Wananchi
wanaumizwa na mgogoro Zanzibar
CHAMA cha ACT-Wazalendo
kinasikitishwa na hali ngumu ya maisha inayowakumba wananchi wa Zanzibar
kutokana na mkwamo wa kisiasa unaoendelea visiwani humo.
Wakati wa mkutano wa
tathmini ya hali ya kisiasa ya Zanzibar uliofanyika Unguja kati ya Desemba 19
na 20 mwaka huu, viongozi wa ACT-Wazalendo walipokea taarifa kutoka kwa
wananchi wa kawaida kuhusu nini hasa kinaendelea.
Bei za vyakula na
huduma nyingine zimepanda kwa kiwango cha kutisha. Sekta ya utalii ambayo ni
muhimu kwa uchumi wa Zanzibar imeathirika kiasi kwamba ziko hoteli ambazo
zimepokea nusu tu ya idadi ya watalii zilizotarajiwa kuwapata kipindi hiki cha
mwishoni mwa mwaka.
Athari hii ya kutokuja
kwa watalii haiwagusi wamiliki wa hoteli pekee, kwani ujio wa wageni husaidia
kuchagiza biashara nyingine mbalimbali za wenyeji zikiwamo za waongoza watalii,
wauza bidhaa pendwa, wasafirishaji na kada nyingine katika mnyororo wa biashara
ya utalii.
Ili kupata picha halisi
ya nini kinaendelea Zanzibar, ni vema tukawapa takwimu kwa mujibu wa Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar. Mfumuko wa bei wa Zanzibar, hivi sasa umefikia
kiwango cha asilimia 11 ambacho hakijawahi kufikiwa katika miaka ya karibuni.
Bei za bidhaa hususani
vyakula zimepanda kwa kiwango cha asilimia 16.4, huku vyakula vya baharini, kwa
mfano samaki, mfumuko wake wa bei umefikia kiwango cha takribani asilimia 30,Kwa
kulinganisha, mfumuko wa bei kwa Tanzania ni asilimia 6.6 kwa mujibu wa taarifa
ya mwezi uliopita ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Huu ni ushahidi wa wazi kwamba mkwamo huu wa
kisiasa umeanza kuwaumiza wananchi wasio na hatia.
ACT-Wazalendo inasema
kwamba hali hii ya kuumiza wananchi wa kawaida haikubaliki na ni LAZIMA ifikie
ukomo haraka iwezekanavyo. Hatuwezi kuumiza wananchi wetu kwa sababu zisizo na
maana.
Ili kuwaokoa wananchi
na maumivu haya, Kamati ya Uongozi ya ACT-Wazalendo imekaa na kutafakari suala
hili la Zanzibar na hivyo inapendekeza yafuatayo;
Mosi,
Mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu atangazwe
haraka ili hali ya utulivu wa kawaida irejee.
Pili,
ACT-Wazalendo imebaini kuwapo kwa idadi kubwa isivyo kawaida ya wanajeshi
wanaolinda Bandari, Uwanja wa Ndege, Vituo vya Redio na maeneo mengine muhimu.
Chama
chetu kinataka askari hao warejee makambini kwao kwani uwepo wao katika maeneo
ya kiraia unasababisha hali ya shaka na hofu miongoni mwa wananchi.
Tatu, kwa ajili ya
mustakabali mwema wa Zanzibar, ACT-Wazalendo kinataka mazungumzo yoyote kuhusu
uchaguzi uliofutwa yahusishe wadau wa vyama na taasisi nyingine walioshiriki
kwenye uchaguzi.
Hii si mara ya kwanza
kwa viongozi wa vyama vya CCM na CUF kukutana na kufanya mazungumzo baada ya
kutokea matatizo. Lakini uzoefu unaonyesha kwamba suluhisho huwa si la kudumu
na badala yake matatizo yaleyale hujirudia baada ya muda.
Suluhisho la hali hii
ni vyama vingine vyote, kujumuishwa katika aina hii ya mazungumzo ili kupata
mawazo jumuishi na yatakayowakilisha sehemu kubwa zaidi ya Wazanzibari ambao
wengi wao, hasa kizazi kipya, hawana uhusiano wowote na vyama hivyo viwili.
Kwa
ujumla hali ya kisiasa Zanzibar ni mbaya sana na inatisha kwani wananchi
wanaishi kwa hofu kubwa na hawaelewi kinachoendelea, ukimya uliotamalaki hauashirii
hatima njema ya siasa za Zanzibar.
ACT-Wazalendo kinapenda
kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa subira
na uvumilivu wa kiwango cha juu waliouonyesha katika kipindi hiki cha hali ya
sintofahamu.
Imetolewa na
Zitto Kabwe
Kiongozi Mkuu wa chama
No comments:
Post a Comment