| Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhuru Publisher, Theophil Makunga ambaye ndiye mwenyekiti mpya wa TEF |
Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kama mmoja wa wadau wa habari na vyombo vya habari, kupitia
Idara ya Habari na Mawasiliano kinatoa pongezi za dhati kwa uongozi mpya wa
Jukwaa la Wahariri (TEF) uliochaguliwa mwishoni mwa juma lililopita katika
Mkutano Mkuu wa TEF ambao hufanyika kila baada ya miaka 4.
Kupitia taarifa hii
tunautakia kila la heri katika kutimiza majukumu yake uongozi huo ambao unahusisha
waandishi waandamizi nchini, Teophil Makunga akiwa Mwenyekiti wa jukwaa,
akisaidiana na viongozi wengine ambao ni; Deodatus Balile (Makamu Mwenyekiti),
Neville Meena (Katibu), Neng’inda Johanes (Katibu Msaidizi), huku Wajumbe wa
Bodi wakiwa ni Bakari Machumu, Lilian Timbuka, Joyce Shebe, Salim Said Salim na
Jesse Kwayu.
Tukiwa taasisi pekee ya
kisiasa ambayo imetia saini Azimio la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri na
Uwajibikaji (DEFIR), tunawiwa kuwajibika kuwapatia ushirikiano wetu katika
kutimiza majukumu yao ya kikazi na kitaaluma kadri tunavyoweza, tukiongozwa na
dhamira ya kuhakikisha tasnia ya habari inaendelea kuwa mhimili imara na huru
kuitumikia jamii ya Watanzania isiyokuwa na sauti ambayo inahitaji sauti ya
vyombo vya habari.
Uongozi huo mpya umechaguliwa
katika kipindi ambacho mazingira ya utendaji kazi wa vyombo vya habari na
wanahabari hata ya kitaaluma pia, yanazidi kuwa magumu kutokana na kutungwa kwa
sheria zingine hatari zinazowasaidia watawala wa sasa kuminya uhuru wa habari
na upatikanaji wa taarifa, kuliko hata ilivyokuwa wakati wa ukoloni,
wakiongezea kwenye sheria mbovu zilizokuwepo.
Ni rai yetu kuwa uongozi huo
wa TEF ambao unaundwa na waandishi waandamizi, utaifanyia kazi changamoto nyingine
‘mpya’ ambayo inatokana na watawala kubadili mbinu za kutisha vyombo vya habari
nchini ambapo sasa wameamua kwenda hatua ya KUFUTA chombo cha habari, tofauti
na huko nyuma ambako walikuwa wanafungia chombo cha habari kwa muda fulani
unaojulikana au usiojulikana.
Huo ni udikteta mkubwa ambao
haukutarajiwa kutokea katika zama hizi ambazo uhuru wa habari na upatikanaji wa
taarifa si tu umesaidia uwajibikaji kuwa nguzo ya ustawi katika jamii za nchi
zilizoendelea lakini pia umekuwa kichocheo cha fikra zenye uwezo wa kuzalisha,
kutafuta na kusambaza taarifa na maarifa kwa ajili ya maendeleo makubwa zaidi.
Uongozi huo mpya umebeba
sehemu ya matumaini ya Watanzania ambao wangependa kuona nchi hii inaondokana
na sheria za ‘kijima’ ambazo badala ya kuwahamasisha watu kuwa watafutaji, wasambazaji
na walaji wa habari na taarifa, zinawafanya wawe waoga hata wa kusoma na
kutumia teknolojia ya mawasiliano kupata habari.
Tukiwa sehemu ya wadau wa
habari na vyombo vya habari nchini na nje ya nchi, tunaamini kuwa uongozi mpya
wa TEF utaendeleza mazuri yaliyofanywa na uongozi uliopita, kisha kushirikiana
na wadau wengine kuwa sehemu ya mapambano ya kuhakikisha nchi yetu inakuwa na
sheria bora zinazosimamia tasnia ya habari, ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari,
hadhi ya wanahabari na haki ya kupata taarifa.
Imetolewa leo Alhamis, Februari 4, 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment