mwambene amesema kuwa Mhe.
Rais Mkapa ni mzima na mwenye afya nzuri 
 anaendelea na shughuli zake kila
siku kama kawaida.


“Mhe. Rais Benjamin
William Mkapa ni mzima hajafariki, wala haumwi na si jambo jema kumzushia tukio
hilo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na nawasihi msiendelee kusambaza
ujumbe huo” alisisitiza Mwambene.

Aidha, katika mkutano
huo Mwambene aliwashukuru wahariri, waandishi wa vyombo vyote vya habari na
mitandao ya kijamii kwa ujumla kwa kuonyesha moyo wa uzalendo katika kipindi
chote ambacho Taifa limekuwa katika mchakato wa uchaguzi na mpaka sasa ambapo
serikali inaendelea na maandalizi ya sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Awamu
ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Mwambene amesema mpaka
sasa maandalizi ya sherehe hizo yanaendelea vizuri, zaidi ya Marais 15 kutoka
nchi mbalimbali wamealikwa baadhi wameshawasili nchini na wengine wanaendelea
kuwasili.

Sherehe za kuapishwa
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Tano zitafanyika kesho
tarehe Novemba, 5 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru.

No comments: