Wednesday, June 22, 2016

CCM NA UKAWA NGUMI JIWE,HII NI MPYA LEO

Viongozi wa Bavicha wakizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani
Viongozi wa Bavicha wakizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani





 MAMBO yanazidi kwenda mrama kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Dani Tibason.

Msimamo uliotolewa na Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) unaakisi mwanzo mpya wa msuguano wa kisiasa nchini.

Tayari Bavicha wametangaza msimamo wa kutoshirikiana na vijana wa CCM katika tukio la aina yoyote.

Mbali na kutangaza msimamo huo pia wametangaza kuzuia mikutano yote ambayo itaandaliwa na CCM kama inavyozuiwa ya Chadema.

Msimamo huo umetolewa leo na Julius Mwita, Katibu Mkuu wa Bavicha wakati akizungumza na waandishi wa habari Dodoma.
Mwita amesema, kutokana na kitendo cha Serikali ya CCM kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya Chadema kinaonesha wazi kuwa, serikali ina mpango wa kuhakikisha inaua upinzani jambo ambalo haliwezi kukubalika.

Amesema, kutokana na hali hiyo kwa sasa Bavicha wametangaza kutoshirikiana na vijana wa CCM katika mazingira yoyote ikiwa ni pamoja na katika masomo, nyumba walizopanga, misiba na katika majamga mengine mbalimbali.
“Kutokana na kuwepo kwa vitendo vya kikatili vinavyofanywa na Serikali ya CCM vya kuzuia mikutano ya upinzani, sasa tunatangaza sisi vijana wa Bavicha hatutashirikiana na wanachama wa CCM kwa njia yoyote ya kijamii wala kimaendeleo.

“Natangaza kwa vijana wote wa Chadema hatutashiriki katika mazizi, hatutashiriki kusoma nao wale waliopo katika vyuo, hatutashiriki sherehe mbalimbali zinazowahusu wao wala hatutashiriki katika jambo lolote la kimaendeleo, na hii ni msimamo wetu.

“Pia tunawapongeza wabunge wetu kwa kususia shughuli zote za ambazo zinafanywa na CCM kwani kwa kufanya hivyo inaonesha kuwa sasa tumechoka na uongozi wa kiimla,” amesema Mwita.

Hata hivyo amedai, Rais John Magufuli ni muoga kuliko marais wote kwa kuwa ni rais ambaye hapendi kukosolewa na kuambiwa ukweli pale ambao amekuwa akikosea jambo ambalo anatakiwa kujitafakari na kujikosoa.

“Sasa vijana vijana tumejipanga kuhakikisha Jeshi la Polisi linazuia mikutano au mikusanyiko ambayo inafanywa na CCM na ikumbukwe kuwa, 23 Julai mwaka huu CCM watakuwa na vikao vya kumkabidhi rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa CCM.

“Sasa tunataka Jeshi la Polisi kuzuia mkusanyiko huo na kama haitawezekana vijana wa Chadema na Ukawa watazui mikutano hiyo.

“Haiwezekani mikutano ya Chadema ikawa ndiyo inayozuiliwa wakati mikutano na mikusanyiko ya CCM inaendelea kufanyika, jambo hili kamwe haiwezi kukubalika na tunasema sasa imefika mwisho wa uvumilivu,” amesema Mwita.

Edward Simbeye, Katibu Mwenezi Bavicha amesema, yeye ndiye mratibu wa mahafali za wanafunzi wa Chadema vyuo vikuu (Chaso) nchini hivyo polisi walipaswa kumkamate yeye na si kuzuia mahafali hayo.

No comments: