Wednesday, June 8, 2016

TAAARIFA ZOTE MUHIMU KUTOKA TFF LEO ZIKO HAPA


MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA KESHI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kocha Mkuu wa zamani wa Nigeria, Stephen Okechukwu Keshi (54) kilichotokea ghafla leo Juni 08, 2016 kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa.

Kutokana na kifo hicho, Rais Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Amaju Pinnick, familia ya marehemu Keshi pamoja na ndugu, jamaa, marafiki walioguswa na msiba huo wa gwiji huyo aliyepata kuwa nahodha wa kikosi cha Taifa Nigeria ‘Super Eagles’.

Katika rambirambi ambazo zimefika pia katika Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Rais Malinzi amesema kuwa japokuwa Keshi ametangulia mbele za haki, mchango wake kwenye mpira wa miguu hautasahaulika kwani atabaki kuwa alama ya maendeleo ya mchezo wa soka.


SERENGETI BOYS KAMBINI JUNI 13, 2016

Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inataingia kambini Juni 13, 2016 kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa Shelisheli utakaofanyika Juni 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa marudiano kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.

Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.

Kadhalika Serengeti Boys ilicheza mfululizo michezo saba  ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.

Katika mashindano ya AIFF, timu hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki katika jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika hatua za juu katika mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani CONCACAF (USA) na AFC (India, Korea na Malaysia).

Haishangazi nchi nyingi za Ulaya, Asia na Marekani zimeulizia uwezekano wa timu hii kutembelea nchi zao kwa michezo ya kirafiki.

Awali timu ya Serengeti Boys ilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kwa sababu ya rekodi zilizokuwa zinaiweka Tanzania katika viwango vya chini katika umri huo kwa nchi za Afrika Magharibi na Kaskazini zilikuwa juu zaidi na vilevile ukweli wa kwamba timu kama USA, Korea, Malasyia na India zilikuwa na bajeti kubwa iliyogharamiwa na Serikali zao na walikuwa na vifaa vya kila namna kiasi cha kuomba magari kwa ajili ya vifaa vya mazoezi na mechi.

Serengeti Boys ilimaliza Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao 3-0. Serengeti Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na awali walipokutana walitoka sare ya 2-2.


TFF YAANZA KUTOA FOMU ZA LESENI KWA KLABU  

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeanza kutoa fomu za Leseni za Klabu (Club Licensing) za Ligi ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na zile za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes.

Klabu hizo zitatumiwa fomu hizo na kutakiwa kuzijaza na kuzirejesha kabla ya Juni 19, mwaka huu ikiwa ni siku 10 mara baada ya Bodi ya Ligi ya TFF (TPLB) kuwatuamia fomu hizo. Klabu itakayojaza fomu hizo kwa wakati ndiyo ambayo maombi yake ya leseni yatashughulikiwa mapema.

Tayari TFF imeteua Kamati ya Leseni ya Klabu (Club Licensing Committee) ambayo ndiyo yenye jukumu la kupitia maombi ya leseni kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza na kutoa uamuzi wa kuzikubali au kuzikataa kwa kuzingatia Kanuni ya Leseni ya Klabu.

Wajumbe walioteuliwa kwenye Kamati hiyo inayoundwa kwa mara ya kwanza ni Wakili Lloyd Nchunga (Mwenyekiti), Wakili Emmanuel Matondo (Makamu Mwenyekiti), David Kivembele, Hamisi Kissiwa na Prof. Mshindo Msolla.

Klabu zinatakiwa kuchukua fomu za maombi TFF ambapo baada ya kuzirejesha zitafanyiwa kazi ambapo zile zitakazokuwa zimekidhi matakwa ya Kanuni husika zitapatiwa leseni husika ili zishiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kwa msimu wa 2016/2017.

Kwa klabu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya leseni yanayolenga kuhakikisha mpira wa miguu unaendeshwa kwa weledi na kupiga vita upangaji matokeo katika maeneo matano ya wachezaji (sporting), viwanja (infrastructure), utawala (administrative and personnel), umiliki wa klabu (ownership) na fedha (financial), hazitapa leseni hivyo kutokuwa na sifa ya kushiriki ligi.

Klabu ambazo zitanyimwa leseni na kutoridhika na uamuzi huo, zitakuwa na fursa ya kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya 5(3) ya Kanuni ya Leseni ya Klabu ya TFF, Kamati hiyo ndiyo itakayosikiliza rufani zinazopinga uamuzi wa Kamati ya Leseni ya TFF.



IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: